December 22, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Sangu ajibu swali kwa mara ya kwanza ,amshukuru Rais Samia


Na Joyce Kasiki Dodoma

NAIBU Waziri Ofisi ya Rais,Menejimenti wa Utumishi na Utawala Bora Deus Sangu amesimama kwa mara ya kwanza Bungeni kujibu maswali ya wabunge tangu alipoteuliwa na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan huku akimshukuru Rais kwa kumuamini katika nafasi hiyo na kuahidi kuitumikia kwa uadilifu na uchapakazi kwa maslahi mapana ya wananchi na Taifa kwa ujumla.

Aidha amemshukuru Spika wa Bunge Dkt.Tulia Ackson kwa uongozi wake na malezi yake kwa wabunge lakini pia amewashukuru wananchinwa jimbo la Kwela na kuahidi kuendelea kuwatumikia na kutanguliza waliyomtuma Bungeni.

Sangu ametoa shukrani hizo wakati akijibu swali la Mbunge wa Nachingwea Amandus Chinguile (CCM) ambaye alitaka kujua kama serikali haioni haja  ya kuanzisha mfumo utakaowezesha kupata idadi sawa ya nafasi za ajira katika kila Jimbo kuliko mfumo wa sasa.
Akijibu swali hilo,Sangu amesema “Kwa Mujibu wa Sera ya Menejimenti na Ajira katika Utumishi wa Umma ya mwaka 2008, Toleo la  pili Aya ya 4.2, nafasi za Ajira hutolewa kwa ushindani na kwa kuzingatia sifa stahiki kwa mujibu wa Miundo ya Maendeleo ya Utumishi ya kada husika.

Vile vile amesema,nafasi wazi za ajira hutolewa kwa kuzingatia Ikama ya Watumishi katika Taasisi husika ambayo inajumuisha mahitaji halisi yaliyopo katika Taasisi husika. 

” Kwa mujibu wa hati idhini inayoanzisha kila Taasisi, mahitaji ya watumishi ya Taasisi moja hutofautiana na ya Taasisi nyingine kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ukubwa wa Taasisi na wingi wa majukumu. “amesema Sangu

Aidha,Naibu Waziri huyo amesema , idadi ya Taasisi za Umma zinatofautiana kwa kila Jimbo. Kwa msingi huo, idadi ya nafasi za ajira hutofautiana kati ya Jimbo moja na jingine.

“Kutokana na maelezo hayo, katika mwaka wa Fedha 2023/2024, Serikali imetoa kibali cha nafasi 47,404 za Ajira mpya kwa waajiri wote ambapo kila mwajiri katika kila jimbo amepata nafasi kwa kuzingatia Ikama ya Watumishi katika maeneo hayo. “Amesisitiza

Ameongeza kuwa “Aidha, katika kutekeleza kibali hicho, Serikali kupitia Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma imetangaza nafasi katika kada za Elimu na Afya kimkoa na usaili utafanyika katika ngazi ya mkoa.”