December 28, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Sababu za watoto wa kike kuacha shule zatajwa

Na Lubango Mleka, Timesmajira Online – Nzenga.

WANAFUNZI wa Kike shule za sekondari Halmashauri ya Wilaya ya Nzega wanaonufaika na mradi wa Arudi Shule unaofadhiliwa na shirika la Msichana Initiative wameeleza sababu mbalimbali za mabinti kuacha masomo wilayani hapa.

Wanafunzi hao zaidi ya 175 ambao wamerudishiwa tabasamu la kutimiza ndoto zao za kupata elimu baada ya kupata fursa ya kurudishwa shule na kuendelea na masomo, baadhi yao kutoka shule ya Sekondari Nkiniziwa na Tongi pamoja na vijana wafeminia kutoka Kata tano za Tongi, Nkiniziwa, Utwigu, Mizibaziba na Mwakashahara kwa nyakati tofauti wameeleza kuwa hangamoto kubwa zinazowakumba ni ndoa za utotoni.

Mfumo dume kutoka kwa wazazi wa kiume, umbali kutoka nyumbani hadi shule ilipo, uelewa mdogo wa jamii juu ya mtoto wa kike kupatiwa elimu.

“Kwanza nashukuru sana Shirika la Msichana Initiative kwa kuniwezesha kuendelea na masomo yangu, sisi watoto wa kike tuna changamoto kubwa hasa zinazotukumba na kutufanya kuacha masomo ni hali ngumu ya maisha kwa wazazi, kufanya vibarua muda wa masomo,utoro, magonjwa, umbali na hata mabinti wengine kuolewa,”amesema Anna.

Huku Teodori Merikiori amesema kuwa, ili kuepukana na changamoto hizo wanaomba kujengwa kwa mabweni ya watoto wa kike katika shule za sekondari, kuwapatia baiskeli pia serikali na wadau kuisimamia na kutilia mkazo mkali sheria ya mtoto, sheria ya ndoa na ukatili wa kijinsia, kutoa elimu juu na kuhamasisha jamii kumsomesha mtoto wa kike na faida zake.

Kwa upande wake Ofisa Ustawi wa Jamii Halmashauri ya Wilaya ya Nzega, Hadija Idrisa, amelipongeza shirika hilo kupitia mradi wake wa Msichana Cafe kwani umewapa mchango mkubwa wasichana wa Nzega katika Kata 10 kukutana na kujadili changamoto zao, kuwapa elimu ya ukatili, sheria ya mtoto na sheria ya ndoa, kwani umewakutanisha waathirika wa vitendo vya ukatili wa kijinsia na mimba za utotoni.

Mradi huu umewakutanisha waathirika wa mimba za utotoni, waliopitia ukatili wa kijinsia na changamoto nyingi ambazo zimekuwa kikwazo kwa wao kutimiza ndoto zao.

Ambapo wamekutana na kupewa elimu juu ya kuweza kutoa taarifa kwa matatizk kama hayo na kuwa mfano kwa wasichana wengine.

“Hata kwetu sisi umekuwa mkombozi kwani tunaona faida nzuri kwa kupata mrejesho kutoka kwa wasichana wenyewe, tumekuwa tukipokea simu mbalimbali kutoka kwa watu ambao sio wasichana walioguswa na mradi huu na wanaufahamu,”amesema Hadija.

Naye mmoja wa wazazi , Merikiori Malusa amelishukuru shirika la Msichana Initiative kwa kuwatatulia changamoto zilizokuwa zinawakabili hadi kupelekea kuacha au kuwaachisha watoto wao wa kike shule.

Hivyo amewaomba viongozi wa serikali kushirikiana na shirika hilo kutoa elimu kwa jamii, kusaidia wanafunzi wenye changamoto mbalimbali kama vile ukosefu wa sare za shule, madaftari, viatu na mahitaji mengine.

“Shirika la Msichana Initiative limekuwa mkombozi kwangu baada ya kumrudisha shule binti yangu Teodori Merikiori aliyepata ujauzito, kwani amepatiwa mahitaji yote ya msingi ya shule na sasa anaendelea na masoma, nina ahidi kuwa balozi kwa wenzangu kwa kuwapatia uelewa juu ya haki za mtoto wa kike kupata elimu,” amesema Merikiori.

Sanjali na hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Msichana Initiative Rebeca Gyumi, amesema kuwa lengo la kufanya ziara wilayani Nzega ni kutembelea mradi wa Arudi Shule ulioanza mwaka 2021 ili kuwasaidia wasichana walioacha shule waweze kurudi na kuendelea na masomo yao.

” Tunaunga mkono juhudi za Serikali za kuamua kumrudisha shuleni mtoto wa kike aliyeacha shule kwa sababu mbalimbali, kupitia waraka namba 2 wa mwaka 2021 na muongozo wa elimu wa mwaka 2022, dira yetu kubwa ni kumtengeneza msichana anayeheshimiwa katika jamii na haki zake zinaheshimiwa hasa katika kupata elimu,”amesema Gyumi.

Ameeleza kuwa kwa sasa wanafanya kazi katika mikoa mitatu ya Dar es salaam, Dodoma kwa wilaya za Bahi na Kongwa pamoja na Tabora katika Wilaya ya Nzega na wemewafikia watoto wa kike zaidi ya 300 ambao wanapata elimu kwenye vituo na shule mbalimbali.

“Bado kuna changamoto ya uelewa katika jamii hasa fursa ya mtoto wa kike kupata elimu, tunajifunza kutoka kwa mabinti wengi bado wana ari ya kusoma ila kuna changamoto zinazowakumba kutoka katika jamii zao, kwa hapa Wilaya ya Nzega tumefikia watoto wa kike 175 na wanaendelea na masomo vizuri,” amesema Gyumi.

Gyumi, amewaomba wadau mbalimbali wa elimu nchini kwa kushirikiana na shirika la Msichana Initiative na Serikali kuendelea kupaza sauti kwa jamii zinazo endeleza mila, desturi na tamaduni zinazo mkandamiza mtoto wa kike kutokupata elimu.

Pamoja na kusaidia kutoa mahitaji ya shule kwa watoto ambao wazazi wao wanashindwa kumudu gharama kutokana na umasikini ili watoto hao wasikatishe ndoto.