-Avipa mbinu vyombo vya habari ya kuviwezesha kufanyakazi
kwa uhuru
-Serikali yake yaanza mazungumzo ujenzi setelaiti
Na Jackline Martin, TimesMajira Online
RAIS Dkt. Samia Suluhu Hassan amevitaka vyombo vya habari nchini mbali na kuwa huru kusema na kuandika, vifuate mila na desturi za nchi .
Alisema kama vyombo vya habari vinataka kuwa huru ni lazima viweze kujiendesha na kujitegemea vyenyewe. Rais Dkt. Samia aliyasema hayo jana uzinduzi wa mradi wa minara ya kurusha matangazo ya Televisheni ardhini (DTT) inayomilikiwa na kampuni ya Azam Media
Alisema Serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi kuhakikisha uendelevu wa sekta ya habari kwa upande wa teknolojia ya utangazaji unakua.
“Uhuru maana yake ni kujiweza wewe mwenyewe kujiendesha na kujitegemea, ndipo utakuwa huru, lakini kama unataka kuwa huru kusema kisha unarudi serikalini tubebe tusaidie ili tuweze kusema hapana uhuru hapo, hivyo kama vyombo vya habari vinataka kuwa huru viweze kujiendesha vyenyewe”
Aidha Rais Dkt. Samia aliwataka wadau wote wa habari kuendelea kufanya kazi kwa ukaribu na Serikali ili waiwezeshe nchi kufikia malengo tarajiwa katika eneo hilo.
Kuhusu Mradi wa DTT, Rais Dkt. Samia alisema ni uwekezaji mkubwa sana kwa Taifa la Tanzania ambao unakwenda sambamba na utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi ibara ya 125 inayosema kuhakikisha sekta ya habari inaboreshwa ili kuongezea wananchi fursa ya kupata Habari kwa kuongeza wigo wa upashanaji wa Habari.
“Niwasihi muendeleze kuwekeza ila wananchi wote waweze kunufaika na matokeo ya uwepo wa miundombinu hii”
Rais Dkt. Samia alisema Mei 13, mwaka huu alizindua minara 758 inayokwenda kujengwa na makampuni za simu nchi nzima , lakini pia minara zaidi ya 300 inayopanda kutoka 2G kwenda 3G hadi 4G, lakini pia minara mipya inayokwenda kujengwa itapanda hadi 5G hivyo Tanzania inazidi kufika mbali sana kutokana na kazi kubwa inayofanywa na serikali ya awamu ya 6.
Wakati huo huo, Rais Samia Suluhu Hassan amesema Serikali yake imeanza mazungumzo kwa ajili ya ujenzi wa satelite.
Endapo mpango huo utakuwa dhahiri, Tanzania itakuwa miongoni mwa nchi za Afrika zilizofanikiwa kupeleka kifaa hicho angani, ambazo ni Algeria, Ethiopia, Kenya, Zimbabwe, Afrika Kusini, Morocco, Misri, Ghana na Nigeria, huku Rwanda ikikusudia kufanya hivyo mwishoni mwa mwaka huu.
Hata hivyo, Rais Samia ameoneka kutofurahia ujenzi wa minara ya mawasiliano unaoendela nchini huku akishauri kuangaliwe namna bora ambayo kwayo nchi inaweza kukusanya mambo yote kwa pamoja bila kuwa na mambo mengi.
“Tatizo nililonalo kichwani kwangu ni moja, nikamuambia Waziri, minara 758 mipya, kuna minara ambayo tayari ipo ndani ya nchi, kuna minara ya Azam Media itakwenda kujengwa na wengine watakuja na minara,” alisema.
Kwa mujibu wa Rais Samia, hali hiyo ya uwepo wa minara mingi ilimfanya kumhoji Waziri mhusika ili kujua kama kunawezakuwa na teknolojia mbadala.
“Nikamuuliza Waziri hakuna teknolojia ya kuchanganya haya yote yakaingia sehemu moja, kwa sababu nchi yote itajaa minara, kila utakapokwenda minara, minara, ukiuliza huu wa wa Azam, Tigo na huu wa Voda, nchi yote itajaa minara,” amehoji Rais Samia.
Alisema ni vyema kama nchi ikatafuta teknolojia itakayoweza kuchanganya vyote kwa pamoja.
“Najua kama Serikali tunajipanga kuja na setelaiti ambayo niwahakikishie kuwa itakuwepo Tanzania, tunajipanga vizuri tumeanza mazungumzo tutajenga setelaiti Tanzania.”
Alisema wakati hilo likifanyika ni vyema kuangalia namna ya kukusanya mambo yote na nchi ikapata huduma zote kwa moja bila ya kuwa na mambo mengi yamesimama.
Kwa upande wake Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye, alisema sekta ya habari imeendelea kukua na vyombo vimeongezeka sana kwa sasa kuna ongezeko la vituo Vya kurusha matangazo ya redio kutoka 210 mwaka 2022 hadi 218 April 2023 sawa na ongezeko la asilimia 2, vituo vya televisheni vimeongezeka kutoka 56 mwaka 2022 hadi 68 Aprili 2023 sawa na ongezeko la asilimia 16, cable televisheni 57, televisheni mtandao 413, magazei 284 hadi 321
More Stories
Waziri Jerry afanya uteuzi wa Makamu Mwenyekiti, Wajumbe watano wa bodi ya Shirika la Posta
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa