February 12, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

RPC Kuzaga ahimiza matumizi sahihi ya silaha

Na Esther Macha, Timesmajira Online, Chunya

KAMPUNI binafsi ya ulinzi na watu binafsi wanaomiliki silaha za kiraia wilayani Chunya mkoani Mbeya,wamehimizwa kuzingatia matumizi sahihi ya silaha ili kuepuka madhara yanayoweza kujitokeza kwao na kwa watu wengine.

Hayo yamesemwa Februari 10,2025 na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya,Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP),Benjamin Kuzaga,wakati akitoa mafunzo maalum kwa kampuni binafsi na wamiliki binafsi wa silaha za kiraia wilayani Chunya.

SACP.Kuzaga amewataka wamiliki wa silaha kuhakikisha wanatumia vizuri silaha hizo kwa ajili ya kujilinda wao wenyewe, kulinda raia na mali wanazomiliki dhidi ya wahalifu wanaovamia katika maeneo yao.

Huku akizitaka kampuni binafsi za ulinzi,kuimarisha ulinzi katika maeneo wanayopewa kazi ya kulinda,wamepewa kibali cha ulinzi kwa mujibu wa sheria ili kulisaidia Jeshi la Polisi kuimarisha ulinzi wa raia na mali zao.

“Imarisheni ulinzi maeneo yote mnayopewa, mna dhamana ya kuhakikisha usalama unakuwepo kwenye maeneo mnayolinda,”amesema Kuzaga.

Kwa upande wake mmiliki wa kampuni binafsi ya ulinzi ya Safank Security ya wilayani Chunya,Abubakari Athuman,amesema mafunzo hayo yanawakumbusha njia sahihi ya kumiliki na kutumia silaha kwa ajili ya ulinzi.

Huku akiahidi kuendelea kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi,katika kubaini na kuzuia uhalifu.

Mkaguzi Msaidizi wa Polisi ,Ally Mgaza,kutoka Kikosi cha Kutuliza Ghasia Mbeya,amewahimiza wamiliki kuhuisha vibali vya umiliki wa silaha za kiraia pamoja na kushiriki mazoezi ya ulengaji shabaha, yanayofanyika kila mwaka chini ya usimamizi wa Jeshi la Polisi kwa ajili ya kuwajengea uwezo na umahiri katika matumizi ya silaha za moto.