Na Mwandishi wetu, timesmajira
TANZANIA imepokea meli ya kitalii kutokea Miami nchini Marekani iliyobeba zaidi ya watalii 300 na wahudumu zaidi ya 300 ikiwa ni mwendelezo wa matokeo ya Filamu ya Royal Tour iliyoongozwa na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa malengo ya kuitangaza Tanzania kimataifa kupitia vivutio vya utalii
Akizungumza wakati wa kupokea wageni hao leo kwenye Bandari ya Dar es salaam Mkurugenzi Mkuu wa Bandari hiyo Mrisho Selemani ,alisema Mamlaka ya Bandari imefurahi kupokea meli ya aina hiyo, (Cruise ships) ambazo hufanya ziara zake za kitalii katika mataifa mbalimbali lakini pia ameongeza kuwa bandari imejipanga vizuri kuhudumia meli hizo za watalii huku ikiweka malengo makubwa ya kujenga eneo maalum la kuhudumia meli hizo.
Amesema kufuatia kuwepo kwa meli kama hizo za kitalii, wamejipanga kujenga eneo maalum kwa ajili ya kuhudumia meli hizo kwani itawapa fursa nzuri ya kukuza uchumi ndani ya nchi pamoja na kuongeza uwepo wa meli kama hizo za kitalii kwani eneo wanalojenga litakuwa na kila kitu ambacho kitamhudumia mtalii kabla ya kwenda kwenye vivutio vyetu.
Kwa upande wake Kaimu Meneja wa Mikutano na Watalii Bodi ya watalii Liliani Fungamtama amesema kuwa, watalii hao wamekuja kwa malengo ya kutalii kwenye vivutio hapa nchini ambao kati yao wengine wameenda Zanzibar, Serengeti na wengine wamebaki hapa kwa ajili ya kutembelea maeneo ya vivutio vilivyopo ikiwa ni pamoja na kupita Soko la vitu vya asili Mwenge Vinyago na kwenye fukwe zilizopo jijini Dar es Salaam.
Amesema uwepo wa watalii hao hapa nchini ni katika juhudi za kumuunga mkono Rais Samia katika filamu yake ya The Royal Tour na kusisitiza kuwa jambo hilo litasaidia kuongeza idadi ya watalii nchini kwani malengo ni kufikia watalii milion 5 hadi ifikapo mwaka 2025.
“Yote hii ni kumuuunga mkono Rais wetu kwani sisi tunamhesabu kama Tour Operator namba moja katika kutangaza muendelezo wa filamu yetu ya The Royal Tour na itasaidia kuongeza idadi ya watalii nchini na kufikia lengo tulilojiwekea,” ameongeza Fungamtama
Naye Nahodha wa Meli hiyo ,Kyraikos Karras amesema safari ilianza January 6, Mwaka huu kutokea Miami kupitia bahari ya Pacific hadi kufikia Dar es Salaam hii leo, huku wakitarajia kukamilisha safari yao Mei 27,2023 huko nchini Hispania katika jiji la Barcelona.
Amesema watalii hao wanatarajiwa kuongeza pato la taifa na kukuza uchumi wa nchi hivyo kurahisisha upatikanaji wa fedha za kigeni na kuchochea shughuli mbalimbali za maendeleo hapa nchini.
Meli hiyo inatarajiwa kuondoka hapo kesho kuelekea nchini Afrika Kusini, ikumbukwe kuwa Novemba mwaka jana bandari ya Dar es Salaam pia ilipokea Meli ya kitalii ya Zaandam inayomilikiwa na Kampuni ya Holland America Line ikiwa na watalii 1060 ikiwa ni sehemu za safari za kitalii za meli hiyo kuelekea sehemu mbalimbali duniani.
More Stories
Zaidi ya wananchi 32,000 Vijiji vya Wilaya za Morogoro na Mvomero kuanza kupata mawasiliano
Wafanyabiashara waomba elimu ya namna watakavyorejea soko kuu
DCEA,Vyombo vya Ulinzi na Usalama vyafanya operesheni ya kihistoria