December 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mfanyabiashara na mwanasiasa mkongwe Zanzibar Salim Turky (kushoto) enzi za uhai wake. Kulia ni mgombea urais wa CHADEMA, Tundu Lissu ambaye ameelezea kwa jinsi alivyokuwa sehemu ya waliotenda miujiza ya kuokoa maisha yake.

Salim Turky afariki, Lissu, wananchi kila kona wamlilia

Na Mwandishi Wetu, timesmajira, online

MFANYABIASHARA maarufu Zanzibar na Mbunge wa Jimbo la Mpendae tangu 2010, Salim Hassan Abdullah Turky, afariki dunia usiku wa kuamkia jana akiwa hospitali ya Tasakhta.

Chanzo cha kifo chake kinadaiwa ni kuugua ghafla. Mwili wake ulifanyiwa Swala ya maiti jana Alasiri katika msikiti wa Othman Maalim na baada ya hapo kuzikwa Fumba, Zanzibar.

Salim Turky ambaye pia alikuwa mgombea ubunge katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu, alizaliwa February 11, 1963 na hadi anafariki alikuwa mwenyekiti wa makampuni ya Turky ambapo chini yake kuna makampuni 12 yanayoendesha biashara zake Tanzania Bara, Zanzibar na visiwa vya Comoro.

Baadhi ya makampuni hayo yanajumuisha hoteli ya Golden Tulip, hospitali kubwa ya Tasakhtaa Zanzibar, pia ilijihusisha na biashara ya cement, Nitak communications, vyakula na mafuta.

Turks Group iliazishwa mwaka 1978 kama duka la nguo na ndugu wa familia moja ambao ni Salim, Murtadha na marehemu Yunus pamoja na baba yao, Hassan Turky na miaka 40 baadaye walibadilisha kuwa moja ya makampuni yanayoongoza Tanzania.

Akizungumzia kifo chake, mgombea urais wa CHADEMA, Tundu Lissu, amesema; “Usiku wa leo (jana) nimepokea taarifa za msiba wa aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Mpendae Ndugu Salim Turky.

“Ile Ndege Iliyonipeleka Nairobi – Kenya Ilidhaminiwa na Salim Turky. Alikuwa mtu mwema, alikuwa mtu safi. Wengi wanasema kuwa kupona kwangu ilikuwa ni miujiza ya Mungu, wanasema kwa usahihi kabisa.

Mwenyezi Mungu huwatumia watu kama Salim Turky kutimiza miujiza yake. Salim Turky alichangia muujiza huo, leo (jana) napenda kutoa salaam za pole kwa ndugu jamaa na familia yake. Mwenyezi Mungu awatie faraja na nguvu kwa msiba huu,” alisema Lissu wakati akihutubia mkutano wa kampeni Njombe