Na Judith Ferdinand,TimesMajira Online-Mwanza
Diwani wa Kata ya Pasiansi, Regina Lubala, amewataka wataalamu na watendaji wa kata hiyo kutafsiri na kutoa elimu ya sheria ndogo ndogo za halmashauri kwa wananchi, ili waweze kuzielewa na kupunguza malalamiko yanayotokana na utozwaji wa faini.
Regina ametoa wito huo Desemba 11, 2025, wakati wa kikao chake cha kwanza na makundi mbalimbali kilicholenga kutoa mwelekeo wa miaka mitano ya uongozi wake 2025-2030, kilichofanyika katika ofisi ya Kata ya Pasiansi wilayani Ilemela mkoani Mwanza.
Regina amesema mara nyingi wananchi hufanya makosa bila wao wenyewe kujua, kutokana na kukosa elimu ya sheria ndogo ndogo zilizopo.Hali hiyo husababisha wananchi kupinga faini au tozo wanazotozwa kwa kudhani wanadhulumiwa.
Ametoa mfano wa mwananchi mwenye duka anayeweza kuambiwa alipe kodi ya shilingi 20,000 au 50,000, lakini akapinga kwa hoja kuwa duka lake ni dogo. Kwa mujibu wake, upinzani huo hutokana na kutokuelewa sheria na taratibu zilizopo, kwani hazijawahi kufafanuliwa kwa wananchi.
Aidha amesema changamoto hiyo inaonekana pia katika masuala ya utunzaji wa mazingira, hususani kwa wananchi wanaoishi karibu na barabara au mitaro ya maji.
Ambapo ameeleza kuwa kisheria mwananchi anatakiwa kusafisha na kutunza mazingira yaliyo mbele ya makazi yake, hata kama siyo mali yake binafsi, jambo ambalo wananchi wengi hawalifahamu.
Amesema endapo wananchi wataelimishwa kuhusu sheria zilizopo na sababu za kuchukuliwa hatua dhidi yao, watakuwa tayari kufuata taratibu na hata kukubali kulipa faini kwa uelewa zaidi.
“Hata akitozwa faini, mwananchi atakubali kwa sababu tayari ana uelewa. ndiyo maana natamani katika kipindi cha uongozi wangu watendaji na wataalamu mkatafsiri Sheria hizo ili jamii izifahamu,” amesema Regina.
Aidha, ameeleza dhamira yake ya kuifanya Kata ya Pasiansi kuwa kata ya mfano katika utunzaji wa mazingira na usafi, akibainisha kuwa utunzaji wa mazingira hauna kikomo bali ni mchakato endelevu unaohitaji ushiriki wa kila mmoja.
“Natamani sana Kata yetu ya Pasiansi iwe Kata ya mfano katika kutunza mazingira na usafi,utunzaji mazingira hauna kikomo ni mchakato ni vitu ambavyo vinaendelea.Waswahili wanasema usafi ni tabia na uchafu ni tabia.Naamini mara nyingi mwenye tabia ya usafi kuharibikiwa siyo rahisi lakini mwenye tabia ya uchafu inawezekana akielekezwa akaelewa,”amesema Regina.
Akizungumzia suala la ukusanyaji wa taka,amesema licha ya jitihada zinazofanyika changamoto ni mawakala wa taka kutokuwa na ratiba wazi ya uzoaji taka,hivyo mara nyingi wanaweza kuja mwisho mwa wiki Moja na ikifika mwisho wa mwezi wanapitia kudai malipo.
“Tutakaa na mawakala hawa watupe ratiba kamili na tukubaliane kuwa watakiwa wanazoa taka lini na mara ngapi kwa mwezi,”amesema Regina.
Sanjari na hayo amekemea tabia ya baadhi ya wananchi kukusanya taka kwenye magunia au vyombo, kisha kuzitupa usiku kwenye mitaro ya maji au maeneo yasiyoruhusiwa hali inayochangia mitaro kuziba, maji kushindwa kupita hasa wakati wa mvua na kusababisha miundombinu ikiwemo barabara kuharibika.
Pia amekemea tabia ya baadhi ya wananchi kutupa taka ovyo katika maeneo ya makaburi,akisisitiza kuwa kitendo hicho hakina utu na kinapaswa kukomeshwa mara moja.
“Nakaa karibu na makaburi mbaya zaidi watu wengi wamekuwa wakitupa takataka katika eneo hilo,jamani kwa sababu wale watu hawawezi kujitetea lakini siyo kitu kizuri.Tuwasaidie hawa ndugu zetu wenye tabia hiyo waache mara moja wasitupe takataka ovyo badala yake wazikusanye,”amesema na kuongeza:
“Wananchi wahifadhi taka vizuri, kuzingatia ratiba za ukusanyaji taka kwani kulinda mazingira ni kulinda maisha na miundombinu ya jamii,”.
Kupitia kikao hicho Regina,amesisitiza umuhimu wa mshikamano na ushirikiano miongoni mwa viongozi, watendaji na wananchi, akieleza kuwa hakuna mtu aliye muhimu kuliko mwingine.
Kwa upande wake Mtendaji wa Kata ya Pasiansi Maarufu Mohammed,ameeleza hatua ambazo Kata hiyo inachukua katika utunzaji na usafi wa mazingira ikiwa ni pamoja kuhamasisha taasisi na watu binafsi kwa kupanda miti toka TFS.
Pia amesema,shughuli za usafi zimekuwa zikifanywa kupitia wataalamu wa afya na vikundi vya usafi katika kila mtaa halikadhalika usafi wa kila jumamosi ya wiki na mwisho wa mwezi ambao umekua ukifanyika kwa jamii yote kushiriki kwa kufanya usafi katika maeneo ya biashara, fukwe na kwenye kaya.
Naye Ofisa Afya wa Kata ya Pasiansi Leticia Mkome,amemuomba Diwani huyo kulisemea jambo la miundombinu ya maji taka kwa wakazi wa kata hiyo ili waweze kuunganisha na mfumo huo.

More Stories
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako
TTCL yaadhimisha siku ya Wanawake kwa kutoa msaada JKCI
Wananchi Dodoma washauri TBA kujenga nyumba za kupangisha watu binafsi