
Na. Israel Mwaisaka, Sumbawanga
Wadau wa maendeleo ndani na nje ya mkoa wa Rukwa wamehamasishwa kuchangia upatikanaji wa madawati kwa ajili ya kuwezesha watoto kusoma kwenye mazingira wezeshi kwa ustawi wa taaluma.
Wito huo umetolewa hivi karibuni na Mbunge wa Jimbo la Kwela ambaye pia ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano Deus Sangu wakati alipokabidhi madawati kwa shule za msingi katika jimbo hilo alipofanya ziara ya kikazi.
Katika ziara hiyo sangu alikabidhi madawati zaidi ya 100 kwa shule za msingi sita (6) yenye thamani ya shilingi Milioni 60 ambayo ameyapata kupitia ufadhili ya Benki ya Taifa ya Biashara (NBC).
Waziri Sangu akizungumza kwenye moja ya mikutano yake na wananchi wa kijiji cha Nankanga tarafa ya Kipeta na kijiji cha Ilemba alisema ametoa msaada huo kuunga mkono jitihanda za wananchi katika kuchangia maendeleo ya elimu.
“ Nimekuja hapa kukabidhi zawadi ndogo kwa Watoto.Leo nimewaletea madawati 20 ambapo yatasaidia Watoto 60 kutoendelea kukaa chini” alisema Waziri Sangu.
Mbunge huyo aliongeza kuwaambia wananchi kuwa yeye ni mbunge wa vitendo na kwamba anapenda vitu vinavyoonekana ambapo aliitumia fursa hiyo kushukuru uongozi wa Benki ya NBC kwa kuguswa na shida za wanaKwela .

“Ninashukuru benki ya NBC kwa msaada wao waliotupatia madawati haya yanayokwenda kupunguza tatizo la watoto kukaa chini. utatuzi huu wa kero za wananchi ni sehemu ya maelekezo tuliyopewa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwetu wabunge” alisema Sangu alipoongea na wananchi wa Kijiji cha Msia kata ya Milepa huku akitoa wito kwa wadau wengine wa maendeleo kuchangia madawati kwa ajili ya jimbo la Kwela.
Miongoni mwa shule zilizopokea madawati hayo na idadi yake kwenye mabano ni shule ya msingi Kalumbaleza (20), Msia (20), Kimambo (15), Ilemba (20) , Nankanga (20) na Deusi Sangu sekondari madawati (30).
Akizungumza kwa niaba ya wananchi, Diwani wa kata ya Mwadui Mahmood Leonce Mgweno alisema amepokea madawati toka Ofisi ya Mbunge na kwa tayari amefikisha shuleni na kumpongeza Mbunge Sangu kwa msaada.
Nao wananchi wametumia fursa ya ziara ya mbunge Sangu kueleza kufurahishwa kwao na jitihada anazozifanya kuchangia maendeleo ya jimbo hilo ikiwemo msaada wa madawati.
Nae Thomas Nsandale ameishukuru Ofisi ya Mbunge kwa kuwezesha wa upatikanaji wa madawati ikiwa ni miongoni mwa vingi walivyopatiwa katika kipindi chote Mhe.Sangu akiwa Mbunge wa Jimbo la Kwela
“Sangu amefanya mambo mengi ambayo yanatufanya sisi wananchi kutokupunguza upendo juu yake na tunamuomba pia Madawati haya yasiwe ya mwisho kwa wananchi wake wa Kwela Bali iwe sababu ya muendelezo wa Maendeleo haya” amesema Nsandale.
Waziri Sangu alikuwa jimboni Kwela wilaya ya Sumbawanga kukagua shughuli za maendeleo pamoja na kuzungumza na wananchi.

More Stories
Madiwani waagiza ziara ya dharura mgodini kisa mapato
Mwalimu auawa akizuia mifugo kupitia eneo la shule
Polisi Mbalizi wachangia damu kuimarisha huduma za afya