Na Mwandishi wetu, Timesmajira Online
KATIKA kuendelea kuwafikia wakulima shirika lisilo la kiserikali la Kilimo Endelevu (SAT), limezindua awamu ya pili ya mradi wa Jarida la Mkulima Mbunifu ili kuhakikisha kila mdau anaweza kushiriki kikamilifu katika uchapishwaji wa taarifa.
Hayo yamebainishwa mkoani Dodoma wakati wa uzinduzi wa mradi wa pili wa mkulima mbunifu unaofadhiliwa na shirika la Biovision Foundation ambapo wadau mbalimbali waliweza kushiriki wakiwemo, wakulima, wadau wa maendeleo pamoja na taasisi mbalimbali za kijamii.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi wa shirika la SAT Tanzania, Janeth Maro amesema awamu ya pili mradi huo itakuwa shirikishi na kuhakikisha taarifa zinazotolewa zinalenga mahitaji ya wakulima.
“Awamu ya pili ya mradi huu umelenga zaidi kufanya ushirikishwaji kwa wadau mbalimbali kwa lengo kuhakikisha wanashiriki katika uchapishwaji wa taarifa katika jarida ili taarifa zinazotolewa zinalenga mahitaji ya wakulima,”amesema.
Amesema kuwa jarida la mkulima mbunifu limesaidia katika kupunguza uhaba wa taarifa za kilimo kwa wakulima.
“Kupitia Jarida la Mkulima Mbunifu limesaidia kupunguza uhaba wa habari kwa wakulima na kuhakikisha wanaweza kupata taarifa sahihi zinazohusiana na kilimo na rafiki ambapo sasa wanaweza kuleta taarifa zao na matokeo ya namna walivyoweza kutumia mbinu na hatimaye kupata mafanikio jambo ambalo limekuwa likileta hamasa kwa wakulima wengine,”amesema.
Aliongeza kuwa katika awamu ya pili ya mradi huo wameongeza idadi ya kurasa ili kuongeza wigo wa habari zinazochapishwa katika jarida.
Aidha amewashukuru washirika wa mradi huo na kueleza kuwa awamu ya pili ya mradi huo utaweza kuleta matokeo chanya yenye tija kwa wakulima na kilimo kwa ujumla.
Kwa upande wake Mgeni rasmi katika hafla hiyo, Mkurugenzi Msaidizi wa Ugani Wizara ya Kilimo, Upendo Mndeme amesema jarida la mkulima mbunifu ni njia ya mawasiliano katika kilimo.
Amesema sekta ya kilimo ni miongoni mwa sekta yenye watu wengi ambao wameweza kujiajiri hivyo ipo haja ya kuwa na kilimo biashara.
” Tukifanya kazi ipasavyo kwa kushirikiana kupitia jarida la mkulima mbunifu tutaweza kuwafikia wadau wengi na tunapaswa kuzingatia kilimo kinachotunza mazingira ili kuwa na mavuno endelevu,”amesema.
Aliongeza kuwa ni jukumu la wataalamu kuelimisha jamii kutambua kuwa wanapaswa kufanya kilimo cha biashara.
Hata hivyo aliwaomba waofisa ugani kuhakikisha wanatekeleza wajibu wao kikamilifu katika maeneo yao ili kuweka alama inayoonesha kuna bwana shamba katika eneo hilo.
“Serikali imeanza kuweka mkazo katika kuimarisha huduma za ugani na pia ni kipaumbele cha Wizara hivyo nawaomba maofisa ugani onesheni juhudi zinazoonekana katika maeneo yenu ya kazi kwa kutumia vitendea kazi kwa ufanisi,”amesema.
Aidha Ofisa Kilimo Mkuu kutoka Tamisemi, Hoffu Mwakaje amesema serikali imekuwa ikitambua mbinu ambazo zimekuwa zikifanywa na wadau ambapo kupitia shirika la SAT watu mbalimbali wameweza kujifunza kilimo endelevu.
Meneja mradi wa mkulima mbunifu, Erica Rugabandana amesema mradi huo ni mawasiliano kwa ajili ya wakulima na umelenga kutoe elimu ya kilimo hai.
Amesema kupitia mradi huo kumeweza kuwa na mafanikio mbalimbali ambapo kwa kila mwezi wamekuwa wakisambaza kopi 15000.
More Stories
Jokate awapa tano vijana UVCCM maandalizi Mkutano Mkuu wa CCM
Watakaokwamisha mapato Kaliua kukiona cha moto
Dkt.Gwajima aagiza kuundwa kamati za ulinzi wa watoto