Na Esther Macha, Timesmajira Online, Chunya
Utaratibu wa kumtumia mwalimu wa saikolojia katika shule ya msingi Holyland iliyopo Mamlaka ya Mji Mdogo wa Makongolosi wilayani Chunya umempa somo pia umemkosha Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Benjamini Kuzaga.
Ambapo ameeleza kuwa ni utaratibu wa pekee ambao umelenga kumjenga mtoto kujiamini ili kumuepusha na ukatili wa aina yeyote.
Akizungumza wakati alipotembelea shule hiyo kwa ajili ya kutoa elimu ya ukatili wa kijinsia shuleni hapo Kamanda Kuzaga amesema shule hiyo ni ya mfano ambayo inafundisha saikolojia ambayo ni msaada kwa watoto.
“Shule zingine sijaenda sina uhakika kama walimu wapo na kama wapo nitashukuru sana serikali yetu kwa shule hii nimeona ni kitu tofauti sana kuna tofauti ya shule zingine nilizotembelea sijaona ubunifu kama huu wa wa shule Holyland”amesema Kamanda Kuzaga.
Hata hivyo Kuzaga amesema kuwa jeshi la Polisi nchini limeanzisha programu ya kutoa elimu kwenye vyuo, shule na mikutano ya hadhara lengo ni kufikisha elimu ya masuala ya ukatili wa kijinsia kuanzia ngazi ya chini.
“Watoto wengi wamekuwa wakifanyiwa ukatili wa kijinsia ndo maana tukasema twende kwenye shule sababu wanakuwa na walimu kwani nyumbani inawezekana wanafanyiwa ukatili lakini hawawezi kusema na hawana mahali pa kusema,kupitia kitengo chetu cha dawati la jinsia,wakuu wa vituo tukaona twende shuleni tuongee na walimu ambao wanaweza kutupa taarifa,”.
Mkurugenzi Mtendaji wa shule ya Holyland , Lawena Nsonda (Baba Mzazi)amesema kuwa amemshukuru Kamanda huyo wa Polisi Mkoa wa Mbeya na dawati la jinsia kutembelea shule hiyo na kuzungumza na wanafunzi.
“Walimu wetu wote hapa shuleni wamesomea saikolojia hivyo wakiona watoto wamepoa au kuteseka nyumbani hujenga urafiki na kuwa karibu na watoto hali inayosaidia kujua changamoto zao kisha kuzitatua na matokeo yake baadae hufanya vizur kimasomo,”amesema Nsonda.
Amesema elimu ya ukatili wa kijinsia iliyotolewa na dawati la jinsia itasaidia watoto hususani wakati wa likizo na watawahimiza wazazi kuwa nao makini kipindi hicho.
Loveness Mtemi ni Mkuu wa Dawati la Jinsia na Watoto Mkoa wa Mbeya amesema kuwa wamefika shuleni hapo kutoa elimu ya ukatili wa kijinsia ambayo itakuwa msaada kwa wanafunzi hao.
More Stories
Waziri Jerry afanya uteuzi wa Makamu Mwenyekiti, Wajumbe watano wa bodi ya Shirika la Posta
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa