March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

RC.Makame awahakikishia wananchi  amani na utulivu Oktoba 29,2025

Na Moses Ng’wat, Timesmajira Online-Tunduma

Wananchi mkoani Songwe wamehimizwa kujitokeze kwa wingi kutumia haki yao ya kikatiba kupiga kura na kuwachagua viongozi wanaowataka huku wakihakishiwa amani na utulivu siku ya uchaguzi mkuu unaotarajia kufanyika Oktoba 29 mwaka huu.

Hayo yamezungumzwa Oktoba 20,2025, na Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Jabiri Omary Makame,wakati akizungumza na wafanyabiashara, madereva wa bajaji, bodaboda pamoja na wananchi wa Mkoa wa Songwe,kupitia vyombo vya habari vilivyokuwa vikirusha moja kwa moja mkutano wake uliofanyika eneo la Kisimani ambalo ni kitovu cha biashara c Mji wa Tunduma wilayani Momba.  

Amesema jeshi la polisi kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama,vimejipanga kuhakikisha hali ya amani inatawala wakati  na baada ya uchaguzi.

“Wananchi wenzangu hakuna haja ya kuwa na hofu, tujitokeze kwa wingi kupiga kura kwa amani na kutumia haki yetu ya msingi kuchagua viongozi wanaofaa kutuongoza kwa miaka mitano ijayo,” amesema Makame.  

Pia  amewaonya  baadhi ya watu wanaopanga au kushawishi vurugu wakati wa uchaguzi, akisisitiza kuwa vyombo vya ulinzi na usalama vipo macho na vitachukua hatua  kwa yeyote atakayevunja sheria.  

Sanjari na hayo amesema, maendeleo ya Mkoa wa Songwe yanategemea uongozi bora, hasa katika sekta za kilimo, biashara ndogondogo na huduma za kijamii.Pia makundi kama machinga na waendesha bodaboda ustawi wa kazi zao hutarajia uamuzi wa viongozi wanaochaguliwa katika ngazi mbalimbali za utawala.  

” Vijana wenzangu na wananchi kwa ujumla, tuilinde amani yetu, jukumu la kulinda amani si la vyombo vya dola pekee, bali ni letu sote,tukiona dalili za uvunjifu wa amani, tuchukue hatua kwa kutoa taarifa mapema,” amesisitiza Makame.

Akizungumzia maandalizi ya uchaguzi mkuu wa 2025, Makame amesema Mkoa wa Songwe umeendelea kushiriki kikamilifu katika hatua zote zinazosimamiwa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi  (INEC), huku wananchi wakiendelea kuonesha muamko na ushirikiano katika maandalizi hayo.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Umoja wa Madereva Bodaboda wa Mji wa Tunduma, Paulo Mjwang maarufu kwa jina la Magufuli, amewataka vijana wenzake kutokubali kurubuniwa na watu wanaotaka kuvuruga uchaguzi, badala yake washiriki ipasavyo katika kupiga kura kwa amani na utulivu.