December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

RUWASA kuongeza upatikanaji wa maji vijijini ifikapo 2025

Na Judith Ferdinand, TimesMajira Online, Mwanza.

Wakala wa Huduma za Maji Vijijini (Ruwasa) katika kuhakikisha inapanua wigo wa utoaji wa huduma imepanga kutumia zaidi ya bilioni 88 kwa ajili ya kupeleka huduma ya maji vijijini ifikapo 2025.

Akizungumza na watendaji wa Ruwasa Mkoa wa Mwanza kwenye kikao kazi cha kukumbushana na kujengeana uwezo wa majukumu yao, Meneja wa Ruwasa Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Godfrey Sanga amesema hivi sasa wapo kwenye usanifu wa miradi miwili ya mwisho ili kuanza utekelezaji.

Mhandisi Sanga ameeleza kuwa kukamilika kwa miradi hiuo mikubwa itaongeza utoaji wa huduma ya maji kwa watu wote wanaoishi maeneo ya vijijini na watakuwa wamevuka malengo ya ilani ya Chama Cha Mapinduzi ambayo ilipanga kufikisha maji maeneo hayo kwa asilimia 85 ifikapo mwaka 2025.

“Kiwango ambacho kitaongezeka kwa asilimia 7,hivi sasa tunatoa huduma hiyo kwa asilimia 67 na kupitia miradi mipya mitano iliyosainia hivi karibuni itaongeza utoaji wa huduma ya maji kwa asilimia 25 na hivyo kufikisha utoaji wa huduma hiyo kwenye vijiji vyote nchini kufikia asilimia 92 ifikapo 2025,,”ameeleza Mhandisi Sanga.

Aidha ameeleza kuwa zipo changamoto zinazorudisha nyuma utendaji kazi wa Ruwasa ambapo baadhi ya wananchi katika maeneo hayo wanahujumu miundombinu hivyo kurudisha nyuma shughuli zao pamoja na ukosefu wa usafiri unaosaidia watendaji kufika kwenye maeneo ya miradi kwa wakati.

Kwa upande Kaimu Meneja wa Ruwasa Wilaya ya Misungwi, Marwa Kisibo amesema pamoja na mafanikio ya miradi katika wilaya hiyo changamoto kubwa ni wananchi kushindwa kulipa ankra za maji kipindi cha masika.

Ambapo ameeleza kuwa kwenye kipindi cha masika makusanyo ya maji yanakuwa madogo kwakuwa wananchi badala ya kutumia maji ya bomba wao wanatumia maji ya mvua na visima ili kukwepa gharama hali inayosababisha makusanyo kuwa madogo.

Watendaji wa Wakala wa maji vijijii Ruwasa wakimsikiliza Meneja wa Ruwasa Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Godfrey Sanga( hayupo pichani) kwenye kikao kazi kilichofanyika jijini Mwanza.( Picha na Judith Ferdinand)
Meneja wa Ruwasa Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Godfrey Sanga akizungumza kwenye kikao kazi kilichofanyika jijini Mwanza.( Picha na Judith Ferdinand)