Judith Ferdinand, Timesmajira Online, Mwanza
Imeelezwa kuwa moja ya sababu inayochangia vifo vinavyotokana na uzazi ni pamoja na wajawazito kutopata matibabu sahihi kipindi cha ujauzito.
Hayo yameelezwa na Mratibu wa Huduma za Mama na Mtoto Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela Nyabwire Lukumay wakati akiwasilisha taarifa yake ya Januari hadi Novemba mwaka huu katika kikao kazi cha tathimini cha viashiria mbalimbali katika huduma za afya zinazotolewa na vitengo vinavyopatikana katika Divisheni ya Afya, Huduma na Lishe.
Tathimini hiyo kwa kipindi cha Januari hadi Novemba 2023 imelenga kuboresha na kupima utendaji kazi kwa waliofanya vizuri na waliofanya vibaya ili kuweza kuweka mpango kazi wa mikakati kwa ajili ya maboresho katika maeneo ambayo walifanya vibaya.
Sambamba na kujadili vifo vya mama wajawazito na watoto wachanga ili kuweza kufahamu sababu zilizosababisha na kutengeneza mpango kazi wa kuboresha ili kuzuia na vifo hivyo.
Nyabwire ametaja visababishi vya vifo vya wazazi kuwa ni wajawazito kutopata matibabu sahihi kipindi cha ujauzito, ufuatiliaji hafifu wa wajawazito wanaogundulika na vidokezo hatari pamoja na kutowafuatilia wakina mama wenye uchungu pingamizi.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Huduma za Uchumi, Afya na Elimu Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela ambae ni Diwani wa Kata ya Ibungilo Hussein Magera, ameeleza kuwa tathimini za utendaji kazi na mabadilishano ya uzoefu na changamoto yatasaidia uboreshaji wa utoaji wa huduma za afya katika vituo vya kutolea huduma za afya ndani ya Wilaya ya Ilemela.
Huku akiwapongeza watoa huduma za afya wa Halmashauri hiyo na kuwataka kutovunjika moyo katika kutoa huduma bora kwa wananchi.
“Tathimini ya utendaji kazi wetu inatupa picha ya namna bora ya kufanya pia tunabadilishana mawazo, itatusaidia namna ya kubadilishana changamoto tulizonazo kwani changamoto za Sangabuye haziwezi kuwa sawa na za Buzuruga,”amesema Magera.
Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela Dkt. Marwa Samson amefafanua kuwa lengo la kikao hicho cha tathmini ni kupata uhalisia wa taarifa za utoaji huduma zinazotolewa na vituo vya afya na zahanati katika mitaa na kata walipo wananchi
Nae Katibu wa Afya wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela Emila Msengi amesema kuwa ipo haja ya kushawishi na kufanya zoezi la utoaji wa elimu ya afya kuwa ajenda ya kudumu katika vikao vya Kamati za Maendeleo za ngazi za mitaa na kata (WDC)
Mganga wa zahanati ya Nyerere Kata ya Buswelu Leah Matondo,amesema kupitia kikao hicho ameweza kupata uzoefu mpya sanjari na kushauri utaratibu huo uwe endelevu ili wataalam wa sekta ya afya waweze kupata uzoefu mpya na kubadilishana changamoto wanazokutana nazo katika kuhudumia wananchi.
More Stories
Maofisa Watendaji watakiwa kufanya kazi kwa weledi
Muhoji Sekondari kumaliza changamoto ya umbali kwa wanafunzi Musoma vijijini
Tanzania mwenyeji mkutano wa nishati wa Wakuu wa Nchi za Afrika