October 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Ali Mohamed Shein na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan na viongozi wengine wakiwasili kwenye sherehe za kuzindua Mfumo wa Ukusanyaji Mapato kwa Njia ya Kielektroniki Kijitonyama jijini Dar es Salaam Juni Mosi, 2017. Serikali imepiga hatua kubwa ya ukusanyaji mapato nchini, hatua ambayo imewezesha utekelezaji wa miradi ya kihistoria nchini.

Safari ya miaka mitano, tumefika wapi?

Na Hudson Kamoga

SHALOM. Asalaam Alyekhum. Tumsifu Yesu Kristo,kwanza nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa Rehema aliyetukirimia baraka na uzima tele kwa kuilinda nchi yetu.

Mungu ameendelea kutuongoza katika vita ya kupambana na virusi vya corona (COVID-19) ambayo kwa kiasi kikubwa sana tunaendelea kuishinda.

Watanzania wametupilia mbali hofu, wameendelea kuchukua tahadhari zote, wameendelea kuchapa kazi na kujenga uchumi wa nchi yetu.

Tumeona watalii kutoka nchi mbalimbali duniani wameanza kuingia nchini, hii inaonyesha dhahiri shahiri kwamba wameridhishwa na namna ambavyo watanzania na serikali yao chini ya Rais Dkt.John Pombe Magufuli ilivyojizatiti kuhakikisha usalama wao.

Mataifa makubwa yamebaki mdomo wazi, maana walijua tutashindwa na matarajio yao ya kuokota maiti za Waafrika barabarani kumbe zimeshindwa, maana tunaye Mungu tuliamua kumkimbilia kwanza. Yeye ambaye uhai wa binadamu uko mikononi mwake. Tanzania na Rais wake wameonyesha njia na Dunia inafuata.

Leo natamani kwa pamoja tujiulize swali hili muhimu katika maisha, ili kufanya tathimini binafsi ya maendeleo yetu kama nchi.

Waswahili tuna misemo yetu ‘bhana’! “Safari hatua” ,”Maisha ni safari” na mingine mingi. Basi kwa muktadha huo; katika kampeni za uchaguzi wa 2015, watanzania wote bila kujali vyama walisema wanataka mabadiliko, watanzania walikuwa wamechoshwa na utendaji kazi wa baadhi ya watendaji wa serikali usijali maisha yao na badala yake kujijali maisha yao na familia zao.

Watumishi wa umma hasa wenye nafasi za juu maisha yao na watanzania wengine yalikuwa ni kama peponi na kuzimuni, wao siku za sikukuu walikuwa ni Ulaya, kutibiwa Ulaya, kupumzika wikiendi mjini Dubai, China na kwingineko.

Watanzania wakasema hapana, tumechoka, tunataka mabadiliko na kiongozi atakayekomesha hili. Watanzania walitaka madadiliko katika usimamizi wa rasilimali zao, walitaka kiongozi anayetambua utajiri wa nchi hii na wampate kiongozi mwenye uchungu wa dhati na mali ya Tanzania na atakayeisimamia kwa dhati kwa maslahi mapana ya taifa.

Walitaka wampate kiongozi ambaye toka ndani ya moyo wake anayechukia haswa rushwa na ufisadi na atakayewashughulikia hasa wala rushwa na mafisadi ili kuhakikisha wananchi wanapata maendeleo na si wachache kunufaika na utajiri wa nchi hii. Wakasema tunataka mabadiliko.

Kwa msingi wake Watanzania walitaka mabadliko katika nyanja mbalimbali na mabadiliko hayo yaonekane kwa vitendo.

Na kila mgombea kwa nafasi zao walinadi namna watakavyoweza kukidhi kiu hiyo ya wananchi ya kutaka mabadiliko.
Chama Cha Mapinduzi (CCM) kupitia mgombea wake, Dkt.John Pombe Magufuli kikapata ridhaa ya wananchi, kwamba kupitia dereva wake mgombea kiti cha urais kwa safari ya miaka mitano, basi iwafikishe wananchi kwenye hayo mabadiliko chanya iliyoahidi kupitia kauli mbiu yake ya ‘Hapa Kazi Tu’.

Sasa swali kwetu la msingi sana ni kujiuliza hivi katika safari hii ya miaka mitano, tumefika wapi? Yale yaliyoahidiwa kwenye majukwaa ya kampeni, yametimizwa au yanaendelea kutimizwa?. Swali hili ni kwa kila mgombea kwa nafasi yake.

Mathalani kwa waheshimiwa wabunge wetu. Hivi karibuni Mheshimiwa Rais Dkt.John Pombe atakwenda bungeni kulihutubia Bunge la 11 na kulivunja kwa mujibu wa katiba yetu, na hivyo kufikia ukomo wa wabunge wetu. Kwa maana nyingine safari ya miaka yao mitano ndio inakuwa imeishia hapo.

Sasa wajibu wetu sisi kama wananchi ni lazima tuwaulize wabunge wetu kwa dhati kabisa na tuchunguze wenyewe pia kwa makini;

Mosi, jukumu kubwa la Mbunge bungeni ni kuwakilisha mawazo yetu katika chombo kile kikubwa cha heshima cha maamuzi. Je, katika miaka hii mitano alikuwa anawakilisha mawazo yetu?.

Amewakilisha ipasavyo changamoto za jimbo letu? Alikuwa anatetea maslahi yetu au maslahi yake?. Pili kazi nyingine ya wabunge ni kupitisha bajeti ili serikali tekeleze mipango yake kwa kutumia bajeti hiyo, hivyo wabunge kwa niaba yetu wanapata fursa ya kujadili na kupitisha bajeti ili serikali itekeleze na isipotekeleza ni wajibu wao tena kwa niaba yetu kuihoji serikali, kwa nini haikutekeleza kama ilivyopitishwa.

Sasa tujiulize wabunge wetu wakati wa bajeti walipisha hii miradi tunayoiona kwenye majimbo yetu? Angalia miradi barabara, maji, umeme, shule, afya, kilimo, mifugo na miradi mingine mingi.

Tujiulize katika kupitisha bajeti iliyotekeleza haya, mbunge wetu alishiriki au alikuwa kikwazo? Je, hivi hakuwa anagomea maendeleo yetu? Hivi katika uwakilishi wake bungeni, aliyokuwa anayafanya ndio tuliyomtuma kweli?
Hivi ni kweli mawazo yetu kama wananchi wa jimbo lake yalikuwa ni kugomea bajeti? Hivi ni kweli sisi tulimwambia awe anapinga tu hata miradi ya maendeleo tunayopata?.

Haya ni machache tu katika mengi ambayo kila mwananchi anayependa maendeleo ya nchi atajiuliza na kumpima kiongozi wake wa ubunge, udiwani na uwakilishi ili kuona kama amekidhi matakwa yetu kama wananchi wa jimbo lake, kata au sheia yake. Lazima tujitathmini katika safari hii miaka mitano.

Na wakati tunaelekea kwenye kipindi kingine cha uchaguzi mkuu, tutakuwa na kampeni, najua watajitokeza tena na ahadi zao nyingine, tujiulize hivi tunataka tena wakafanye yale yale yao kwa kipindi kingine cha miaka mitano ijayo.

Wakati mgombea urais anaomba kura alisema, “Nitatoa elimu bila malipo, nitaimarisha miundombinu ya barabara katika miji, mikoa na kujenga madaraja, nitapunguza msongamano wa barabara mijini kwa kujenga Tazara flyover, Ubungo interchange,nitasimamia nidhamu kwa watumishi wa umma,nitasimamia ukusanyaji wa mapato na kudhibiti mianya ya upotevu wa mapato, nitadhibiti rushwa na ufisadi, kutakuwa na umeme wa uhakika, nitarejesha shirika imara la ndege,”alisema hayo na mengine mengi.

Swali la msingi la kujiuliza, katka miaka hii mitano, haya tunayaona? Kwa mtu aliyekaa nje ya Tanzania kuanzia kabla ya uchaguzi mkuu 2015, halafu akarudi nchini leo na pengine si mtu anayejihusisha sana na mitadao ya kijamii, ukweli ni kwamba anaweza akadhani amepotea kidogo.

Maana atakuja na taswira ya uwanja wa zamani wa ndege, ghafla atajionea maajabu, akifika Tazara atashangaa, akifika ubungo ataduwaa tu.

Tumshukuru Mungu kwa kutupatia dereva bora, makini, mwenye maono mapana aliyetusafirisha salama, kwa mwendo wa kasi, mwenye ‘control’ nzuri, maana katika mazingira magumu tumepita salama, kwenye milima tumeona uwezo wake, kwenye mteremko ametumia breki vizuri, kwenye tambarare mwendo ‘mdundo’. Safari inaendelea, na abiria tuko salama na tunafurahia safari.

Tutaendelea kumshukuru Mungu maana ametupatia kiongozi bora Dkt. John Pombe Magufuli.
Mungu Ibariki Tanzania

#NiUzalendTu.