December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

REA III Awamu ya Pili yazinduliwa Mtwara

Na Veronica Simba – REA

WAZIRI wa Nishati Dkt. Medard Kalemani amezindua Mradi Kabambe wa Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili katika Mkoa wa Mtwara unaolenga kufikisha umeme katika vijiji vyote vilivyosalia vya Mkoa huo.

Dkt. Kalemani alizindua Mradi huo Juni 19, 2021 katika kijiji cha Namtumbuka, Mtwara Vijijini akiwa ameambatana na Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Dunstan Kyobya aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa, Wabunge, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Wakala wa Nishati Vijijini (REB) Wakili Julius Kalolo, Mjumbe wa Bodi hiyo Oswald Urasa, Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa Wakala, Mhandisi Jones Olotu pamoja na viongozi na wataalam mbalimbali wa Wizara, REA na TANESCO.

Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani (katikati), akikata utepe kuashiria kuzindua rasmi Mradi Kabambe wa Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili katika Mkoa wa Mtwara. Uzinduzi huo ulifanyika katika kijiji cha Namtumbuka, Mtwara Vijijini, Juni 19, 2021.

Akizungumza na wananchi wakati wa hafla hiyo ya uzinduzi, Waziri Kalemani alieleza kuwa lengo la Mradi husika ni kupeleka umeme katika vijiji 384 vya Mkoa wa Mtwara ambavyo havijafikiwa na nishati hiyo.

“Mkoa wa Mtwara una vijiji vyenye umeme 413 kati ya 797. Kwa kutambua hilo, leo ninawakabidhi wakandarasi waushambulie mkoa huu kwa pamoja na kuhakikisha vijiji vyote vilivyosalia vinapatiwa umeme katika mradi huu,” anesema Waziri.

Amesema, mradi umefadhiliwa na Serikali kwa kushirikiana na Benki ya Dunia hivyo akaishukuru Taasisi hiyo na kwa niaba ya Serikali akaahidi kuimarisha uhusiano mzuri baina ya pande hizo mbili.

Waziri Kalemani amewataka wananchi wa Mtwara kuutumia umeme huo katika shughuli za kimaendeleo ili kuboresha maisha yao na hali ya kiuchumi ya nchi kwa ujumla.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Wakala wa Nishati Vijijini (REB), Wakili Julius Kalolo akizungumza na wananchi wakati wa uzinduzi rasmi wa Mradi Kabambe wa Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili katika Mkoa wa Mtwara. Uzinduzi huo ulifanyika katika kijiji cha Namtumbuka, Mtwara Vijijini, Juni 19, 2021.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi, Wakili Kalolo alieleza kuwa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) umeandaa Mpango Kazi wa Miaka Mitano uliojikita katika kufanikisha malengo ya Serikali ya kusambaza nishati ya umeme katika vijiji vyote ifikapo Disemba 2022 na vitongoji vyote mwaka 2025.

Alisema kuwa Mpango Kazi huo ni wa miaka mitano kuanzia 2021/22 hadi 2025/26 na umejikita katika kufikisha umeme kwa Watanzania wote, maeneo ya viwanda, madini, kilimo, uvuvi na ufugaji.

“Mheshimiwa Waziri, Mradi huu unaouzindua leo ni sehemu tu ya Mpango Mkakati wa Wakala na umelenga kusambaza umeme katika vijiji 1956 ambavyo havijafikiwa na miundombinu ya umeme,” alibainisha.

Sehemu ya umati wa wananchi wakishangilia wakati wakimsikiliza Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani (hayupo pichani) alipokuwa akizungumza nao wakati wa uzinduzi rasmi wa Mradi Kabambe wa Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili katika Mkoa wa Mtwara. Uzinduzi huo ulifanyika katika kijiji cha Namtumbuka, Mtwara Vijijini, Juni 19, 2021.

Alieleza zaidi kuwa Mradi utatekelezwa katika mikoa 24 ambayo imegawanywa katika mafungu 39 na kwamba unakadiriwa kugharimu takribani shilingi trilioni 1.3 ambapo unatarajiwa kukamilika Disemba, 2022.

Wakili Kalolo aliongeza kuwa Mradi utakapokamilika utawezesha vijiji vyote 12,268 kupatiwa umeme na kuifanya Tanzania kuwa nchi ya kwanza kwa Ukanda wa Kusini mwa Jangwa la Sahara kufikisha umeme katika vijiji vyote.

Naye Mkurugenzi wa Huduma za Ufundi kutoka REA, Mhandisi Jones Olotu, aliyemwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa Wakala, alieleza kuwa katika Mradi huo mkoani Mtwara, wateja wa awali 6,182 wataunganishwa.

Mkurugenzi wa Huduma za Ufundi kutoka Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Jones Olotu akizungumza na wananchi wakati wa hafla ya uzinduzi rasmi wa Mradi Kabambe wa Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili katika Mkoa wa Mtwara. Uzinduzi huo ulifanyika katika kijiji cha Namtumbuka, Mtwara Vijijini, Juni 19, 2021.

Aliongeza kuwa utekelezaji wa Mradi katika Mkoa huo utagharimu shilingi bilioni 62.146 ambapo utatekelezwa na Mkandarasi Namis Corporate Engineers and Contractors katika Wilaya ya Masasi na Nanyumbu na Mkandarasi Central Electricals Internationals katika Wilaya ya Mtwara Vijijini, Newala na Tandahimba.

Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Dunstan Kyobya, alisema umeme una umuhimu wa pekee katika Mkoa wa Mtwara kwani pamoja na kuwa ni fursa katika shughuli za kimaendeleo lakini pia ni muhimu kwa shughuli za kiusalama ikizingatiwa kuwa mkoa huo uko pembezoni mwa nchi.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, baadhi ya Wabunge wa Mtwara, Geofrey Mwambe (Ndanda), Issa Mchungahela (Lulindi), Katani Katani (Tandahimba), Hassan Mtenga (Mtwara Mjini) na Abdallah Chikota (Nanyamba) walipongeza jitihada zinazofanywa na Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu katika kuwapelekea wananchi wake maendeleo kupitia usambazaji umeme vijijini.

Aidha, wawakilishi hao wa wananchi waliipongeza Wizara ya Nishati, REA na TANESCO kwa kazi kubwa ambayo wamekuwa wakiifanya kuhakikisha Mtwara inafikiwa na umeme katika pande zote.

Waliwataka wakandarasi waliopewa dhamana ya kutekeleza Mradi husika kuhakikisha wanafanya kazi hiyo kwa uaminifu na weledi huku wakiwahakikishia kuwa watawasimamia ipasavyo ili wasiiangushe Serikali na wananchi.