Na Penina Malundo, timesmajira
RAIS Samia Suluhu Hassan, amezidi kukoleza uwekezaji kwenye Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) baada ya ndege mpya aina Boeing 737-9 Max iliyonunuliwa nchini Marekani, kuwasili nchini.
Ndege hiyo inafanya Shirika hilo kuwa na ndege 14 huku zingine zikiwa hatua mbalimbali za utengenezwa.
Ndege hiyo iliwasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere, jana mchana na kupokelewa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kwa niaba ya Rais Samia Suluhu Hassan.
Akizungumza kwenye hafla hiyo Waziri Mkuu Majaliwa ameitaka Wizara ya Uchukuzi kusimamia ipasavyo ATCL ili kuhakikisha uwekezaji mkubwa uliofanywa unaleta matokeo chanya na kuwa kichocheo cha ukuaji wa sekta nyingine mtambuka na uchumi kwa ujumla wake.
Amesema kuwa ongezeko la ndege na huduma za usafiri inasaidia kuongeza fursa za biashara kati ya Tanzania na mataifa mengine, kuongeza upatikanaji wa fedha za kigeni na kuongeza idadi ya watalii wanaokuja nchini.
Aidha, Majaliwa ametoa maelekeza saba ikiwemo za kuendelea kuikuza sekta ya anga nchini, Wizara ya Uchukuzi iandae mpango wa kuongeza wataalamu wazalendo katika fani zinazohusu masuala ya ndege hususan katika eneo la matengenezo na urubani.
Kadhalika, Majaliwa amewataka watumishi wa Shirika la Ndege Tanzania kuongeza uzalendo na kuwafichua wale wote wenye nia ya kulihujumu shirika hilo pamoja na kudhibiti upotevu wa mapato kupitia tiketi na mizigo.
Pia, Amewataka viongozi na watendaji wa Shirika hilo wahakikishe ndege zote zinaendeshwa kwa tija kwa kufanya tafiti za kutosha wa masoko kabla ya kupeleka ndege.
Amesema kuwa usafiri wa anga umekuwa chachu ya kuongeza mnyororo wa thamani wa mazao ya kilimo na biashara. “Uwepo wa usafiri wa ndege umeongeza tija kubwa kwa wakulima hususan wa mazao ya mbogamboga na matunda, wafugaji na wafanyabiashara wa Kitanzania”
Katika Hatua nyingine, Majaliwa amesema katika kipindi cha uongozi wa Serikali ya awamu ya sita imesaini mikataba ya miradi mipya 6 yenye thamani ya sh. Bilioni 674.3 inayohusu ujenzi wa kiwanda cha kujengea meli (shipyard) katika Ziwa Tanganyika, ujenzi wa meli kubwa ya kubeba mizigo tani 3,500 na meli nyingine yenye uwezo wa kubeba tani 3,000 za mizigo ambayo inajengwa katika Ziwa Victoria.
Kwa upande wake, Waziri wa Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa amesema kuwa sambamba na ununuaji wa ndege za abiria na moja ya mizigo, Serikali imenunua ndege mbili za mafunzo kwa ajili ya Chuo cha Usafirishaji (NIT) ili kusaidia kuongeza idadi ya marubani kwenye soko la ajira na kupunguza uhaba wa marubani nchini.
“Pia NIT iliwezesshwa mitambo na vifaa vya kisasa kwa ajili ya kutoa mafunzo ya shahada na Stashahada ya uhandisi wa ndege ili kuzalisha wahandisi na mafundi mchundo watakaoingia kwenye soko la ajira,”amesema.
Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL) Mhandisi Ladislaus Matindi, amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuijengea kampuni hiyo uwezo wa kutoa huduma kwa kuinunulia ndege mpya na kuijengea miundombinu wezeshi katika biashara ya anga.
“Hadi sasa Serikali imewekeza sh.trilioni 2.4 katika ununuzi wa ndege, ujenzi wa mindombinu wezeshi ya kibiashara pamoja na ulipaji wa sehemu ya madeni yaliyolimbikizwa”amesema
Ameongeza kuwa ATCL inaendelea kutekeleza mpango mkakati wake wa pili wa miaka mitano ulioanza mwaka wa fedha 2022/23 na kumalizia 2026/27 ambao pia unahusisha mpango wa maendeleo wa Taifa wa miaka mitano yaani 2021/22-2025/26 ambao unatarajiwa kuiwezesha ATCL kuwa na ndege 20 “Hadi sasa ATCL inandege 14 zilizonunuliwa katika kipindi cha ufufuaji”
More Stories
CCM Tabora yamfariji mjane wa kada anayedaiwa kujiua
FDH yaanza kutekeleza mradi wa kuwajengea uwezo wanawake wenye ulemavu
Airtel yatoa zawadi kwa wateja wake