Na George Mwigulu, Timesmajira Online,Katavi
Wafanyabiashara wa Mkoa wa Katavi wametahadharishwa kuepuka kuuza bidhaa ya sukari kinyume na bei elekezi ya serikali kwani kufanya hivyo ni kosa na hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.
Ambapo Januari 23, 2024, serikali imetoa bei elekezi ya kuuza biadhaa ya sukari nchini kufuatia kuwepo kwa mfumuko wa bidhaa hiyo ambapo kwa Kanda ya Magharibi inayojumuisha Mikoa ya Katavi,Kigoma,Rukwa na Kagera bei ya rejareja ya sukari kwa kilo moja ni Tsh 2,800/= hadi Tsh 3,200/= huku bei ya jumla ni kati ya Tsh 2,600/= hadi 2,900/=.
Mkuu wa Mkoa wa Katavi,Mwanamvua Mrindoko ametoa agizo hilo Januari 27,2024 kwa wafanyabiashara wakati wa tamasha maalumu (Family Day) lililoandaliwa na Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na Klabu ya Waandishi wa Habari (KTPC) lililo fanyika katika uwanja vya Polisi Mpanda ambalo ni sehemu ya kuimarisha uhusiano wa kikazi na familia za kada zote mbili.
Amesema upatikanaji wa sukari nchini umekuwa mdogo kutokana na sababu ambazo Waziri wa Kilimo ameshazitoa na wote wanafahamu.
Hivyo wafanyabiashara wanapaswa kuhakikisha sukari iliyopo kwenye maghala na maduka inauzwa bila masharti bali iuzwe kwa bei ambayo Mkoa imepewa isiyozidi Tsh 3,200/=
Mrindoko amesisitiza wafanyabiashara wote wa Mkoa wa Katavi kuuza sukari kwa bei elekezi huku akilitaka Jeshi la Polisi kufanya ufuatiliaji kwa yeyote atakaye jaribu kuuza kwa bei kubwa akamatwe na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.
“ Wananchi mtusaidie kama utafika mahali ukaambiwa sukari ni Tsh 3,500/=, Tsh 4,000/= na kadhalika toa taarifa kwa haraka kwa uongozi uliopo karibu na wewe ili tuweze kupata hizo taarifa na kuzifanyia kazi kwa haraka,” amesitiza Mrindoko.
Katika hatua nyingine Mkuu wa Mkoa huyo amesema serikali inaendelea kufanya maboresho kwa jeshi la Polisi.
Hivyo ametaka magari matatu waliyopatiwa ya thamani ya milioni 390 Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Katavi,ACP Kaster Ngonyani na wasaidizi wake kuyasimamia.
“ Huu ni mwanzo wa kuelendelea kuimarisha usimamizi wa usalama wa raia na mali zao…hakikisheni magari haya yanatumiwa kwa malengo yaliyokusudiwa ya kuimarisha usalama,ulizi pamoja na amani ndani ya Mkoa wetu wa Katavi na sivinginevyo,”amesema Mkuu wa Mkoa huyo.
Aidha mesisitiza utunzaji wa magari hayo yaweze kutumika kwa muda mrefu zaidi na yasipate hitilafu zisizo za lazima wala ajali zinazosababishwa na uzembe.
Mariam Rashidi,Mkazi wa Mtaa wa Kawajense Manispaa ya Mpanda amefurahishwa na agizo la Mkuu wa Mkoa wa Katavi kwa kuweza kutoa tamko ambalo litawasukuma wafanyabiashara kuacha tabia ya kupandisha bei ya sukari kiholela.
“ Kudhibitiwa kwa mfumuko wa sukari utatoa ahueni kwetu sisi wananchi wa chini na hata sasa licha ya bei elekezi ya sukari bado mfumuko huo unahitajika kudhibitiwa” Amesema Mariam.
Anthony Shilla,Mfanyabiashara wa Manispaa ya Mpanda amesema changamoto zinazosababisha mfumuko wa bei zinapaswa kushughulikiwa kwa haraka ili kutuliza hali ya wasiwasi ya kupanda gharama za maisha kwa wananchi.
Amesema kushughurikiwa kwa changamoto hizo ni utakuwa mwanzo mwema wa kumkomboa mwananchi hususani wa chini ambaye wakati mwingine upatikaji wa milo mitatu kwa siku ni mgumu kwake.
More Stories
Wenje:Tuwanadi wagombea bila kuchafuana
Mtoto darasa la tatu adaiwa kujinyonga kwa kukosa nguo ya sikukuu
Jeshi la Polisi Katavi laanika mafanikio 2024