March 18, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

RFB yajivunia mafanikio kipindi cha miaka minne

Judith Ferdinand, Timesmajira Online,Dodoma

Inakadiriwa nchini hapa zaidi ya asilimia 90 na 80, ya abiria na mizigo mtawalia hutumia njia ya barabara kwa ajili ya usafiri na usafishaji,hivyo kutokana na umuhimu huo katika kipindi cha miaka minne Serikali imekuwa ikitenga wastani wa bilioni 900 kila mwaka,kwa ajili ya kugharamia matengenezo ya barabara.

Huku Mtandao wa barabara hapa nchini ukiwa na jumla ya kilometa 181,602.2,kati ya hizo kilometa 37,225.7 ni barabara za Kitaifa zinasimamiwa na Wakala wa Barabara Tanzania(TANROADS) huku kilometa 144,376.5 barabara za Wilaya zinasimamiwa na Wakala wa Barabara za Mijini na Vijiji(TARURA).

Hivyo ufanisi wa mipango ya Serikali inayolenga maendeleo ya vijijini, uzalishaji wa ajira, maendeleo ya viwanda, kwa kiasi kikubwa, unachangiwa na ubora wa huduma za usafiri wa barabara.Miundombinu ya barabara ndiyo rasilimali ya umma yenye thamani kubwa zaidi ambayo inakadiriwa kufikia tirioni 39.5 sawa na asilimia 23 ya Pato la Taifa.

Hayo yamebainishwa na Kaimu Mtendaji Mkuu, Mfuko wa Barabara(RFB),Mhandisi Rashid Kalimbaga, wakati akitoa taarifa ya bodi hiyo kwa vyombo vya habari,katika kuadhimisha miaka minne ya uongozi wa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan.

Mhandisi Kalimbaga,amesema, Serikali kwa kutambua thamani na umuhimu wa barabara kwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi,imekuwa ikiimarisha uwezo wa kifedha na kitaasisi ili kuzilinda barabara kwa lengo la kuziwezesha kutumika kwa muda uliopangwa.

“Kwa kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Rais Dkt. Samia,amekuwa akitenga wastani wa bilioni 900 kila mwaka,ambapo fedha hizi zimewezesha utekelezaji wa wastani wa miradi 700 ya matengenezo ya barabara za Kitaifa na miradi 900 kwa barabara za Wilaya kila mwaka, pamoja na kuimarisha uwezo wa TANROADS, TARURA na Bodi ya Mfuko wa Barabara, kwa kuziongezea vitendea kazi pamoja na wataalam,”amesema Mhandisi Kalimbaga.

Amesema,hatua ya Serikali za kuimarisha uwezo wa kifedha na kitaasisi zimewezesha matengenezo ya barabara kufanyika mara kwa mara hivyo zaidi ya asilimia 90 za mtandao wa barabara za kitaifa na asilimia 60 za mtandao wa barabara za Wilaya, mtawalia zipo kwenye hali nzuri na wastani.

Pia amesema sehemu kubwa ya mtandao wa barabara unapitika kipindi chote cha mwaka na hali hiyo imeiwezesha Tanzania kuwa moja ya nchi za Afrika zenye mtandao bora wa barabara ambao sehemu kubwa inapitika majira yote.

Pia amesema,pindi mawasiliano ya barabara yanapokuwa yamekatika kutokana na mafuriko, Serikali imekuwa ikitoa fedha mara moja, ili kuyarudisha kwa wakati na kuwawezesha wananchi kuendelea na shughuli zao za kijamii na kiuchumi.Huku akitolea mfano kazi za dharura zilizofanyika maeneo ya Hanang (Manyara) na kurejesha mawasilano kati ya Dar-es-Salaam na Mtwara Aprili 2024.

“Kwa kuboresha miundombinu ya barabara, wananchi wamewezeshwa kuzifikia huduma za kijamii na kiuchumi, zinazotolewa na Serikali kama vile elimu, afya, masoko, ajira na fursa nyingine za kujipatia kipato.Bodi ya Mfuko wa Barabara itaendelea kufanya kazi kwa juhudi na umahiri ili kutoa mchango unaotarajiwa ili kufikia malengo ya Serikali,”.

Sanjari na hayo amebainisha kuwa moja ya mafanikio ya kuanzishwa kwa Mfuko wa Barabara na Bodi yake, ni kuimarika kwa ubora wa mtandao wa barabara nchini.

Ambapo barabara za Kitaifa zilizo kwenye hali nzuri zimeongezeka na kufikia wastani wa asilimia 90 kutoka wastani wa asilimia 13 mwaka 2000. Aidha, barabara za Wilaya zilizo kwenye hali nzuri na wastani zimeongezeka na kufika asilimia 60 toka asilimia 10 mwaka 2000.