December 22, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mchungaji, Askofu, Dokta Getrude Rwakatare

Rwakatare kuzikwa jijini Dar leo

Na Mwandishi Wetu

MAZISHI ya mwanzilishi wa Kanisa la Mlima wa Moto (Mikocheni B Assemblies of God ) Mchungaji Getrude Rwakatare (70), yanatarajia kufanyika leo jijini Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa utaratibu uliotangazwa juzi Bungeni jijini Dodoma na Spika wa Bunge, Job Ndugai, mazishi ya Mchungaji Rwakatare yatahudhuriwa na washiriki wasiozidi 10. Alisema walipata taarifa kutoka kwenye familia wakipendekeza mazishi yake yafanyike Mikocheni, jijini Dar es Salaam eneo la Kanisa la Mlima wa Moto

“Mazishi ya Mchungaji Rwakatare yatafanyika Alhamisi (kesho) na Serikali ndiyo itakayosimamia mazishi hayo ambayo washiriki wake hawatazidi 10,” alisema Spika Ndugai na kuongeza; “Sisi wabunge lazima kuielewa Serikali na ushiriki wetu uwe ni kwa kadiri tunavyopewa maelekezo na Serikali.”

Mchungaji Rwakatare alifariki Jumatat alfajiri jijini Dar es Salaam. Kwa mujibu wa mtoto wake, Muta Rwakatare,  Mchungaji Rwakatare alikuwa akisumbuliwa na shinikizo la damu.

“Ni bahati mbaya imetokea, alikuwa na matatizo ya moyo, jana tulimkimbiza hospitali lakini bahati mbaya imetokea, tupo katika hatua ya kuangalia namna gani tutafanya ili tuweze kumpumzisha mama yetu,” alisema juzi Muta.