Judith Ferdinand
Sehemu ya kwanza ya makala hii tuliishia Magdalena Sakaya ambaye ni Naibu Katibu Mkuu wa CUF,akieleza mafanikio na alama alizoacha jimboni Kaliua katika kipindi cha miaka mitano ya Ubunge wa Jimbo, na leo tunaendelea kwa kuelekea namna alivyoweza kubadili mitazamo hasi kwa jamii juu ya wanawake.

Kubadili mitazamo hasi ya jamii
Sakaya anasema kabla ya kuwa Mbunge,alikuwa anafanya mikutano ya hamasa kuelimisha jamii kuhusu mazingira au ulinzi wa wanyamapori, asilimia 98 ya wanaohudhuria mkutano huo ni wanaume huku wanawake asilimia 2, na kijiji alipokuwepo kulikuwa na Wamasaia ambao hao ndio walikuwa wanawatenga zaidi wanawake katika mikutano kwa kuwataka wakae umbali wa mita 15.
“Nikawa nawambia wanaoenda kuokota kuni ni wanawake,elimu hii wataipataje kwani wanaume hawaendi kuwaambia,kwamba kuna mkutano wake,nikawa nasema jamani huu ni uonevu,kama wananchi wanatakiwa kushiriki kwanini wanawake wanatengwa.Sasa hivi wanashirikishwa kwenye mikutano,semina mbalimbali na wanasema wanawake wanaweza.Pale ambapo wanawake wamewekwa wengi wao wanafanya vizuri na kutoa picha kwa jamii kumbe hawa wanaweza ,tuwape nafasi,”anasema Sakaya.
Wanawake aliowasaidia
Anasema,kupitia yeye wanawake wengi walihamasika kuingia kwenye nafasi za kisiasa huku wengine akiwasaidia moja kwa moja,ikiwemo wanachama wa CUF.
“Ester Bulaya aliniambia,Madam Sakaya nimeingia Bungeni kutokana na kuvutiwa na wewe, wengine ni Zainabu Kachimba,walisema yani wewe unavyosimama, unajenga hoja, unaitetea.Wengine wameingia katika Udiwani maeneo mbalimbali kwa sababu nimewajenga,nimewapa moyo,kuwasaidia na kuwaelekeza kuwa pita hapa,nawambia wanawake tunaweza ombeni hizo nafasi, fursa ni nyingi kwenye uenyekiti wa mtaa, kijiji,vitingoji na mwisho wa siku anafanikiwa,”.
Pia anasema,kuna wengine walikuwa wanatamani kugombea lakini hana uwezo,hivyo alikuwa anawaambia wakagombee na yeye anawasaidia kuweka mawakala,muziki wakati wa kampeni kupitia fedha aliyokuwa nayo anaigawanya kidogo kidogo, wapo ambao wamefanikiwa kupata udiwani, uenyekiti wa kitongoji ingawa wanaume wengi hawataki wake zao wawe katika nafasi za uongozi na ameona matunda.
Mmoja wa wananchi wa Kijiji cha Ushokora wilayani Kaliua mkoani Tabora Halima Mashaushi,anasema alihamasika na kauli za Magdalena Sakaya,alizokuwa anatoa kwa wanawake kuwa wajitokeze kugombea nafasi mbalimbali kwani wanaweza.
“Mwaka 2014, niligombea katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa,nikashinda nafasi ya Mwenyekiti wa Kitongoji cha Barabara ya Urambo kwa tiketi ya CUF,baada ya kuvutiwa na namna Sakaya alivyokuwa anapambana na kuhamasisha wanawake kugombea nafasi mbalimbali,mwaka 2019 katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa,niligombea tena ila uchaguzi ulikuwa na sintofahamu na hatukuweza kuchaguliwa vyama vingine vya siasa nchi nzima isipokuwa wa CCM,”anasema Mashaushi na kuongeza:
“Mwaka 2020 nikagombea nafasi ya Udiwani Kata ya Ushokora, kwani wanawake uwezo tunao wa kusaidia nchi,Mkoa na Wilaya,lakini napo jina langu na wengine yalikatwa,sikukataa taama,2024 katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa,niligombea uenyekiti wa kijiji,hatukutendewa haki katika demokrasia ambapo tulienguliwa majina yetu licha ya kuwa nchi ni yetu sote,”.

Kwa mujibu wa ripoti ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka 2019,inaonesha kuwa kati ya nafasi 11,915 za wenyeviti wa vijiji,wanawake walishinda nafasi 246 sawa na asilimia 2.1, wanaume wakishika asilimia 97.9 ya nafasi hizo huku nafasi 4,171 za wenyeviti wa mitaa wanawake walishinda nafasi 528 sawa na asilimia 12.6.
Huku ripoti ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya mwaka 2020,inaonesha wanawake waliochaguliwa kwa nafasi za Udiwani ni asilimia 6.58,sawa na Madiwani 260 kati ya 3,953,huku viti maalum walikuwa 1,374 katika halmshauri 184 sawa na asilimia 24.59,hivyo jumla ya madiwani nchi nzima walikua asilimia 29.24.
Mwenyekiti wa CUF Wilaya ya Kaliua mkoani Tabora,Lubaga Katwiga, anasema,chama hicho kinawapa nafasi wanawake za kugombea nafasi mbalimbali, ambapo katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa mwaka 2024 kwa upande wa Kaliua wanawake 10 waligombea nafasi za uenyekiti wa mtaa,saba wa kitongoji na ujumbe walikuwa wanawake.
Pia chama hicho kimejipanga kuwapa kipaumbele na kuwahamasisha wanawake kugombea nafasi mbalimbali kati Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.
Wanawake katika kukuza demokrasia
Sakaya anasema wanawake wanamchango wa kukuza demokrasia nchini,kwani wakipewa nafasi wanaitendea haki,huku akitolea mfano Mkoa wa Manyara yupo Queen Sendiga, hali hiyo inatoa picha kwamba maeneo yote ambayo wanawake wameshika nafasi za uongozi wanafanya vizuri na wanaweza bila kubebwa mgongoni.
“Wanawake wanafanya mengi mfano Profesa Anna Tibaijuka, amekuwa Waziri wa awamu tatu,alionesha uwezo wake na kazi zake zinaonekana mpaka leo,amekua kiongozi wa Umoja wa Mataifa(UN),kwa muda mrefu na leo jina lake linaandikwa,”.
Bituro Kaizeri kutoka taasisi ya Socialogy Tanzania,anasema,wanawake wanamchango katika kukuza demokrasia nchini,akiwemo Sakaya,ambaye amefanya vitu vingi ikiwemo kuhamasisha wanawake kuingia katika siasa,ambaye kwa sasa ameingia kwenye orodha ya wanawake wenye mchango nchini hapa akiwemo Bibi Titi,Getruda Mongela,Dkt.Asha Rose Mingiro.
“Dunia imetoa nafasi za upendeleo kwa wanawake ndio msingi wa sisi kuwa na viti maalum,lakini mkakati sahihi wanawake wasitake kubebwa, wapambane wanaweza kwa sababu talanta ya uongozi anayetoa ni Mungu haijalishi huyu ni mwanamke au mwanaume,wasiogope vikwazo,”anasema Bituro.
Hata hivyo Sakaya,anasema,hali ya demokrasia nchini ,haipo vizuri ingawa inaonekana kwenye chaguzi kwa baadhi ya vyama vya siasa, akitoa mfano katika uchaguzi wa CHADEMA ulifanyika mwaka huu,kimeonesha demokrasia kwa kumtoa kiongozi mkongwe kwenye nafasi ya Uenyekiti na kumuweka mtu mwingine.
“Ndani ya chama chetu ipo demokrasia ya kweli,na mwanamke unapata nafasi kwa uwezo wake,kujiamini,elimu,CUF hakuna kubebana ,na kila mtu ana haki ya kugombea nafasi yoyote lakini asivunje sheria.mwaka 2014 CUF tuliweka historia ya kuwa chama cha kwanza kuwa na Naibu Katibu Mkuu mwanamke,mwaka 2024 pia tumeweka historia ya kuwa na Katibu Mkuu mwanamke haijawai kutokea kwa vyama vyote vya siasa nchini,”anasema Sakaya..
Kitu kipi kinampa huzuni na furaha
Sakaya anasema,kitu kinachomfurahisha ni utumishi wake kwa jamii na alama alizoziacha pamoja na kusaidia wanawake kutoka gerezani na kuwa huru, baada ya kukaa huko kwa ajili ya uonevu na kesi zao kutoeleweka.
Anasimulia kuwa,wakati amepelekwa rumande kwenye kituo cha polisi huko Kaliua,ambako alikaa kwa siku tatu,alimkuta binti amekaa na mtoto mdogo wa miezi saba “lock up,” kwa muda wa siku nne,hivyo alifanya jitihada za kumtoa na kufanikiwa.
Anasimulia kuwa,hata alivyopelekwa mahabusu gerezani ambako alikaa kwa siku 18,aliwakuta wanawake wengi kati yao saba huku mmoja akiwa na binti yake,ambao wamekaa gerezani miaka 7 na hawakuwai kusimama mahakamani hata mara moja ,kwa kesi ya kusingiziwa kuiba godoro la inchi tatu na jirani yao ambaye aliwachukia na mwengine alikuwa na kesi ya wizi wa shilingi 10,000.
Hata hivyo anasema,wakati akiwa kizuizini hakutaka kupewa nafasi ya upendeleo kama Mbunge ya kumtofautisha na wanawake wengine aliowakuta gerezani na badala yake alikula chakula na kushiriki shughuli zote ndani ya gereza kama wengine.
Ambapo kupitia njia mbalimbali aliweza kuhakikisha amepata namba na majina ya kesi za wale wanawake saba.
“Sitasahau siku niliotoka gerezani, wamama walilia sana,nikawaambia tukibaki wote humu hatutapata ukombozi,nikafanye kazi nikiwa nje ya gereza ili na nyie muweze kutoka.Baada ya kutoka gerezani nilianza na kesi hizo kwa kumueleza Waziri husika ni kimwambia kuna kesi fulani,namba fulani ya mwaka fulani ipo gereza fulani,ndani ya miezi mitatu mpaka sita wale watu walitoka gerezani,kila mmoja kwa nafasi yake alinutafuta ananiambia mimi ni fulani nimetoka,”.
“Mpaka leo kinanipa faraja ni wale watu walivyotoka gerezani,nikasema Mungu alinipeleka pale kwa kusudi maalumu,sikwenda kama mfungwa bali mkombozi kwa wengine ,kitu kingine kinachonipa furaha ni kufanikisha sheria mbalimbali ikiwemo ya watu wenye ulemavu,mazingia,”.
‘Wakati nakuwa Mbunge Kaliua ilikuwa na vituo viwili vya afya, lakini leo inavyo zaidi ya sita,hospitali ya Wilaya ambayo awali haikuwepo,zahanati nyingi.Najivunia kuwa huduma za afya zimeboreshwa,shule zimejengwa, ninafurahi kutokana kupiga kelele bungeni haya yamefanyika kwani awali kulikuwa hakuna shule, watoto walikuwa wanakaa chini,”.
Hata hivyo anasema,suala la kupatika kwa katiba mpya ndio linalomuumiza kwani na yeye ni miongoni mwa watu waliolipigia kelele jambo hilo wakati Rais Jakaya Kikwete akiwa madarakani lakini mpaka sasa halijafanyiwa kazi.
Kilichosababisha aende gerezani
‘‘Mwaka 2013,nikiwa Mbunge wa Viti maalumu Mkoa wa Tabora,nilipigiwa simu na wananchi wa Kaliua,wakiniambia njoo utusaidie,mifugo yetu imekamatwa kwa agizo la Mkuu wa Wilaya wa kipindi hicho ambaye kwa sasa ni marehemu, kuwa ina siku sita,imefungiwa,inakufa kwa njaa,tumejaribu kupambana hatuna msaada.Kwa ujasiri nilisafiri usiku kucha kutoka Dodoma mpaka eneo la tukio.Nikaiona mifugo,nikawambia wananchi,hatutaenda kwa shari,tutaenda kwa utaratibu ili tupate majibu kutoka kwa Serikali,”.
Katika harakati za kuwatetea wanachi takribani 1,000,ambao mifugo yao ili kamatwa, kwa sababu walitakiwa kuhama katika eneo ambalo wameishi kwa miaka 30 jambo ambalo hakukubaliana nalo,kwani alitaka wahamishwe kwa utaratibu na wajue wapi wanapelekwa.
Anasimulia kuwa,wakati akimtafuta Mtendaji wa Kata ili haweze kumpatia maelezo ya kwanini wameifungia mifugo hiyo,alizuiliwa na polisi waliokuwa wanalinda eneo hilo wakidai ameenda kuopoa mifugo hiyo.
”Nikawaambia hapana,siwezi kutoa mifugo mimi Sakaya mmoja ambaye sina silaha wakati kuna walinzi,natamani nipate uongozi ambao utaniambia kwanini wameifungia na nini hatima wakati wanakufa mmoja baada ya mwingine,mnawatesa,kama mmewafungia mkawachunge na muwalishe,ikatokea sintofahamu wananchi wakaanza kurusha mawe,katika vurugu hizo zilisababisha vifo vya watu wawili na mimi kupelekwa polisi,ambapo nilifunguliwa kesi ya kuingilia majukumu ya Polisi ,nilikaa polisi kwa siku tatu ya nne nikapelekwa mahakamani kisha gerezani,chama kiliniletea Wakili baada ya siku 18 nikatoka,”.
Wanavyomzungumzia
“Niliosoma nao shule ya msingi,sekondari na vyuoni,wanasema Magdalena Sakaya,alikuwa mpole,amejifunzia wapi ukali,ingawa wananipongeza wakisema umetuheshimisha na umesimama, unajenga hoja,unatetea haki za watu,huna uwoga,una ujasiri na wananitia moyo,”.
Sakaya anasema,watu wake wa karibu na familia yake hasa wazazi wake wakati mwingine wanakuwa na hofu na wanamwambia kuwa wanaogopa na kuhofia usalama wake kwani wanaona watu wanaoongea sana,wanapotea katika mazingira yasioeleweka.
“Mimi nawatia moyo,nawaambia Mungu hawezi kuruhusu mabaya yatokee kwa mtu ambaye anatete haki za wengine ambao wanahitaji kutetewa.Watu wananitia majina mengi mara simba jike,kutokana na ninavyojiamini,ninavyopambana na misimamo yangu,”.
Pia anasema,anajivunia kusemwa kwa mazuri na baadhi ya watu kila anapopita,anapongezwa na kupata maoni chanya,huyu ni Mbunge mstaafu alipambana kutetea Watanzania,huyu amekaa ‘lock up’ kwa ajili yetu,amewatetea wanawake na kupigania huduma mbalimbali.
“Watu wananiambia kwa nini ugombei Urais kwani unaweza,hoja zako ‘tunazimiss’,rudi bungeni utafikiri najiweka na kujiondoa mwenyewe kumbe ni mfumo,ninachojivunia kazi zangu zimepata kibali,”.
Hata hivyo katika suala la kugombea kama wananchi wakaliua wanavyomuomba, bado hajalitolea maamuzi kama familia na chama bado wanajadiliana,na kwa sasa wanajipanga kwa ajili ya uchaguzi mkuu,kwa kukipanga chama kwenye ngazi za matawi,Kata Kanda za Wilaya.
Mwenyekiti wa CUF Wilaya ya Kaliua mkoani Tabora,Lubaga Katwiga, anasema,uonevu uliokuwepo Kaliua uliisha, kutokana na jitihada za Sakaya,ndio maana mpaka leo wananchi wa Kaliua wanamuhitaji aje kugombea tena nafasi ya Ubunge kwani kila mmoja anatambua mchango wake.
Hata hivyo anasema,kupitia Sakaya amejifunza mwanamke akipewa jambo analisimamia na wanatetea na kuikuza demokrasia,hivyo vyama vya siasa viwape kipaumbele wanawake,ili kuleta usawa na demokrasia ya kweli.

Nini kifanyike kuhamasisha wanawake kugombea
Mjumbe Kamati Tendaji CUF Wilaya ya Nyamagana mkoani Mwanza,Martha Haule,anasema,ili wanawake waweze kushiriki kikamilifu katika siasa na kukuza demokrasia,vikwazo vya kijamii vishughulikiwe kama vile mitazamo potofu kuhusu majukumu ya wanawake katika jamii na familia.
“Wanawake wanapaswa kuacha uoga na kujitokeza kuwania nafasi mbalimbali ikiwemo Ubunge wa majibo na kuacha kuamini kuwa nafasi hizo wanastahili wanaume tu,kwani hata vyama vya siasa kwa sasa vinatoa fursa kwao,tulionao kwa sasa ni wale walioingia kwenye siasa muda mrefu na wakapata ukomavu,”anasema Mwenyekiti wa chama cha ADC Taifa,Shabani Itutu.
Hata hivyo kukuza ushiriki wa wanawake katika vyombo vya habari kwa kuwapa wanawake nafasi za kuzungumza masula mbalimbali ikiwemo ya kisiasa inaweza kusaidia kubadili mitazamo ya jamii kuhusu uwezo wa wanawake katika uongozi wa kisiasa na kuvunja mifumo ya kijinsia na kuongeza ushiriki wa wanawake.
Ambapo jambo hilo limeanza kufanyiwa kazi na Women Writers Forum Tanzania(WriFOM), kwa kuwezesha waandishi wa habari wanawake takribani 15, nchini kuandika makala za wanawake waliofanya mambo mbalimbali katika siasa na kuwa na mchango wa kukuza demokrasia nchini ili kuhamasisha wengine na kuonesha mambo ambayo yamefanywa na wanawake hao,kupitia mradi wa wanawake na demokrasia (Women in Democracy).
More Stories
Sakaya:Mungu,ujasiri na kujiamini ndio siri ya mafanikio safari ya siasa/ kutetea wananchi-sehemu ya kwanza
Wakazi mabogini waomba mabadiliko ya Sheria kurahisisha upatikanaji haki kwa waathirika wa ukatili
Changamoto za mabadiliko ya tabianchi zinavyoweza kuathiri ustawi wa familia,watoto