November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Ruwasa,Tanesco watakiwa kupunguza malalamiko

Na Hadija Bagasha, Timesmajira Online

Mkuu wa wilaya ya Lushoto Mkoani Tanga Kalist Lazaro amesema migogoro mingi inayotokea kati ya mipaka ya kijiji na kijiji inatokana na maslahi binafsi ya viongozi wa maeneo hayo baada ya kuibuka kwa fursa mbalimbali za kiuchumi.

Pia Kalist amewataka watendaji wa Taasisi za Ruwasa na Tanesco wilayani humo kupunguza malalamiko kwenye ofisi zao na badala yake wahakikishe wanawaletea wananchi maendeleo kwa haraka na hatimaye kupunguza malalamiko kwa serikali.

Mkuu huyo wa wilaya ya Lushoto ametoa kauli hiyo mara baada ya kuwasilisha taarifa ya utekelezaji wa ilani ya chama cha mapinduzi CCM kwenye kwenye kikaoc cha halmashauri kuu ya chama chicho.

Kalist amesema wilaya hiyo kwa kushirikiana na wilaya ya Korogwe wamejiwekea utaratibu wa kufanya mikutano ya pamoja ili kutoa uelewa kwa wananchi ili waachane na migogoro ya aina hiyo na kwamba katika eneo hilo migogoro hiyo itakuwa ya kihistoria.

“Mwananchi hana mipaka, mipaka ya kiutawala haiwezi kuleta migogoro kinacholeta migogoro ni maslahi ya viongozi wa vijiji baada ya fursa kutokea kwa mfano eneo likigundulika madini kila mtu anavutia kwake au ikigundulika kwamba eneo lina maslahi ya misitu wanataka iwe kwao ili badae wavune, ikigundulika ardhi ya kuuza anataka awauzie wawekezaji wa mkonge ndio mgogoro unaanzia hapo kwahiyo mgogoro uliopo kimsingi ni mgogoro wa kimaslahi wa viongozi, “alisisitiza DC Kalist.

Aliongeza kuwa inapojitokeza fursa kwamfano kwenye eneo lenye mashamba ya mkonge watu wengi baada ya uhamasishaji wa zao la mkonge watu wanakimbilia mashamba kule mashamba yamekuwa ni dili kwa wenyeviti wa vitongoji kwahiyo wanavutana kimsingi wananchi hawana shida kulima upande wowote kwamaana ya kwamba mwananchi wa korogwe kulima lushoto au wa lushoto kulima korogwe sio mgogoro bali mgogoro unatokea kwenye mamlaka za vijiji kwamba kila mmoja anavutia kwake, “alibainisha Mkuu wa Wilaya Kalist.

Katika hatua nyingine Mkuu wa Wilaya ameziagiza taasisi hizo za Ruwasa na, tanesco kuwaondolea wananchi kero mbalimbali ambazo zimekuwa zikijirudia mara kwa mara kwani mkakati uliopo mpaka mwezi desemba vijini vyote vinatakiwa kuwekewa umeme wa Rea kisha ufuate utaratibu wa vitongoji.

“Kiongozi unapoona maswali yamekuwa mengi maana yake kuna jambo halijakaa sawa kuna eneo haliridhishi kwahiyo maswali yao maoni yao na ushauri wao kwetu ni chachu ya kuongeza jitihada ya kuhakikisha tunaposoma ilani ijayo tutakuwa tumepunguza matatizo mengi, “alisema DC

Madiwaniwa halmashauri ya Lushoto akiwemo Jambia Juma Shehoza wa kata ya Mng’aro na Dhahabu Jumaa wa kata ya Vuga wamesema migogoro ya mipaka inaathiri shughuli za kiuchumi kwenye maeneo yao hivyo ipo haja ya kuchukua hatua za haraka.

Ikupa Mwasyoge ni mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Lushoto hapa ameipongeza serikali chini ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa namna ambavyo imekuwa ikitekeleza miradi mbalimbali ikiwemo ya elimu, afya na barabara kwa ajili ya kuwaletea wananchi wa Lushoto maendeleo.

Maeneo yenye mgogoro wa mipaka ni Vuga wilaya ya lushoto na Mombo wilaya ya Korogwe, Korogwe vijijini na kata ya Umba wilaya ya Lushoto, Mashewa wilaya ya Korogwe na Mahezangulu wilaya ya Lushoto.