November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila

Rc Mbeya ataka utaratibu kuzuia magari katika miteremko

Na Esther Macha, TimesMajira Online, Mbeya

MKUU wa Mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila  amelisisitiza Jeshi la Polisi mkoani humo kuendelea na utaratibu wa kuzuia magari ya abiria na mizigo kupishana kwenye maeneo yenye miteremko mikali ili kuepusha ajali za barabarani.

Chalamila amesema kupitia mitandao alipokuwa anatoa salamu za pole kwa wananchi wa Mkoa wa Iringa kufuatia ajali ya basi iliyotokea katika mteremko wa Mlima Kitonga ambayo iligharimu maisha ya watu kadhaa na wengine kujeruhiwa.

Amesema katika Mkoa wa Mbeya baada ya ajali za barabarani kukithiri hasa kwenye maeneo ya milima, Kamati ya Ulinzi na Usalama ilichukua hatua kadhaa ikiwemo kuyasimamisha magari ya mizigo kabla hayajaanza kuteremka kwenye milima ili kuyakagua mifumo yake ya breki.

Amesema magari ya abiria na ya mizigo yanapita kwa awamu katika maeneo yote ya miteremko kwa maelezo kuwa utaratibu huo unasaidia kupunguza madhara kwa binadamu endapo ajali itatokea.

“Nampa pole sana Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Ally Hapi, Jeshi la Polisi mkoani humo pamoja na wananchi wote wa Mkoa wa Iringa kwa kuwapoteza wapendwa wetu katika ajali hiyo na ninawaombea majeruhi wapone na waendelee kufanya shughuli za maendeleo,” amesema Chalamila.

Aidha amesema alisikitika baada ya kuona wengi wa waliopoteza maisha kwenye ajali hiyo walikuwa ni watoto wadogo ambao walikuwa wanasafiri na wazazi wao.

Amewataka wazazi waliowapoteza watoto wao kwenye ajali hiyo kuwa wavumilivu katika kipindi hiki kigumu.

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Chalamila ni mzaliwa wa Mkoa wa Iringa na kabla ya kuteuliwa na Rais kuwa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, alikuwa Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) katika Mkoa huo.