March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rungwe yajivunia uzalishaji mazao yenye ubora

Na Esther Macha Timesmajira Online-Mbeya

HALMASHAURI ya Wilaya ya Rungwe mkoani Mbeya, imesema kuwa uzalishaji wa mazao umekuwa ukiongozeka mwaka hadi mwaka, kutokana na elimu ya ugani pamoja na Serikali kuweka ruzuku ya pembejeo kwa wakulima wilayani humo.

Kauli hiyo imetolewa Agosti 6,2025 na Majaliwa Mwalembe kutoka Ofisi ya kilimo ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe,wakati katika maonesho ya Nane Nane kwa wakulima ambayo kikanda yanafanyika jijini Mbeya kwenye viwanja vya John Mwakangale.

“Kazi yangu ni kutoa elimu kwa wakulima kufanya kilimo chenye tija ambacho kitaongeza uzalishaji ili waweze kuendesha maisha yao kwa ufanisi,”amesema Mwalembe.

Mwalembe amesema, katika Halmashauri hiyo kuna mazao ya chakula na biashara ikiwemo ndizi,mahindi,viazi, magimbi,maharagwe na mengineyo.

Amesema mazao ya biashara ni kahawa,chai,kokoa ambapo katika mazao hayo uzalishaji umekuwa ukiongozeka mwaka hadi mwaka kutokana na huduma ya ugavi na Serikali kuweka mazingira mazuri kwa wakulima.

“Ukiangalia uzalishaji wa zao la viazi umekuwa ukiongozeka mwaka hadi mwaka,hii inatokana na wakulima kufuata kanuni bora za kilimo ambapo wakulima kabla ya kulima mazao lazima wapime afya ya udongo ili kufanya utambuzi wa kuona shamba la mkulima limekosa kirutubisho cha aina gani “amesema.

Hata hivyo amesema upimaji wa udongo unafanya mkulima kufanya kilimo chenye tija kwake pia amesema kuwa maafisa ugani wanaendelea kutoa elimu kushauri wakulima watumie mbegu zipi ambazo zinatoa mazao mengi na kustahimili magonjwa.

Atuganille Juma ni mkulima kutoka Kata ya Kiwira Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe, anayejishughulisha na kilimo cha viazi amesema kupitia watalaamu wa Halmashauri hiyo,wamesaidia mabadiliko katika kilimo ambacho alizoea na hivi sasa amekuwa na mabadiliko kwa uzalishaji wa mazao mengi ambayo yamebadilisha mfumo wa maisha yake.

Lenatus Mpatili ni Ofisa Biashara Wilaya ya Rungwe,amesema Wilaya hiyo inahilimili mazao karibu yote hivyo kuifanya kuwa na uzalishaji mkubwa wa mazao.

Amesema kuwa wilaya ya Rungwe inazalisha viazi na ndizi,zenye ubora ambapo wafanyabiashara toka nje wanafika kujaza mzigo na kupelekea kwenye masoko na kusema ni biashara nzuri ambayo inawainua wakulima.