March 20, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Sakaya:Mungu,ujasiri na kujiamini ndio siri ya mafanikio safari ya siasa/ kutetea wananchi-sehemu ya kwanza

Judith Ferdinand

UNAPOTAJA jina Magdalena Sakaya picha inayokuja kwa haraka ni mwanamke jasiri, mwenye msimamo na asiyeyumbishwa katika kutetea jambo analoamini lina maslahi mapana kwa taifa lake.

Kutokana na sifa hizo aliingia katika historia ya kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha wananchi CUF,ikiwa ni mara ya kwanza kwa nafasi ya juu ndani ya chama cha siasa kukaliwa na mwanamke, huku akisota rumande kwa siku 21 kwa ajili ya kuwapambania wananchi wa Jimbo la Kaliua.

Sakaya anasema aliingia kwenye siasa baada ya kuona chanagmoto za wananchi kwenye maeneo anayofanyia kazi hazitatuliwi huku kiu yake ikiwa ni kuona haki inatendeka kwa kila mtu.

“Kutetea haki za wananchi,kunahitaji kumtegemea Mungu,ujasiri na kujiamini ili kuweza kuacha alama na kukumbukwa na watu kulkiniweka kizuizini kwa siku 21 kizuizini kwa,”amesema.

Naibu Katibu Mkuu wa CUF Magdalena Sakaya picha kwa msaada wa mtandao

Ni Januari 28,2025, napiga simu inapokelewa na Magdalena Sakaya, najitambulisha na kumueleza nia yngu,anakubali bila kinyongo na tunaanza mahojiano maalumu yaliochukua dakika 78.

Mazungumzo yetu yanaanza kwa kunielezea safari yake ya kielimu na siasa ambayo ni yenye milima,mabonde,misukosuko na mafanikio lukuki yalioweka historia ya kukumbukwa nchini hapa.

“Nimezaliwa Mkoa wa Kilimanjaro,Wilaya ya Moshi Vijijini ,Novemba 21,1970,ni mtoto wa kwanza katika familia ya watoto watano ya Constantine Sakaya mke wake.Wakike tupo wa tatu na wakiume wawili,pia ni mama wa mtoto mmoja na Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi CUF,”anasema Sakaya.

Sakaya anasema baba yake ni mtu muhimu katika maisha yake,na anaendelea kumshukuru Mungu kwa kumlea kwa upendo na kumsaidia kuwa na mafanikio.Ktika shukrani zake Sakaya anasema”Namshukuru Mungu ,nimelelewa vizuri na amenipa neema mpaka sasa wazazi wangu wapo hai,”.

Kutoka Kibosho hadi chuo kikuu

Elimu yake ilianza shule ya msingi Kombo iliopo Kibosho wilayani Moshi Vijijini na kuhitimu mwaka 1985.Mwaka 1986,alijiunga na shule ya sekondari ya wasichana Kibosho(Kibosho Girls),akahitimu mwaka 1989.

Hakuishia hapo,alijiunga na shule maalum ya wasichana ya Msalato(Msalato Girls) kwa elimu ya kidato cha tano na sita,na kuhitimu mwaka 1992.

Mwaka 1993,aliingia Jeshini Oljoro na kisha kuendelea na masomo ya elimu ya juu mwaka 1995 ambapo alijiunga na chuo cha Mifugo Tengeru kwa ngazi ya Stashahada ya Uzalishaji Wanyama(Diploma inAnimal Productio) hadi nwaka 1997.

Mwaka 1998,alijiunga na Chuo Kikuu cha Sokoine na kumalizaShahada ya Usimamizi wa Maisha ya Wanyama (Degree in Animals Life Management) mwaka 2001.

“Baada ya kumaliza masomo nilipata kibali cha kupata ajira mapema kutoka mashirika ya nje ya nchi,ambayo yanajishughulisha na usimamizi na masuala ya wanyamapori nchini Tanzania kutoka chini Denmark.Nilifanya kazi maeneo ya Pwani na kisha mkoani Tabora,”anasema Sakaya.

Harakati za kisiasa, demokrasia

Sakaya anasema alianza harakati za kupigania demokrasia akiwa hana kadi ya chama chochote cha kisiasa,kwa sababu hakuwa na nia ya kujihusisha na siasa zaidi ya kufanya jitihada katika masuala ya taaluma yake.Hata hivyo anasimulia kuwa alijikuta anaingia katika siasa baada ya kufanya kazi na wanasiasa katika miradi ya mazingira na wanyamapori.

Anasimulia kuwa,mwaka 2000,alianza harakati za kupigania demokrasia chini chini kwa sababu kipindi hicho hakuwa kwenye nafasi ya uongozi,hivyo akisikia mtu amedhulumiwa haki au mtoto kanyanyasika anaenda kufuatilia,ili kufahamu hatua gani zimechukuliwa.

Pia akisikia mtu kaonewa anakwenda moja kwa moja kwa viongozi nawaambia wamekaa tu ofisini lakini kuna shida moja,mbili,tatu,anaenda kuwaonesha,ambapo anasema kuwa aliwai kwenda Tume za Haki za Binadamu, kufuatilia haki za watu.

Kilichomvutia

“Niliona changamoto zinazowakabili wananchi zinakosa ufumbuzi wa haraka,hivyo nikajikuta nahitaji kupata jukwaa la kisiasa au na uwanda mpana wa kuzipatia suluhiso la haraka kwa njia sahihi ,siyo kwa mtindo wa kisiasa bali kwa njia ya kisayansi na kitaalamu,”anasema Sakaya.

Anasema,kutokana na kazi aliyokuwa anafanya alijikuta anakuwa na ushawishi na wananchi walimpenda,hivyo walimuhimiza kuingia kwenye siasa ili aweze kuwasaidia zaidi.Na kabla ya kuingia kwenye siasa,alijitahidi kujifunza na kusoma katiba ya vyama mbalimbali vya siasa.

“Nilivutiwa na Katiba ya CUF,na sijawahi kuwa na kadi ya chama kingine.Mimi ni mtu ninayependa sana haki,si haki yangu pekee,bali haki za kila mtu.Napenda kila mmoja atendewe haki. Kitu kinachoniumiza sana ni kuona haki ya mtu ikipotea hivi hivi, au mtu anaponyang’anywa haki yake isivyo halali,”anasema Sakaya na kuongeza:

“Hilo linaniuma sana,hata kama ni jambo dogo nalia ikiwa najua ni haki yangu imeporwa kinyume cha sheria, na anayenipora hana haki ya kufanya hivyo, hata nikiwa kwenye basi,nione mtoto analia mfululizo lazima nimuulize mzazi au mtu aliyenaye ili kujua shida ni nini au mtoto kaibiwa,”.

“Hali hiyo ya kutaka kusaidia ipo ndani yangu,ni kitu nimezaliwa nacho,na ninajikuta nimeingia kwenye kesi ambazo siyo zangu kutokana na kuguswa na matatizo ya watu,roho ina niingia kwa ajili ya kutetea haki ya mtu ambayo imeporwa au inanyang’anywa bila sababu,”.

Naibu Katibu Mkuu wa CUF Magdalena Sakaya picha kwa msaada wa mtandao

Anasema baada ya kusoma katiba ya vyama mbalimbali vya siasa,aliona chama kilichokuwa kinajishughulisha na masuala ya haki za watu ni CUF,kilieleza wazi kuwa haki ni haki ya kila mtu,haki za afya,haki za huduma,haki za uzazi,haki ya lishe bora n.k.

“Hii ndio ilinivutia na kunihamasisha kwani ndicho chama nilichokuwa nakihitaji kutokana na sare z ake ya kutetea haki za watu.Hii ndio sababu niliweza kuwa mtu wa kupambana kwa hali yoyote,na wakati mwingine kujikuta katika mazingira ya kukaa mahabusu au ‘lock-up’,kwa sababu ya kutetea haki za watu,”anasema Sakaya.

Safari ya Ubunge, uongozi

Sakaya anasema alichaguliwa kuwa Mbunge wa Viti maalum Mkoa wa Tabora kwa awamu mbili mfululizo yanii mwaka 2005-2010 na mwaka 2010-2015.Mwaka 2015,alijitosa kugombea Ubunge wa Jimbo la Kaliua akichuana na aliyekuwa Mbunge wa Jimbo hilo na Waziri wa zamani wa Elimu,Sayansi na Teknolojia Profesa Juma Kapuya mpaka mwaka 2020.

Akiwa na nia ya kuendelea kutetea haki za wananchi aligombea tena Ubunge wa Jimbo la Kaliua mwaka 2020,lakini kutokana na sintofahamu katika uchaguzi wa mwaka huo kwa nchi nzima vyama vya upinzani havikufanikiwa kupata nafasi za Ubunge.

Hata hivyo, kwa mujibu wa Taasisi ya Kitaifa ya Kidemokrasia (NDI), inasema katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020,wanawake waliochaguliwa kwa nafasi za Ubunge ni asilimia 9.5,huku wabunge wa Viti maalum ni asilimia 29,hivyo kufanya jumla ya Wabunge wanawake kuwa 142 kati ya 393.

Pia ndani ya chama cha CUF ameshika nafasi ya Naibu Katibu Mkuu kwa awamu tatu mfululizo akiwa mwanamke wa kwanza kushika nyadhifa hiyo ya juu ndani ya vyama vya siasa nchini hapa,ambapo mara ya kwanza alichaguliwa kutumikia nafasi hiyo 2014-2019, awamu ya pili 2019-2024 na awamu ya tatu 2024-2029.

Siri ya kushinda mfumo dume

Sakaya anasema,mfumo dume upo ila,Imani yake kwa Mungu, kujiamini na ujasiri aliozaliwa nao na kutoogopa ndio siri ya kupambana na mfumo huo,Mwaka 2015 wakati anaanza harakati za kugombea Jimbo la Kaliua,watu walimwambia anaenda kupambana na mtu ambaye hatomuweza kwani ana mzidi kielimu na kifedha,amekuwa Profesa na Waziri.

“Sifa zote alikuwa nazo,nikijilinganisha naye mimi najiona mdogo nilisema haijalishi,wananchi hawahitaji degree,hawahitaji kuona kwamba wewe ni mkubwa kiasi gani,wanahitaji huduma. Kwa kuwa najua kuna mahali hawajatendewa vizuri,nikasema sera zangu watazielewa vizuri na mwisho wote watanichagua kwani ni ulinzi wa Mungu,hawezi kuruhusu kitu kibaya kinitoke kwa sababu anapenda suala la kutetea haki za watu wengine,” anasema Sakaya na kuongeza:

“Hata hivyo mpinzani wangu mkuu alikuwa anatoa vitisho,matusi,kejeli lakini kwasababu Wananchi wa Kaliua walikuwa wanataka mtu mmoja atakayetetea maslahi yao bila kuwabeza,nilisema sitarudi nyuma,”.

“Namshukuru Mungu niliweza kushindana na Profesa Juma Kapuya nikamshinda,ingawa jamii yaatu wa Kaliua wengi ni Wasukuma,Wanyamwezi na Waha,ambao kuwapa heshima wanawake kwao ni hapana,mimi walinipa heshima na mpaka sasa,wananipigia simu wananiambia mama njoo,’tumekumiss’,kutokana na kazi nilizofanya bila kubagua,”.

Mafanikio aliyapata

Sakaya anasema,akitazama nyuma na sasa anaona amefanikiwa kwa kiasi kikubwa,kwani yale mambo aliyokuwa anayatamani kabla na baada ya kuwa mwanasiasa pamoja na nafasi ya Ubunge kwa kipindi cha miaka 15,yamefanyiwa kazi ingawa yapo ambayo hayajafanyiwa kazi.

Huku miongoni mwa mambo aliokuwa anatamani ni wanawake kupata fursa sawa kama wanaume ikiwemo elimu,uongozi mbalimbali ikiwemo wa kisiasa kwani historia ya Tanzania,wanawake wengi waliachwa nyuma,kielimu huku akitolea mfano halisi kijijini wakati akisoma shule ya msingi Kombo,darasa lao lilikuwa na wasichana 16 kati yao waliondelea na sekondari ni wawili huku waliobaki wakiishia kuolewa na kupata wajukuu ambao maisha yao siyo mazuri.

“Kijiji kizima tuliondelezwa ni mimi na rafiki yangu Monica ambaye kwa sasa ni mwalimu,shule yetu kwa kipindi hicho haikutoa hata mtoto mmoja aliyefaulu.Ilikuwa bahati tulipelekwa shule ya binafsi kwani baba wa rafiki yangu alikuwa tajiri kijijini kwetu,na baba yangu allikuwa tajiri kwenye kilimo,alipenda nisome,na elimu ilikuwa kama almasi kwake,alichekwa sana kwamba anaenda kusomesha mke wa watu,atabeba mimba,”anasema Sakaya.

Anasisitiza kuwa alitamani wanawake wengi wapate nafasi za uongozi na kuonesha kuwa wanaweza wakipewa nafasi siyo wakiwezeshwa ikiwemo nafasi za utumishi wa Serikali na siasa,siyo wanaume tu hapana.

“Mambo niliokuwa nayapigania yamefanikiwa mfano leo wanawake wengi wanateuliwa kushika nafasi mbalimbali serikalini ikiwemo za Uwaziri,Naibu Waziri,Wakuu wa Mikoa na Wilaya, Wakurugenzi,eneo la siasa nafasi za juu zilikuwa zinaongozwa na wanaume.Nilipo ingia CUF, nikasema lazima Katiba yetu tuibadilishe na tuweke mfumo wa wanawake kupata nafasi za kuongoza pale juu,mwaka 2014 kilikuwa chama cha kwanza Tanzania nafasi ya Naibu Katibu Mkuu Taifa ikashikwa na mwanamke ambaye ni mimi,baadae ndio vikafuata vyama vingine,”anasema Sakaya.

Pia anasema alipigia kelele suala la matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa kuhakikisha kuna kuwa na majiko sanifu kwa ajili ya kusaidia wanawake,jambo alilolifanya ata kabla hajawa Mbunge.

“Nilikuwa kwenye Kamati ya Maliasili kwa miaka kumi mfululizo,kulikuwa na agenda ya nishati nbadala,nikawa na hoji Bungeni kwanini tusiwe  tunapikia gesi na makaa ya mawe yachakatwe tupate nishati ya kupikia kuliko kuharibu misitu,tumefanikiwa kwa kiasi kikubwa, kwa sababu leo Tanzania agenda ya nishati safi aliyonayo Rais Samia, aikuja hivi hivi,ilianzia huko nyuma niliyapigia kelele, ili wanawake wapate fursa za kushiriki mambo mbalimbali ya kijamii,kiuchumi na siasa,”.

Pia anasema,alitetea watoto wanaofanyiwa ukatili ikiwemo kubakwa na kulawitiwa pamoja na watu wenye ualbino kuuwawa, kwa kupaza sauti Bungeni kwamba kuwe na sheria maalumu kwa ajili ya kesi za namna hiyo ziwe zinachukua muda mfupi,kwani zilikuwa zinapigwa danadana inachukua muda mrefu na kusababisha mtoto kutokusoma mwaka mzima na mauaji mfululizo ya wenye ualbino yakawa yamepungua.

Anasema,gerezani kuna uonevu ambapo wapo watu hawastahili kukaa kule,unakuta mtu ameiba godoro la shilingi 20,000-40,000,amekaa gerezani miaka saba,miaka kumi,kuna mwingine amekaa kule hajui kesi gani imemuweka huko.

“Nilivyotoka gerezani wakati huo Waziri wa Mambo ya Ndani alikuwa Dkt.Emmanuel Nchimbi ambaye sasa hivi ni Katibu Mkuu wa CCM nilisema nitapiga kelele bungeni mpaka mbadilishe sheria za gerezani,wananchi wapewe haki,kesi ndogo ndogo za wizi wa magodoro,ndoo zisiwe kesi za kufungwa badala yake ziwe za kupewa adhabu kama vile kifungo cha nje.Namshukuru Mungu sasa hivi kuna kitu kimefanyika, zile kesi ndogo ndogo watu hawaendi gerezani,wanapewa adabu ikiwemo kifungo cha nje,”.

Aidha, anasema,alipambana ili watu wenye ulemavu wawe na sheria yao maalum,ambayo kwa sasa ipo ili haki ipatikane,kwani kundi hilo linastahili kupata  elimu,huduma kama wengine,ajira, miundombinu rafiki na rahisi kwao.

“Leo unaambiwa wanaojenga hoteli wanalazimika kuweka miundombinu rafiki ya watu wenye ulemavu,hospitali ata shule,kwani imekuwa sheria kwamba kila taasisi au sekta yoyote iweke miundombinu rafiki kwa watu hao.Nilioyapigania kwa muda mrefu na kuonekana hayana maana yameanza kufanyiwa kazi,”.

“Yapo mengi najivunia ambayo nimeyapigia kelele hasa kwenye vyama vya siasa nafasi za juu wanawake waonekane,maana nyuma kitu hicho kulikuwa hakiwezekani,lakini sasa tunamshukuru Mungu angalau tunaonekana kwenye nafasi mbalimbali,mfano Dorothy Temu,kiongozi mkuu wa ACT- Wazalendo,”.

Pia anasema, wamekuwa na Jumuiya za wanawake kwenye vyama vyao vya siasa ikiwemo Juke-CUF,BAWACHA,UWT,ambazo zinatumika kama majukwaa ya wanawake kukaa na kujadili mambo yao ikiwemo ya uchumi,siasa.

Hata hivyo anasema,amefanya kazi Mkoa wa Tabora na amefanikiwa kuacha alama kila alipopita,hat katika miaka yake mitano ya Ubunge jimboni Kaliua,kila Kata kuna  alama.

“Utasikia hospitali hii mama Sakaya alijenga msingi,shule hii alijenga darasa,hapa zahanati alifanya hiki,hakuna sehemu ambayo sijaacha alama,kila nilipo pita na kukanyaga niliweka alama, namshukuru Mungu kwa hilo kwa sababu unaweza kufanya kazi kwa muda mrefu ukasemwa vibaya na kila mtu akawa anasema ahaa! huyu hapana,”.

Naibu Katibu Mkuu wa CUF Magdalena Sakaya picha kwa msaada wa mtandao

Kauli yake inaungwa mkono na Mwenyekiti wa CUF Wilaya ya Kaliua mkoani Tabora,Lubaga Katwiga,anasema Sakaya,amekuwa na mchango na kila mmoja Kaliua anautambua,ikiwemo kutetea wananchi wakaachiwa na Serikali maeneo yao yaliokuwa yanadaiwa kuwa yapo ndani ya hifadhi ambapo mpaka sasa wanaendelea na shughuli zao za kiuchumi,amefanikisha kujengwa shule za msingi.

“Wakati anakuwa Mbunge hali ya Kaliua kimaendeleo ilikuwa chini,ambapo kituo cha afya Kaliua kulikuwa hakuna kitanda ata kimoja,wajawazito walijifungulia chini,ila yeye alifanikisha kuweka vitanda 11.Hospitali ya Wilaya ya Kaliua ilikuwa haina usajili,alipambana ikapata usajili na wananchi wakapata huduma nzuri ikiwemo kufanyiwa upasuaji,alihakikisha hupatikanaji wa maji safi na barabara, pamoja na kuwasaidia baadhi ya vijana wa Kaliua kujiunga na jeshi na sasa wana ajira,”anasema Katwinga.

Itaendelea kesho sehemu ya pili