March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

RFB yakagua barabara ya Dodoma hadi Kitinku

Judith Ferdinand,Dodoma

Wajumbe wa Bodi ya Mfuko wa Barabara(RFB), wametembelea na kukagua utekekalezaji wa mradi wa matengenezo ya barabara katika barabara ya Dodoma hadi Kitinku yenye urefu wa Kilomita 66.7.

Ambapo bodi hiyo imeainisha sehemu zingine za barabara hiyo zinazohitaji kufanyiwa matengenezo zaidi.

Ziara hiyo ya kutembelea mradi wa matengenezo ya barabara ya Dodoma hadi Kitinku, unaotekelezwa kwa fedha za Serikali kupitia Mfuko wa Barabara, imeongozwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Mfuko wa Barabara Mhandisi Mussa Bally Natty.

Wajumbe wa Bodi ya Mfuko wa Barabara(RFB)wakiongozwa na Mwenyekiti wa Bodi hiyo Mhandisi Mussa Natty (wa kwanza kulia), wakiangalia sehemu ya mtaro wenye urefu wa mita 450, uliojengwa katika barabara ya Dodoma hadi Kitinku yenye urefu wa Km 66.7,eneo la Kizota, wakati Bodi hiyo ikikagua kazi za matengenezo ya barabara zilizotekelezwa kwa fedha za Serikali kupitia Mfuko wa Barabara

Awali wajumbe hao, walikagua matengenezo mbalimbali ya miundombinu ya barabara ikiwemo ujenzi wa mtaro wenye urefu wa mita 450 pembezoni mwa barabara ya Dodoma hadi Kitinku, eneo la Kizota.

Mtaro huo umejengwa ili kuzuia uharibifu wa tabaka la barabara pamoja na kupunguza athari zitokanazo na mafuriko ya mvua kwa wakazi waishio maeneo ya jirani. 

Aidha wajumbe hao pia, wamekagua matengenezo ya uwekaji wa tabaka jipya la barabara kwa kutumia zege katika eneo la Nala Mizani, kwenye barabara hiyo ya Dodoma hadi Kitinku, ambapo matengenezo hayo yanalenga kuimarisha na kupunguza athari za uharibifu wa barabara unaotokana na uzito wa magari makubwa yanayotumia Mizani ya Nala.  

Vile vile Bodi hiyo imejionea ukarabati wa tabaka la jipya la barabara kwa kutumia lami (mita 150), kwa sehemu zilizokuwa zimeharibika na kusababisha usumbufu kwa watumiaji wa barabara ya Dodoma hadi Kitinku katika eneo la Bahi.

Mwenyekiti wa Bodi ya Mfuko wa Barabara Mhandisi Mussa Natty(kulia) akimuelekeza jambo Kaimu Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Barabara, Mhandisi Rashid Kalimbaga, wakati Bodi hiyo ikikagua utekekalezaji wa mradi matengenezo ya barabara katika Barabara ya Dodoma hadi Kitinku yenye urefu wa Km 66.7,unaotekelezwa kwa fedha za Serikali kupitia Mfuko wa Barabara.

Kwa upande wake Kaimu Meneja wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS), Mkoa wa Dodoma Mhandisi Christina Nyamziga, amesema kuwa, utekelezaji wa mradi wa matengenezo ya barabara ya Dodoma hadi Kitinku yenye urefu wa Km 66.7), umegharimu kiasi cha milioni 911.

Mhandisi Nyamziga,amesema mpaka sasa utekekalezaji wa mradi huo umefikia hatua za mwisho na tayari upo katika hatua za maangalizi.

Hata hivyo Bodi ya Mfuko wa Barabara inaendelea na zoezi la ukaguzi wa kazi za matengenezo ya barabara katika Mikoa ya Singida, Manyara na Arusha, ili kujionea utekelezaji wa miradi hiyo inayofanywa kwa fedha za Serikali kupitia mfuko huo.

Muonekano wa barabara baada ya matengenezo yaliyohusisha uwekaji wa tabaka jipya la barabara kwa kutumia lami eneo la Bahi, barabara ya Dodoma hadi Kitinku yenye urefu wa Km 66.7,uliofanywa kwa fedha za Serikali kupitia Mfuko wa Barabara.
Muonekano baada ya matengenezo ya barabara yaliyohusisha uwekaji wa tabaka jipya la barabara kwa kutumia zege katika eneo la Nala Mizani,barabara ya Dodoma hadi Kitinku yenye urefu wa Km 66.