November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mkuu wa Mkoa wa mbeya akiwa na madereva bodaboda katika halmashauri ya wilaya ya mbeya baada ya kukabidhi mkopo wa sh. Mil.243 kwa vikundi vya vijana, wanawake na walemavu. Picha na Esther Macha

RC Mbeya ashauri wanaorejesha mikopo kwa wakati wakopeshwe magari ya abiria, matrekta

Na Esther Macha, Timesmajira Online, Mbeya

MKUU wa Mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila ameutaka uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya kuanza utaratibu wa kuwakopesha wakulima na vikundi vya wajasiriamali magari ya kusafirisha abiria, matrekta na pawatila ili waweze kuongeza uzalishaji na kipato kitakachowawezesha kupata faida na kurudisha mkopo kwa haraka.

Chalamila ametoa wito huo wakati akikabidhi mkopo wa fedha kiasi cha sh. milioni 243 kwa ajili ya vikundi vya vijana wenye ulemavu na wanawake.

Amesema kuwa, sasa ni wakati kwa halmashauri ya wilaya hiyo, kuacha kukopesha vitu vidogo kwa wajasiriamali badala yake wakopeshe fedha au vifaa ambavyo vitasaidia kujiongezea kipato.

“Inabidi tupige hatua sasa kutoka hapa tulipo hadi kukopesha vitu vya maana ambavyo vitabadili maisha yetu, vikundi vya bodaboda vikupeshwe angalau Coaster na wakulima wapewe mapawatila na matrekta ili kuongeza ufanisi na uzalishaji wa mazao yao, lakini naipongeza halmashauri ya wilaya kwa kuwa miongoni mwa wilaya zinazotoa mikopo mingi kwenye vikundi cha muhimu sasa ni kuongeza thamani ya mikopo hiyo,” amesema Chalamila.

Aidha, amewakumbusha vijana kuwa na nidhamu ya matumizi ya fedha walizokopeshwa kwa kuhakikisha wanatumia kwa malengo yaliyokusudiwa badala ya kuhonga na kuongeza nyumba ndogo na hatimaye kushindwa kurudisha mikopo.

Awali akifafanua mchanganuo wa fedha hizo sh.milioni 243 kwa ajili ya mikopo, Ofisa Maendeleo ya Jamii, Zena Kapama amesema, kwa kipindi cha miezi mitatu kuanzia Machi hadi Juni jumla ya vikundi 26 viliomba mikopo na kati ya hivyo 16 vilikidhi vigezo ambavyo ni wanawake saba, vijana nane na wenye ulemavu kimoja.

Amesema, kati ya vikundi hivyo 16 vilivyopata fursa ya mkopo huo vina jumla ya wanakikundi 195 kati yao wanawake 70 na vijana 120 na wenye ulemavu watano huku akidai tayari vilipewa elimu juu ya matumizi sahihi ya mkopo huo ili kupata faida.

“Vikundi hivi 16 ambavyo vimenufaika na mkopo vinajishughulisha na miradi mbalimbali kama vile bodaboda, uzalishaji wa miche ya parachichi, uchanaji na uuzaji wa mbao, uuzaji wa pembejeo za kilimo cha bustani ya kitalu nyumba, ufugaji wa kuku na biashara ya mazao,” amesema Kapama.