Na Allan Vicent, TimesMajira Online, Tabora
WASWAHILI husema kila penye nia pana njia, hivyo ndivyo tunavyoweza kusema baada ya serikali kutimiza dhamira yake ya kumaliza kero ya maji kwa wakazi wa vijijini kwa kuanzisha Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) kwa ajili ya kushughulikia kilio hicho.
Katika Makala haya nimefuatilia baadhi ya miradi ya maji inayotekelezwa na RUWASA Wilayani Igunga Mkoani hapa na kubaini kuwa maeneo yote ambayo miradi hiyo imetekelezwa maisha ya wananchi yameanza kubadilika.
Wakazi wa Vijiji ambavyo miradi hiyo imekamilika wanaeleza jinsi miradi hiyo ilivyobadilisha maisha yao hasa ikizingatiwa kuwa hawakuwa na ndoto yoyote kwamba siku moja huduma ya maji safi na salama ya bomba itafika kijijini
Wanatoa ushushuda
Mwalimu Zebedayo Mwampembe, mkazi wa kijiji cha Iborogelo anaeleza kuwa tangu azaliwe hadi anastaafu hakuwahi kuota kuwa siku moja watapata maji safi ya bomba lakini sasa yametimia, na manufaa ya maji hayo wameanza kuyaona.
Anaeleza kuwa RUWASA imebadilisha maisha ya jamii, kwani wananchi wengi walikuwa hawaogi hata kwa wiki nzima, hivyo suala la usafi lilikuwa mtihani, lakini sasa mambo yamebadiika, neema imekuja, maji ya bomba hadi kijijini
Mariamu Kigwangala mkazi wa Kijiji cha Nyandekwa anaeleza kuwa mbali na kuwafanya kuwa wasafi pia miradi hiyo imewaongezea kipato akina mama walio wengi kupitia miradi ya mamantilie na kuuza maji ya viroba kwa bei ya sh 20.
Anaongeza kuwa hata makazi yao sasa yamebadilika tofauti na huko nyuma, anaeleza kuwa ujio ya maji ya bomba umeleta neema kubwa kwa wananchi hasa wakazi wa vijijini, kwani hata magonjwa ya kuhara, vidonda vya tumbo, vipele mwili mzima na mifugo kufa kwa kukosa maji sasa yamekwisha.
Meneja wa RUWASA aeleza mafanikio
Meneja wa Wakala huo Wilayani hapa Mhandisi Marwa Sebastian Muraza anaeleza kuwa dhamira ya serikali ya kumtua ndoo kichwani mama wa kijijini imeanza kutimia kupeleka fedha za kutosha kwa ajili ya utekelezaji miradi hiyo.
Anasema kuwa takribani vijiji vyote katika kata 35 za wilaya hiyo kuna miradi ya maji inayoendelea kutekelezwa ikiwemo ya visima virefu na hata pale ambapo visima vimeharibika fedha zimetengwa kwa ajili ya matengenez
Anaeleza kuwa miradi hiyo imekuwa mkombozi kwa wananchi kwani awali walikuwa wanakunywa yasiyo salama ambayo yalipelekea afya zao kutetereka hivyo kushindwa kutekeleza majukumu yao ya kila siku.
Anaongeza kuwa miradi hiyo imekuwa kichocheo kikubwa cha shughuli za kiuchumi kwani wazazi wengi sasa hawapotezi muda kwa kwenda kutafuta maji mtoni au kwenye madimbwi, kila mmoja anafanya kazi zake kwa wepesi zaidi.
Ataja miradi iliyotekelezwa
Mhandisi Sebastina anasema katika mwaka wa fedha uliopita wa 2022/2023 jumla ya miradi 11 yenye thamani ya sh bil 8 ilitekelezwa na mingine utekelezaji bado unaendelea, na hadi sasa kiasi cha sh bil 5.6 kimeshatumika katika miradi hiyo.
Anataja vijiji ambavyo wananchi wake sasa wananufaika na miradi hiyo kuwa ni Mwazizi, Bukoko, Ibologero, Imalilo, Matinje, Ziba, Igumila, Nyandekwa, Mwamakingi, Mwamala, Kazima na Mgunga.
Vijiji vingine ambavyo viko mbioni kupata huduma hiyo ni Ntigu, Moyofuke, Matinje, Buchenjegele, Ziba, Nkinga, Nsimbo na Mangungu, vingine ni Mwasung’ho, Mwamapuli, Igogo, Igulubi, Matinje, Choma, Bukoko na Mtungulu.
Miradi mipya
Mhandisi Marwa Sebastian Muraza anabainisha kuwa katika mwaka wa fedha 2023/2024 jumla ya miradi 4 yenye thamani ya sh bil 9.967inatarajiwa kutekelezwa katika vijiji 41 ili wananchi waanze kupata maji safi ya bomba.
Anasema miradi 3 kati ya hiyo ni mwendelezo wa miradi iliyoanza kutekelezwa mwaka jana na ile iliyoko katika hatua za manunuzi ambayo utekelezaji wake unaanza mwaka huu ikiwemo mradi 1 wa kusaidia matengenezo makubwa.
Anaeleza kuwa kutekelezwa kwa miradi hiyo kutaongeza upatikanaji huduma ya maji safi na salama ya bomba katika wilaya hiyo kutoka asilimia 72 ya sasa hadi 89 hivyo kuvuka lengo la serikali la kufikia asilimia 85 ifikapo 2025.
Manufaa ya Mradi wa ziwa Victoria
Mhandisi Sebastian anaeleza kuwa serikali imeendelea kupanua mradi mkubwa wa maji ya Ziwa Victoria kutoka jijini Mwanza ambapo sasa vijiji vya Ziba, Nkinga, Mwanzelwa, Kitangili, Itulashilangi, Ulaya, Barazani, Ugaka, Ikunguipina, Njiapanda na Simbo vitaanza kunufaika na mradi huo.
Anaeleza kuwa upanuzi wa mradi huo utakaogharimu kiasi cha sh bil 4.5 utawezesha wakazi wa vijiji 4 vya Bukoko, Mtungulu, Matinje na Choma kunufaika.
Meneja anaeleza kuwa mradi huo pia utapanuliwa kutoka Igogo kwenda Igurubi ambapo utatekelezwa katika kata 8 na kunufaisha wakazi wa vijiji 18 vilivyoko katika kata hizo kwa gharama ya sh bil 5.2.
Anataka miradi mingineni ni ukarabati na matengenezo ya miradi ya maji ya bomba na visima iliyopo katika kata zote 35, utakaohusisha ununuzi wa vipuri, bomba, pampu, ufundi na gharama nyinginezo, sh mil 200 zimetengwa kwa ajili ya kazi hiyo.
DC ampongeza Rais Samia
Mkuu wa wilaya hiyo Sauda Mtondoo anatoa shukrani nyingi kwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuwapelekea fedha za kutosha ili kukamilisha miradi yote ya mwaka jana na mwaka huu , hakika KAZI IENDELEE.
Mwenyekiti wa Halmashauri apongeza
Mwenyekiti wa halmashauri hiyo Lucas Bugota anabainisha kuwa ufanisi mkubwa wa miradi ya maji vijijini unaofanywa na Wakala huo wilayani hapa unachangiwa na weledi mkubwa wa Meneja wa RUWASA Mhandisi Sebastian Marwa.
Anaeleza kuwa kama serikali kupitia Wizara ya Maji watamwacha katika kituo hicho cha kazi kwa miaka 5 au zaidi kero ya maji katika wilaya hiyo itabakia historia.
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri atoa neno
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyoJoseph Sambo anaeleza kuwa ujio wa RUWASA umekuwa neema kubwa kwa wakazi wa wilaya hiyo na umerahisisha kwa kiasi kikubwa utekelezaji shughuli za maendeleo.
Anaongeza kuwa miradi hiyo imemrahisishia kazi ya kuhamasisha shughuli za maendeleo, imeboresha usafi wa mazingira na kuchochea uchumi wa wananchi kwa kiasi kikubwa.
More Stories
Siri ya Rais Samia kutembea kifua mbelea kijivunia Mapinduzi Matukufu ya Z,bar
Rais Samia anavyotimiza ahadi yake ya kumtua ndoo ya maji mwanamke
Rais Samia anavyozidi kusogeza karibu watoto wa kike na kasi ukuaji teknolojia