Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma
WAZIRI Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu,Vijana, Ajira,Kazi na wenye Ulemavu,Ridhiwani Kikwete ametoa wito kwa jamii kuepuka hali ya kuwanyanyapaa watu wenye ulemavu bali kuwapa fursa kama wanavyostahili watu wote katika jamii.
Vilevile amesema kuwa Serikali imeendelea kutoa Ruzuku ya Mafuta kinga ya Saratani ya ngozi kwa Watu wenye Ulemavu wa ngozi(Albino) na kupelekea upatikanaji wa uhakika wa mafuta hayo katika maeneo mbalimbali.
Waziri Kikwete ameeleza hayo jijini hapa leo Mei 9,2025 wakati akifungua Kongamano la Mafunzo ya Sheria ya Ununuzi wa Umma na Matumizi ya Mfumo wa NeST kwa watu wenye mahitaji Maalum.
Pia amesema kuwa Serikali kupitia Wizara hiyo imeendelea kuimarisha huduma za watu wenye ulemavu kwa kujenga Vituo vya Afya zaidi ya elfu 12,300 ambavyo vimejengwa katika Mazingira ya kukidhi na rafiki kwa watu wenye mahitaji maalumu.

“Pamoja na hayo nataka nitoe salamu kwamba,Serikali imeendelea kutoa ruzuku na Uboreshaji hapa nchini wa mafuta kinga ya Saratani ya ngozi kwa Watanzania wenye ualbino ambayo hii imepelekea upatikanaji wa mafuta hayo katika maeneo mbalimbali hapa nchini”.
Na Kwa upande wake Winfrida Samba ambaye ni Mwakilishi kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) amesema kuwa mpaka sasa wana jumla ya makundi maalum 335 yaliyokamilisha usajili na uhuishaji wa Taarifa zao katika Mfumo wa Ununuzi wa Umma yaani NeST, lakini makundi ya watu wenye ulemavu yameonekana kuwa na muitikio mdogo ukilinganisha na makundi mengine ambapo wao wana vikundi vitano sawa na asilimia 2,hivyo matarajio yao ni kuwa na ongezeko la usajili wa Vikundi vya watu wenye mahitaji maalumu mara baada ya Kongamano hilo.
“Mpaka sasa tuna jumla ya makundi maalum 335 yaliyokamilisha usajili na uhuishaji wa taarifa zao katika mfumo wa Ununuzi wa Umma yaani NeST, miongoni mwao ni makundi ya vijana ambayo ni vikundi 204Â sawa na asilimia 61 ambao wamekamilisha usajili,lakini tuna makundi ya wanawake ambavyo vikundi 108 sawa na asilimia 32,”amesema.

“Na Makundi ya watu wenye ulemavu ni vikundi vitano sawa na asilimia 2, na makundi ya wazee tuna vikundi 18 sawa asilimia 5,hivyo hapo utaona namna ambavyo ushiriki wa watu wenye ulemavu ni mdogo na tunatarajia baada ya kusanyiko hili tunaenda kupata ongezeko la vikundi la watu wenye ulemavu kujiunga ili kuweza kupata fursa mbalimbali “.
Naye Muasisi na Taasisi ya Ikupa Trust Foundation,Stella Ikupa akitoa salamu za Taasisi hiyo amegusia suala la Bima ya afya kwa wote ambapo ameiomba Serikali kuweka utaratibu mzuri na rafiki kwa watu wenye ulemavu ambao hawana uwezo wa kulipia gharama zilizoainishwa.
Sambamba na kuomba upatikanaji wa uhakika wa mafuta kinga ya Saratani ya ngozi kwa watu wenye ualbino nchini.
Kongamano hili ni la siku mbili na limejumuisha Taasisi na Vyama mbalimbali vya watu wenye ulemavu kutoka Tanzania Bara na Visiwani.

More Stories
Madiwani Ilala walia na dampo la Pugu
TLS yaishauri serikali kuanzisha chombo maalumu
Twange aanza kazi rasmi TANESCO