June 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

RC SENDIGA : Maafisa Tarafa na Kata hakikisheni mnasimamia upandaji miti

Na. Israel Mwaisaka,Rukwa

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Queen Sendiga ametoa agizo kwa Maafisa Tarafa na Kata kusimamia na kuhamasisha kampeni ya upandaji miti kwenye maeneo yao ili kutunza mazingira.

Mkuu huyo wa Mkoa ametoa kauli hiyo wakati akizindua kampeni ya mkoa kupanda miti kwenye barabara na makazi ya watu katika maeneo ya Utengule na Nambogo Manispaa ya Sumbawanga leo .

Katika kuhakikisha kampeni ya urejeshaji uoto wa asili mkoani Rukwa inafanikwa Sendiga amezitaka halmashauri za Nkasi, Manispaa ya Sumbawanga, Kalambo na Sumbawanga kuboresha sheria ndogo ili ziweze kuchua hatua kwa waharibifu wa vyanzo vya maji.

“Maafisa watendaji wa kata zote jukumu lenu ni kwenda kusimamia zoezi la upandaji miti kwenye maeneo yenu. Maafisa Tarafa nendeni pia mkasimamie zoezi hili la upandaji miti Rukwa” amesisitiza Sendiga.

Sendiga amesema mkoa huo una changamoto ya utapiamlo ,hivyo sasa ni wakati wa wananchi kupanda miti ikiwemo ya matunda ili kuimarisha lishe ya familia.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Queen Sendiga akizungumza na wananchi wa Utengule Manispaa ya Sumbawanga leo alipozindua kampeni ya upandaji miti ambapo ametaka kando ya barabara kuanzia Sumbawanga hadi Tunduma zipandwe miti na kutunzwa.

Katika hatua nyingine Sendiga ametoa siku saba kwa Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga Dkt. Jane Nyamsenda kuhakikisha mitaa ya Manispaa ya Sumbawanga inakuwa safi pamoja na kupandwa miti na maua.

Kwa upande Mwenyekiti wa CCM Mkoa Rukwa, Silafu Maufi ameshiriki zoezi hilo amesema zoezi hilo la upandaji miti lililofanywa na viongozi wa Rukwa ni utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM na kuwa linapaswa kuwa endelevu.