January 15, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Samatta awaomba mashabiki kuwa na subira

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online

NAHODHA wa kikosi cha timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ Mbwana Samatta anayeitumikia klabu ya Fenerbahce ya nchini Uturuki amewaomba mashabiki wa soka hapa nchini kuwa na subira na kuacha kutoa kauli zisizofaa katika kurasa za mitandao za klabu yake mpya pamoja na ile ya Aston Villa.

Samatta ametoa kauli hiyo mara baada ya kutua katika uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere kujiunga na wenzake katika maandalizi ya mchezo wa kimataifa wa kirafiki dhidi ya Burundi utakaochezwa Oktoba 11 katika uwanja wa Mkapa.

Toka anatua katika klabu ya Aston Villa, mashabiki walikuwa wakiandika mambo mengi yaliyoonesha kuwakera viongozi wa klabu hiyo pamoja na mashabiki jambo ambalo pia lilifanya mashabiki wa timu hiyo kumtolea Samatta maneno ya kukera.

Wakati Samatta anakwenda Fenerbahce, mashabiki kutoka hapa nchini bado waliendelea kutoa maneno makali katika ukurasa wa Villa lakini pia wakihamasishana kujiondoa ‘Unfollow’ katika ukurasa huo.

Kutokana na kitendo hicho Samatta amesema kuwa, kinachofanywa na mashabiki hao kinaweza kuwa jambo baya baadaye kwani huneda kikaleta ugumu kwa watanzania wengine kusajiliwa ndani ya klabu hiyo.

Amesema, bado kuna vijana wengi hapa nchini wanaocheza soka na hatuwezi kujua siku moja wanaweza kuonywa Aston Villa lakini wakijua kuwa ni Mtanzania na kukumbuka mambo ambayo yametokea wanaweza kuwaacha.

“Nawaomba sana mashabiki kuwa na subira na kuacha kutoa kauli zisizofaa kwani kunaweza kuwakosesha watu bahati, wengi hawajua lakini mpira una mambo mengi na kitu pekee kinachotakiwa ni subira, ” amesema Samatta.