January 17, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Safu ya ulinzi yaendelea kumpa jeuri Kaze

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online

WAKATI klabu ya Yanga ikiwa imebakiza mechi moja dhidi ya Ihefu kabla ya kumaliza mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu Tanzania Bara (VPL), safu ya ulinzi ya klabu hiyo imeendelea kumpa kiburi kocha mkuu Cedric Kaze pamoja na benchi lake la ufundi.

Licha ya awali kutoonesha kuwa na wasiwasi wowote huku akivijunia safu imara ya ulinzi katika mechi zao zilizopita, mabeki hao sasa wameendelea kudhihirisha ubora wao baada ya kuonesha umahiri wao kwenye kupachika mabao.

Katika mchezo wao uliopita dhidi ya Dodoma Jiji FC, Nahodha wa Yanga Lamine Moro alifungua kitabu cha mabao kwa timu yake dakika ya 25 ukianzishiwa mpira wa adhabu na Deus Kaseke na kuisawazishia timu yake baada ya wapinzani wao kupata goli la dakika ya tatu lililofungwa na Seif Abdallah Karihe akimalizia mpira uliotemwa na kipa Metacha Mnata kufuatia krosi ya Dickson Ambundo.

Goli hilo ni la nne kwa beki huyo ambaye msimu huu ameonesha kiwango bora baada ya kuipa ushindi timu yake katika michezo muhimu dhidi ya Mbeya City na Mtibwa Sugar ambayo yote walipata ushindi wa goli 1-0 huku goli lingine akifunga katika mchezo dhidi ya Mwadui ambao timu hiyo ilipata ushindi mnono wa goli 5-0.

Beki huyo sasa ana magoli ya kufunga sawa na mshambuliaji Michael Sarpong ambaye pia ana goli nne alizofunga katika mechi dhidi ya Tanzania Prisons, Biashara United, Simba pamoja na katika mchezo dhidi ya Ruvu Shooting.

Lakini pia anashikilia rekodi ya kuwa beki pekee mwenye goli nyingi ndani ya Ligi Kuu na sasa amewema wazi kuwa anachokitaka ni kuvunja rekodi yake ya kufunga goli saba aliyoiweka wakati akiitumikia Buildcon FC ya Zambia.

Katika mchezo dhidi ya Dodoma, goli la pili lilifungwa na mshambuliaji mpya Said Ntibazonkiza dakika ya 69 kwa mpira wa faulo uliomshinda kipa Arone Kalambo na kuingia moja kwa moja wavuni.

Lakini dakika ya 75, beki na nahodha msaizidi, Bakari Mwamnyeto aliwainua tena mashabiki wa Yanga baada ya kukwamisha mpira wavuni akimalizia mpira wa adhabu uliopigwa na Ntibanzonkiza.

Ushindi huo umewafanya Yanga kuendelea kujichimbia mizizi kileleni mwa msimamo wa Ligi baada ya kufikisha pointi 40 wakiwa wameshinda mechi 12, sare nne huku ikiwa ni timu pekee katika Ligi ambayo haijapoteza mchezo wowote hadi sasa.

Baada ya mchezo huo kocha Kaze ameweka wazi kuwa, hata kabla ya mchezo huo, alijua kuwa wanakutana na timu inayojilinda sana hivyo matokeo yataamuliwa zaidi kwa mipira ya faulo kwani walishawaona na kusoma mbinu zao katika video za mechi zao zilizopita.

“Tulikuwa tunajua tunakutana na mpinzani wa aina gani na hata baada ya kutufunga mapema bado vijana wangu walipambana licha ya mwanzo kuwa na presha na kupoteza pasi lakini waliweza kurudi mchezoni jambo lililotusaidia kusawashinda na kupata magoli mengine yaliyotupa ushindi,” amesema Kaze.

Kuhusu mabeki wake, Kaze amesema kuwa, toka awali alijuwa kuwa wachezaji hao ni wazuri hasa katika mipira iliyokufa na wangekuwa na msaada mkubwa kwao jambo linaloongeza morali ya upambanaji kwa timu.

Amesema, hadi sasa muunganiko imara wa walinzi hao wa kati Lamine na Bakari Mwamnyeto kumemlinda zaidi kipa Metacha Mnata katika eneo lake kwani wamekuwa wakifanya kazi ya ziada pia kwa kuwasaidia walinzi wa pembeni.

Kitendo hicho pia kimeendelea kuwaweka salama kwani katika mechi 16 ambazo wamezicheza hadi sasa, Yanga imeruhusu goli sita pekee lakini wakifanikiwa kupachika wavuni goli 25 baada ya hivi karibuni kuanza kupata ushindi wa goli nyingi na kupunguza presha aliyokuwa nayo kocha Kaze.