Na Judith Ferdinand, Timesmajira Online-Mwanza
Madiwani wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela,mkoani Mwanza wametakiwa kudumisha na kuhamasisha amani,ili kuwa na taifa lenye utulivu na kuweza kuwaletea wananchi maendeleo.
Wito huo umetolewa Desemba 2,2025 na Diwani wa Kata ya Buswelu,Sara Ng’hwani,mara baada ya kutangazwa kuwa Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela kwa kipindi cha miaka mitano(2025-2030).

Zoezi hilo ambalo limefanyika kipitia mkutano wa kwanza wa Halmashauri ambao umehusisha Madiwani kula viapo,uchaguzi wa Meya, Naibu Meya na wajumbe wa kamati za kudumu,kuunda kamati za kudumu za Halmashauri.
Pia kupitisha ratiba ya vikao vya halmashauri na kamati za kudumu pamoja na kupokea taarifa ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya utekelezaji wa shughuli za halmashauri zilizofanyika kipindi ambacho Baraza la Madiwani lilivunjwa.
Sara,alikuwa mgombea pekee katika nafasi hiyo kwa kupata kura zote za ndiyo,27,ambapo Diwani wa Viti Maalum(CCM),Kuluthum Abdallah amechaguliwa kwa kura 23 kuwa Naibu Meya wa Halmashauri hiyo kati ya kura 27 zilizopigwa huku mpinzani wake katika nafasi hiyo Diwani wa Kata ya Kitangiri(ACT-Wazalendo)Donald Ndalo akipata kura 4.
Akizungumza mara kutangazwa kuwa Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela,Sara Ng’hwani,amewasisitiza madiwani hao kwenda kudumisha amani ya Tanzania,umoja, mshikamano na upendo.
Kwani amani ndiyo kila kitu,ikikosekana hata hizi huduma ambazo wananchi wanapaswa kuzipata hawatazipata.
“Niombe tukahamasishe amani,bila amani tutakimbia miji yetu, viongozi wa dini tuzungumze na waumini wetu kuhusu amani,kwa kufanya hivyo tutatekeleza mambo ambayo wananchi wetu wametuagiza,”amesema Sara.

Sanjari na hayo Sara ametumia fursa hiyo kuwashukuru madiwani hao kwa kumpigia kura huku akiwasisitiza kukaa na wananchi katika ofisi zao kuwasikiliza, kutatua matatizo yao,kuwasaidia pamoja na kusimamia vyema miradi.
“Asante kwa kura zote za ndiyo,kura zenu hazijapotea naimani Mungu atatenda,nawahidi kwamba hamkufanya kazi bure,”amesema Sara.
Naibu Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela,Kuluthum Abdallah,amesema watashirikiana na Mstahiki Meya,Madiwani wenzake chama na Serikali kuhakikisha wananchi wanapata maendeleo na amani inatawala.
Akizungumza katika uzinduzi wa Baraza jipya la Madiwani, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela,Ummy Wayayu,amewataka viongozi hao kufanya kazi kwa ushirikiano bila kujali tofauti za vyama.
“Manispaa inaweza kusonga mbele endapo tutashirikiana na kutanguliza maslahi ya wananchi,”amesema Wayayu.


More Stories
Bilioni 7 kuwainua vijana 308 sekta ya uvuvi
Clara:Miaka 50 ya Sabasaba fursa mpya za Biashara na Uwekezaji
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako