December 27, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

RC Songwe apokea malalamiko ya madiwani dhidi ya DED Mbozi

Na Esther Macha,Timesmajira,Online,Mbozi

MKUU wa Mkoa wa Songwe,Bregedia Nicodemas Mwangela amesema malalamiko yaliyotolewa na madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi dhidi ya Mkurugenzi wa halmashauri hiyo ameyapokea kwa sababu yeye sio mwenye maamuzi ya mwisho atafikisha kwenye ngazi za juu ili kupata ufumbuzi wa masuala hayo.

Breg.Mwangela amesema hayo jana wakati akifunga kikao maalum cha Baraza la Madiwani alichokihitisha kwa lengo la kusikiliza malalamiko na majibu ya mkurugenzi kutokana na tuhuma zilizoelekezwa dhidi yake kwa madiwani wa halmashauri hiyo.

Aidha amewaomba madiwani kuendelea kumpatia ushirikiano mkurugenzi huyo, wakisubiri maamuzi ya Serikali Kuu kwa kuhakikisha wanasimamia na kukamilisha miradi mbalimbali ya maendeleo.

“Nimesikiliza kwa makini hoja na mapendekezo yenu madiwani kwa sehemu yangu nimefanya kwani nimeitisha kikao hiki kwa vile mnataka Mkurugenzi aondoke mie sina maamuzi hayo Serikali kuu au viongozi wangu wa kitaifa watajua namna wakavyolishughulikia suala hilo, ombi langu ni kuendelea kuchapa kazi, mpeni ushirikiano Mkurugenzi ili kusimamia na kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo inayoendelea kwa manufaa ya wanambozi naomba amani na utulivu uendelee kama kawaida,” amesema Mwangela.

Mkuu wa mkoa Songwe Bregedia Nicodemas Mwangela akizungumza na madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Mbozi

Hata hivyo katika kikao hicho,Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi, Hanji Godigodi aliwaomba radhi madiwani kwa mambo mbalimbali aliyotuhumiwa kuyafanya na kuahidi kutorudia tena na ataendelea kuchapa kazi kwa kushirikiana na watumishi wa Halmashauri hiyo pamoja na kusimamia miradi ambayo haijakamilika.

Amesema Baraza la Madiwani lilimtaka kujibu hoja tisa ambazo zilihusu usimamizi wa miradi na alifanikiwa kuzitolea ufafanuzi licha ya kukiri pia kuwa taarifa ya hoja hizo haikukamilika.

“Nawaomba radhi madiwani wote wa Halmashauri ya Mbozi kwa mambo yote niliyoyafanya mimi ni binadamu nina mapungufu naahidi kubadilika na kutorudia tena, kikubwa tuendelee kushirikiana,” amesema mkurugenzi huyo.

Aidha Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi, George Msyani amesema wakati wanaendelea kusubiri maamuzi kutoka kwa viongozi wa juu wa kitaifa ni muhimu sasa kuendelea kushirikiana ili kuongeza makusanyo kutoka kwenye vyanzo mbalimbali vya mapato.

Amesema wilaya hiyo ina vyanzo vingi vya mapato lakini tatizo ni kwamba fedha zinazokusanywa ni ndogo hivyo aliangiza usimamizi zaidi kwa kuwaomba maofisa wanaosimamia ukusanyaji kuwa wazalendo.

Awali madiwani hao wakati wakichangia hoja,walidai kuwa mkurugenzi aliwahi kuandika bango la kupiga marufuku madiwani kuingia kwenye ofisi yake.

Kauli hiyo ilithibitishwa na Diwani wa Bara, Aloyce Mdalavuma alidai Mkurugenzi amekuwa na manyanyaso kwa watumishi hali iliyosababisha pia kuweka bango katika ofisi yake kuzuia madiwani kutokukanyaga ofisini kwake waraka ambao pia ulimfikia Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri kwa wakati huo.

Aidha Diwani wa Itumpi,Samson Nzunda amesema watumishi wa Halmshauri wanahusika na ubadhirifu wa fedha za miradi hivyo alihitaji Takukuru kuingilia kati na kwamba yuko tayari kutoa ushirikiano atakapohitajika kwani anawafahamu.

Diwani wa Nyimbili, Tinson Nzunda amelieleza baraza hilo kuwa miongoni mwa masuala yanayomkabili Mkurugenzi huyo ni matumizi mabaya ya fedha zinazotokana na makusanyo ya Kahawa kiasi cha fedha milioni 187.

Amesema baada ya kubaini usimamizi mbovu wa makusanyo ya kahawa walimshauri Mkurugenzi kuunda kikosi kazi cha kufuatilia lakini aligoma kutoa ushirikiano ndipo waliamua madiwani kujitolea kwa gharama zao kufuatilia na kubaini kiasi cha shilingi milioni 187 ambacho kingeweza kupotea.