November 8, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Saba kizimbani kwa kuingilia miundombinu ya umeme

Na Mwandishi Wetu,TimesMajira, Online,Dar es Dalaam

WATU saba wakazi wa Ukonga Jijini Dar es Salaam, wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wakikabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi kwa kuisababishia hasara TANESCO.

Washtakiwa ni Mwalimu Boniphace Singaille (48) Twalibu Kasamu (32), Mwarami Mussa (45), Vumilia Kambi na Haidary Hassan (35).

Wamesomewa mashtaka yao na Wakili wa Serikali Mkuu, Materus Marandu akisaidianaia na Kija Luzungana, mbele ya hakimu  Mkazi Mkuu Kassian Matembele.

Wakili Marandu amedai,washtakiwa kwa pamoja na wenzao wawili ambao ni wagonjwa wanadaiwa Januari 2018, eneo la Kichangani Ukonga Madafu,  waliingilia miundombinu inayotumika kutoa huduma muhimu kwa kutoa mita ya TANESCO kutoka katika kiboksi kinachohifadhia mita na kuifunga moja kwa moja.

Pia,kati ya Januari 18 na Agosti 2020 katika eneo hilo,washitakiwa wote kwa makusudi waliingilia mita ya umeme wa TANESCO na hivyo kuisababishia hasara ya S. 6,868,910.

Upande wa mashtaka umedai upelelezi haujakamilika na kwamba wanaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.

Hakimu Matembele amesema kosa hilo linadhamini kwani thamani ya mali wanayodaiwa washtakiwa hao kuisababishia hasara TANESCO ni chini ya Sh.milioni 10 .

Ametaja masharti ya dhamana, Hakimu Matembele alisema kila mshtakiwa anatakiwa kuwa na wadhamini wawili, mmoja kutoka Taasisi inayotambulika kisheria, atakayesaini kusaini bondi ya Sh.milionin 1.

Mdhamini mwingine anatakiwa kuwa na barua kutoka Serikali ya Mtaa inayowatambulika ikiwa imeambatanishwa na picha ndogo ya rangi (passport).

Washtakiwa wameshindwa kutimiza masharti ya dhamana na kesi hiyo itatajwa tena, Desemba 16,2020.