January 4, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

RPC Mbeya:Jeshi la Polisi tupo timamu kuhakikisha wananchi wanasherekea mwaka mpya kwa amani

Na Esther Macha,TimesmajiraOnline,Mbeya

KUELEKEA mkesha wa  sikukuu ya mwaka mpya jeshi la polisi mkoani Mbeya limejipanga kikamilifu katika kuimarisha ulinzi kwenye nyumba za ibada na wakati misa za mkesha ili kuhakikisha wananchi wanasherekea sikukuu hiyo kwa amani na utulivu.

Kauli hiyo imetolewa leo Disemba 31,2024 na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Kamshina msaidizi mwandamizi wa Polisi,(SACP) Benjamin Kuzaga mara baada ya mazoezi ya ukakamavu .

Kuzaga amesema kuwa Jeshi hilo limejipanga vizuri kuendelea kuimarisha doria za magari, miguu na Mbwa wa Polisi katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Mbeya.

Aidha Kamanda Kuzaga amepiga marufuku mtu yeyote kupiga au kulipua milipuko (Fataki) bila kuwa na kibali cha Jeshi la Polisi kwa kueleza kuwa ili kupiga fataki ni lazima mhusika awe ameomba na kupewa kibali na Jeshi hilo.

Pia, amesema  katika kuhakikisha usalama barabarani una kuwepo, Kamanda Kuzaga ameeleza kuwa kipindi hiki, Jeshi la Polisi Mkoani humo halitokuwa na muhali kwa mtu yeyote atakayekiuka sheria za usalama barabarani kwani elimu ya usalama barabarani imekwisha tolewa kwa madereva.

“Tutakuwepo katika maeneo yote tete, barabara kuu na katika milima Iwambi, Igawilo na Mlima Nyoka ili kudhibiti ukiukwaji wa sheria za barabarani, tunavyo vifaa vya kupima mwendo kasi, vipima ulevi hivyo tutachukua hatua kali za kisheria kwa yeyote atakayebainika kukiuka sheria” amesema Kamanda Kuzaga.

Kamanda Kuzaga ametoa wito kwa wananchi kuacha tabia ya kuchoma matairi barabarani kwa kufanya hivyo ni kuharibu miundo mbinu iliyowekwa na Serikali na  kutofanya  vurugu za aina yoyote badala yake washerehekee kwa amani na utulivu.