January 4, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

RC Mara aagiza simu zitumike kusajili wananchi huduma CHF

Na Fresha Kinasa, Mara

MKUU wa Mkoa wa Mara, Adam Malima amewaagiza wakurugenzi watendaji wa halmashauri za mkoa huo kununua simu za kisasa (Smart Phone)ambazo zitatumika kusajilia wanachama wapya wa Huduma ya Afya ya Jamii (CHF) iliyobooreshwa katika maeneno yao ili kufikia malengo ya Kitaifa ya kusajili asilimia 30 ya wananchi ifikapo Juni 30, 2021.

Amesema Serikali imedhamiria kuhakikisha wananachi wote wanapatiwa huduma bora za matibabu kupitia CHF iliyobooreshwa, na hivyo kukosekana kwa simu za kusajilia wanachama ni uzembe.

Mkuu huyo wa mkoa ametoa maelekezo hayo leo katika kikao cha lishe ngazi ya mkoa kilichofanyika mjini Musoma kufuatia taarifa ya Mratibu wa CHF iliyobooresha Mkoa wa Mara, Elizabeth Mahinya kuwa hadi sasa kaya zilizojiunga na CHF ni kaya 3,549.

Amesema idadi hiyo ni sawa na asilimia moja tu, huku malengo ya kitaifa yakiwa ni kufikia asilimia 30. Mkoa wa Mara unashika nafasi ya mwisho kwa tathmini ya mwaka jana kwa kuandikisha idadi ndogo ya wanachama tangu ulipoanza zoezi la uandikishaji oktoba 29 mwaka jana.

“Zoezi la kuandikisha wanachama wapya wa CHF iliyobooreshwa linahitaji simu za Smart Phones,maofisa uandikishaji 501 walipewa elimu ya kuandikisha lakini wanaofanya kazi hiyo ni 180 tu, na mwongozo unataka kila kijiji kiwe na ofisa uandikishaji tatizo kubwa ni kukosa simu za kisasa ambazo zitatumika katika zoezi hilo na baadhi ya halmashauri ambazo zimefanya vizuri katika hili, zimekuwa zikitumia simu zao binafsi kufanya jukumu hili, kukosekana kwa simu ni sababu mojawapo ya kusuasua zoezi hili,” amesema Mahinya.

Ameongeza Kuwa ili zoezi hilo lifanikiwe kunahitajika simu ambapo kila ofisa uandikishaji aweze kufanya kazi hiyo. Amesema ni muhimu kwa kila kiongozi kuanzia ngazi ya kijiji kuhamasisha wananchi kuchangamkia fursa hiyo ambayo itawapa uhakika wa matibabu hata Kama mgonjwa akiugua akiwa hana fedha atatibiwa kuanzia zahanati, kituo cha afya, hospitali ya wilaya hadi Hospitali ya Rufaa kwa sh. 30,000.

Mara baada ya maelekezo hayo, Malima amesema wakurugenzi walioshindwa kununua simu kwa ajili ya uandikishaji wanapaswa kujitathimini iwapao wanawatendea haki wananchi.

Amesema suala la afya za wananchi halipaswi kufanyiwa mchezo wala uzembe, bali linahitaji ufanisi na kutiliwa mkazo wa dhati. Ameagiza baada ya kikao hicho aelezwe hatua gani zimechukuliwa.

Katika hatua nyingine, Malima amemtaka Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mara Dokt. Frolian Tinuga na Waganga Wakuu wa Wilaya ya Mkoa wa Mara kuweka utaratibu wa ushirikishanaji katika kutoa Matibabu ya kibingwa mkoani humo.

Ametolea mfano Hospitali ya Wilaya ya Tarime kuwa ina daktari bingwa wa magonjwa ya ndani na kwamba mgonjwa wa tatizo hilo akibainika yuko Musoma apelekwe kutibiwa Tarime jambo ambalo litapungiza usumbifu kwa wananchi kufuata huduma hizo nje ya Mkoa wa Mara.

Naye Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mara, Dkt. Florian Tinuga amesema kuwa Mkoa huo kwa sasa umeonesha mafanikio mazuri katika kukabiliana na tatizo la udumavu. Ametaja baadhi ya mambo yaliyochangia kuwa ni pamoja na wakuu wa wilaya kujua vigezo vya jambo hilo na kuimarisha ukusanyaji na utunzaji wa taarifa za lishe ambapo kila halmashauri huwasilisha kila wiki taarifa husika.

Mkazi wa Kata ya Kitaji Manispaa ya Musoma, Neema Paul, akizungumza na Majira kuhusiana na Serikali kuanzisha utaratibu wa CHF iliyobooreshwa, amesema ni hatua nzuri kwani inawapa uhakika wa matibabu wakati wote wananchi hata kama wakiugua hawana fedha watahudumiwa.