December 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Samia afanikisha muafaka Kariakoo

Na Jackline Martin, TimesMajira,OnlineDar

UAMUZI wa Rais Samia Suluhu Hassan kuwatuma wasaidizi wake wakiongozwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Waziri wa Fedha na Pipango, Mwigulu Nchemba, Waziri wa Biashara, Viwanda na Uwekezaji, Ashatu Kachwamba Kijaj na Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) umetoa nafasi kwa wafanyabiashara wa soko la Kariakoo kueleza dukuduku lao na mwisho kutoka na muafaka kwa kukubaliana kuendelea na biashara.

Mara baada ya kikao chao cha jana chini ya Waziri Mkuu wafanyabiashara hai waliafiki kusitisha mgomo baada ya Serikali kutanganza kuunda Tume ya watu 14 kutoka Serikalini na wawakilishi wa wafanyabiashara kwa ajili ya kufanyia kazi yale yaliyowasilishwa na kupendekezwa na wafanyabiashara hao.

Aidha, Serikali imetoa maelekezo tisa ikiwemo kusitisha kabisa shughuli zilikuwa zikifanywa na Task Force (kikosi kazi) kilichokuwa kimeundwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa ajili ya kufanikisha ukusanyaji mapato.

Uamuzi huo ulifikiwa jana kwenye mkutano baina wafanyabiashara na viongozi wa Serikali walioongozwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, uliofanyika Anatoglou jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na wafanyabiashara hao baada ya kusikiliza dukuduku zao, Majaliwa alisema Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuthamini sekta ya biashara amefungua milango ya kufanyika biashara na malengo hayo yameanza kufanikiwa.

Alisema hoja zote zilizotolewa kwenye kikao cha jana wanaendelea kuzifanyia kazi, lakini zitafanyiwa kazi kwa mfumo shirikishi na kazi hiyo siyo ya Serikali peke yake.

Alisema ili kufanikisha hillo ni lazima kuwe na Tume ya pamoja na kukumbushana yale waliokubaliana na yale yatakayosaulika ili yaweze kufanyiwa kazi.

Muundo wa Tume

Akitangaza Tume hiyo, Waziri Mkuu Majaliwa alisema itakuwa na wajumbe 14, ambapo saba watatoka Serikalini na saba kutoka miongoni mwa wafanyabiashara.

“Lengo ni kufanyia kazi yaliyosemwa leo na yale ambayo hayatakuwa yamesahaulika,” alisema Majaliwa na kuongeza;

“Yaliyosemwa yote yatachakatwa na mrejesho mtapewa.” Kwa upande wa Serikali Majaliwa alisema amemteua Katibu Mkuu wake, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha.

Wengine ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo Jamii, jinsia na Makundi Maalum na Katibu Tawala wa Dar.

Aidha, alisema Mtendaji Mkuu wa TRA na Tafiti naye atakuwa moja anainia ndani ya tume hiyo. Pia Kamishna wa Kodi za ndani mmoja wa wajumbe wa Tume.

Kwa upande wa wawakilishi wa wafanyabiashara watakaoingia kwenye Tume hiyo ni Mwenyekiti wa Taifa wa Wafanyabiashara, Livembe na Mwenyekiti wa Soko Kariakoo, Martin Mbwana .

Wengine waliopendekezwa na wafanyabiashara ni Issa Msoud, Vunja Bei, Mpandila, Salome Maarufu kama Mama Bonge na wa mwisho ni Omary Hussen kutoka Ugunja.

Kwa mujibu wa Majaliwa Tume hiyo itakuwa na uwezo wa kuhoji mtu yeyote, wafanyabiashara na itafanyakazi kwenye masoko na kwenye majiji makubwa.

Alisema dhamira ya Serikali ni kuona wanafanya walilojipangia na Serikali imesikia kilio chao, hivyo waelewe nia ya dhati ya Serikali yao na inawapenda mno.

“Tunajua nyie mna mikopo na wengine wana mikopo umihiza na mnahitaji kupanua biashara, tukipunguza siku moja mnapunguza mitaji ya kufanya biashara,” alisema na kusisitiza.

“Soko ili ni soko la kimataifa, wale walioondoka na kwenda kufanya biashara nje tuwarudishe, haipendeze vitenge vishuke hapa viende Zambia, halafu virudi nyuma nyuma kuuza hapa.”

Alisema njia mliotumia (kugoma) walikuwa wanafikisha ujumbe. “Nawahakikishia kuanzia leo (jana), mkipata matatizo kuanzia njooni. Agizo langu la kuvunja Task Force linabaki pale pale, kodi itakusanywa na maofisa wetu wa TRA ili wakikosea tutawabane kwa maadili yao,” alisema.

Kuhusu Polisi

Majaliwa alisema kazi ya kukagua risti sio ya kwao, labda pale watakapokuwa na dhamana hiyo, watajitambulisha, vinginevyo italeta lawama.

Tozo za Stoo

Kuhusu tozo za Stoo, alisema ipo sheria ya stoo inayotekelezwa na Wizara ya Viwanda na Biashara, kila anayefanya biashara analipa kodi. “Biashara mnazobeba hamrudi nazo nyumbani, kuna sehemu mnaporundika, huyo ndiye anatakiwa atozwe kodi,” alisema.

Alisema Sheria za TRA za kutoza kodi ya maghala zinasimamishwa na zinapitiwa ili kuona kama sheria inamletea hasara mfanyabiashara.

***Mizigo iliyokamatwa

Majaliwa aliagiza mizigo hiyo iachiwe kwa TRA kuangalia namna wanavyoweza kulipa, au iachiwe kabisa

Kauli ya dharau kwa viongozi

Alisema Waziri mwenye dhamana, waziri mkuu, makamu wa Rais, Rais wa Zanzibar na Rais hao wakishasema ni agizo, hawakiwi kuandika barua, wataandika barua ngapi? “TRA isirudie tena kudai barua, hivi wanapozungumza nyie hamkai kwenye televisheni?

Wanapokuwa wanazungumza kaa kwenye televisheni, sikiliza linalokuhusa, nenda kashuhulikie mara moja. Mkisikia mtu anadai barua ya Rais tuletee jina lake tushughulike naye. Mkuu wa nchi anatamka, mnakuwa na mashaka!”

Mfumo wa ukoamboaji makontena yenye mizingo

Kuhusu hilo, Majaliwa aliagiza upitiwe upya na alitaka TRA ikachambue hilo ili kujua limekaaje.

Rushwa

Kwa upande wa rushwa, alisema bado inaleta athari kwa maendeleo yetu. “Rushwa inafanya watu watabiri mfumo wa maisha yao kila siku. Mapambano ya rushwa ni mapana mno na lazima tupambane nalo sote.

Ili lazima lisimamiwe, kwani imeonekana ipo mifumo kwenye sheria zetu zimetengeneza mianya ya kujadili, tuambieni ili turekebishe ili tuweze kubana mianya hiyo kuanzia hapa hadi bandarini,”alisema Majaliwa.

TRA

Aliitaka TRA na Polisi kukaa na kujitafakari kwa kulaumiwa kuhusu rushwa.

Sheria

Majaliwa alitaka Wizara ifanya mapitio ya sheria na kanuni zinazoumiza wafanyabiashara. “Haiwezekani umma wote ulalamikie Sheria iliyotengeneza kanuni hizo,”alisema Majaliwa.

Awali kabla ya Majaliwa wafanyabiashara walipata fursa ya kuelea dukuduku lao, huku wakitoa mifano mbalimbali jinsi wasivyoridhishwa na utendaji wa TRA .

……………………….