May 11, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

REA kuwawezesha Watanzania mikopo yenye riba nafuu

Na Penina Malundo Dar es Salaam

MKURUGENZI wa Huduma za Ufundi wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Jones Olutu amesema REA itawawezesha watanzania kupata mikopo yenye riba nafuu ya asilimia tano ili kuweza kujikwamua kiuchumi.

Akizungumza hayo jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Huduma za Ufundi wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Jones Olutu wakati akizungumza na waandishi wa habari katika maonesho ya 47 ya biashara ya Kimataifa maarufu Sabasaba yanayoendelea kwenye viwanja vya Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam

Amesema wanatoa mkopo kiasi cha Sh. Milioni 70 ambacho kinaweza kumsaidia mtu kuanzisha kituo kidogo cha kuuza mafuta na kupata mtaji wa kuweka mafuta na kuendesha maisha.

Olutu amesema watanzania wote wenye uhitaji wa mikopo hiyo wanaweza kufika katika Banda lao lilipo katika viwanja hivyo vya Sabasaba ili kuweza kupatiwa vigezo na masharti yakupata mkopo huo.

“Tunawakaribisha watanzania wenye mahitaji ya kupata mkopo huu kufika katika viwanja vya sabasaba katika maonesho haya ya 47 wataelezwa namna ya kujaza maombi yao ili waweze kupata,” amesema.

Amesema kupitia maonesho hayo wamejipanga kuonesha miradi mbalimbali ambayo wameitekekeza pamoja na mafanikio yaliyopatikana na kuwaeleza watu namna bora ya kutumia nishati ya umeme kwa lengo la kujipatia kipato.

Olutu amesema Jumla ya vijiji 10,125 kati ya 12,318 vilivyopo Tanzania bara tayari vimeshapatiwa huduma ya umeme huku vilivyobakia vyote ifikapo Desemba mwaka huu navyo vitafikiwa na hyduma hiyo.

“Ifikapo mwaka 2030 vitongoji ambavyo vipo 64,760 navyo vitakuwa vimefikiwa na umeme na kwamba mpaka sasa vitongoji 28,000 tayari vimeshapatiwa huduma hiyo ya umeme,”Amesisitiza