November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

RC Tabora awabana wakurugenzi, ataka mapato asilimia 100

Na Allan Vicent, TimesMajira Online, Tabora

MKUU wa Mkoa wa Tabora Balozi Dkt Batilda Burian amewaagiza Wakurugenzi wa halmashauri zote 7 za Mkoa huo kuhakikisha wanaongeza kasi ya ukusanyaji mapato na kila kila mmoja afikie au kuvuka lengo lake kwa asilimia 100 au zaidi.  

Ametoa agizo hilo jana alipokuwa akiongea na madiwani na wataalamu wa halmashauri ya wilaya ya Urambo Mkoani hapa katika kikao maalumu cha mapitio ya hoja za Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

Alisema kama Mkoa walijiwekea lengo la kukusanya kiasi cha sh bil 29 katika mwaka wa fedha 2022/2023 lakini hadi kufikia Juni 9 mwaka huu kiasi kilichokwisha kukusanywa ni sh bil 26.6 sawa na asilimia 87 tu na bado wiki 2.

Alisisitiza kuwa licha ya baadhi ya halmashauri kufanikiwa kufikia lengo la makusanyo, baadhi ya Wakurugenzi kasi yao bado ni ndogo sana, hivyo akaagiza kila mmoja kuhakikisha anafikia asilimia 100 ya mapato kabla ya Juni 30, 2023.

‘Wakurugenzi ongezeni kasi kukusanya mapato, nataka kila mmoja afikie asilimia 100 au au zaidi, tumieni vizuri muda uliobakia ili ifikapo mwishoni mwa mwezi huu kila halmashauri iwe imetimiza makisio yake’, alisema.

RC Batilda alibainisha kuwa halmashauri ya wilaya hiyo hadi sasa imekusanya kiasi cha sh bil 2.5 sawa na asilimia 95 ya lengo la kukusanya sh bil 2.7, hivyo akaelekeza Mkurugenzi na madiwani kusimamia zoezi hilo ili kufikisha lengo.

Alipongeza halmashauri ya wilaya ya Uyui kwa kufanikiwa kuvuka lengo la mapato yao kabla ya Juni 9 kwani hadi sasa wamekusanya kiasi cha sh bil 3.5 sawa na asilimia 107 ya lengo la kukusanya bil 3.3.

Alitaja halmashauri nyingine zilizofanikisha makusanyo yao kwa asilimia 100 kuwa ni manispaa Tabora waliokusanya sh bil 5.5, Kaliua sh bil 4.4 na halmashauri nyingine zimeendelea kupiga hatua zaidi.

Halmashauri ya Nzega Mji tayari imekusanya bil 2.6 sawa na asilimia 84 ya lengo lao la kukusanya bil 3.1, Igunga wamekusanya sh bil 2.8 sawa na asilimia 73 ya lengo la sh bil 3.8 na Nzega DC sh bil 1.8 sawa na asilimia 64 ya lengo la bil 2.8.

Aidha aliwataka kuhakikisha fedha zote zinazokusanywa zinapelekwa benki na kila mashine ya kukusanyia mapato (POSS) ifuatiliwe ili kujua nani amekusanya kiasi gani na fedha ziko wapi huku akiagiza kuchukuliwa hatua wote watakaotumia vibaya mapato hayo.

Katika kikao hicho RC aliwapongeza Wakurugenzi wa halmashauri zote 7 kwa kuandaa taarifa zao vizuri na kupitiwa na Wakaguzi wao wa ndani hali iliyowawezesha kupata hati safi, ila akaagiza kufanyia kazi hoja zote zilizosalia ili kuhakikisha zinafungwa kabla ya mwaka huu wa fedha kumalizika.

Picha ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora Balozi Dkt Batilda Burian akiongea na wataalamu na madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Urambo Mkoani Tabora jana…ambapo alitangaza kuunda kamati ya kuchunguza tukio la mtumishi wa hospitali ya wilaya ya Sikonge kubaka mgonjwa wodini. Pucha na Allan Vicent.
Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Urambo Mkoani Tabora Adam Malunkwi akizungumza jana katika kikao maalumu cha baraza la madiwani wa halmshauri hiyo jana. Picha na Allan Vicent