November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Samia afanya kufuru, wawekezaji wafurika


-Uongozi wake wawezesha TIC kusajili miradi ya USD bil. 3.16 kwa miezi mitano itakayozalisha ajira 21,297.

-Ni rekodi mpya kuandikwa

Na Jackline Martin, TimesMajira Online

SERIKALI ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, imevunja rekodi kwa kusajili miradi ya uwekezaji 132 katika kipindi cha Julai hadi Novemba 2022.

Miradi hiyo ni sawa na ongezeko la asilimia 22.2 ikilinganishwa na miradi 108 iliyosajiliwa katika kipindi hicho hicho mwaka 2021.

Matokeo ya ongezeko kubwa la kusajiliwa miradi mingi ya uwekezaji inaelezwa na wachumi kuwa linatokana na uamuzi wa Rais Samia kuboresha mazingira ufanyaji biashara na uwekezaji nchini Tangu ashike wadhifa huo, Machi 19, 2021.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TIC, John Mnali , alisema sababu za ongezeko kubwa la miradi iliyosajiliwa na TIC linatokana na jitihada za Serikali za kutangaza fursa mbalimbali za Uwekezaji zilizoko hapa nchini kupitia ziara mbalimbali za viongozi wa kitaifa nje ya nchi pamoja na juhudi za Serikali katika kuboresha mazingira ya uwekezaji nchini.

Tangu alipoingia madarakani Rais Samia amekuwa akiwataka watendaji wa Serikali kuhakikisha wanaweka mazingira muafaka kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi ili kustawisha uchumi wa nchi hiyo.

Mfano, wakati Rais Samia akizungumza mara baada ya kuwaapisha makatibu wakuu wa wizara mbalimbali na manaibu wao, alisema licha ya Tanzania kutangazwa kuingia kwenye uchumi wa kati mwaka uliopita, Rais Samia alisema hali ya kiuchumi bado ni ngumu kutokana na wawekezaji wengi kuamua kuhamisha biashara zao katika mataifa mengine kufuatia kile alichokitaja kuwa ni urasimu na unyanyasaji wa baadhi ya watendaji serikalini.

Rais Samia mara kadhaa amekuwa akiweka wazi kuwa Tanzania inawahitaji zaidi wawekezaji kuliko wao wanavyohitaji kuwekaza katika nchi hii.

Akitilia mkazo hoja yake ya kurahisisha mazingira ya uwekezaji, Rais Samia aliitaka ofisi ya waziri mkuu, kuhakikisha wanaondoa urasimu katika mchakato wa kutolewa kwa vibali vya kazi kwa wawekezaji na kuwataka kuacha mara moja kuwalazimisha wawekezaji kuajiri wafanyakazi wa kitanzania kwani wanao uhuru wa kuchagua wa kufanya nao kazi.

Rais Samia ataka watendaji kuhakikisha wanaondoa urasimu katika mchakato wa kutolewa kwa vibali vya kazi kwa wawekezaji
Tanzania.

Maelekezo hayo ya Rais Samia yamejibu kwa kasi kutokana na kile ilichothibitishwa na Mnali kwamba TIC imesajili jumla ya miradi 132 sawa na ongezeko la asilimia 22.2 ikilinganishwa na miradi 108 iliyosajiliwa katika kipindi hicho hicho mwaka 2021.

Mnali alisema kati ya miradi hiyo, miradi ya 50 inamilikiwa na wageni wakati Miradi 30 inamilikiwa na Watanzania na miradi 52 inamilikiwa kwa ubia kati ya Watanzania na wageni (Joint ventures).

“Miradi hii ina jumla ya thamani ya Dola za Kimarekani bilioni 3.16 na inatarajiwa kutoa ajira 21,297,” alisema Mnali.

Kwa mujibu wa Mnali mgawanyo wa miradi iliyosajiliwa katika kipindi hiki unaonesha kuwa Sekta ya Viwanda iliweza kuongoza kwa kuvutia miradi mingi (67), ikifuatiwa na Sekta ya Usafirishaji miradi 25 , Utalii miradi 12 , Kilimo 9, Huduma 8 , Majengo ya Biashara 7 , Rasilimaliwatu 3 na Sekta ya Fedha mmoja.

Mnali alieleza kwamba thamani ya miradi (USD bilioni 3.16) iliyosajiliwa katika kipindi cha Julai – Novemba 2022 imeongezeka kwa asilimia 259 ikilinganishwa na thamani ya miradi (USD milioni 881) iliyosajiliwa katika kipindi cha Julai – Novemba 2021.

Vilevile, Mnali ilieleza kwamba kiwango cha ajira kinachaotarajiwa kutokana na miradi iliyosajiliwa Julai – Novemba 2022 kimeongezeka kwa asilimia 57 kutoka ajira 13,578 (Julai – Novemba 2021) hadi ajira 21,297 (Julai – Novemba 2022).