December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

RC.Makalla:Toeni taarifa kwa waandishi wa habari

Daud Magesa na Judith Ferdinand, Timesmajira Online, Mwanza

MKUU wa Mkoa wa Mwanza,Amos Makalla,amewaagiza viongozi wa serikali na wakuu wa taasisi zake wakiwemo wakurugenzi wa halmashauri za Jiji, Manispaa na Wilaya,wasikalie taarifa wanazozihitaji waandishi wa habari,wazitoe kwa wakati ili kuepuka upotoshaji.

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza,Amos Makalla, akizungumza na waandishi wa habari wa vyombo mbalimbali mkoani humo

Kutokana na umuhimu mkubwa wa vyombo vya habari katika jamii na serikali,amewaahidi ushirikiano,kuhakikisha wanatumia kalamu zao kwa weledi wakizingatia miiko ya taaluma yao,hivyo kuiwezesha nchi kuwa salama na kupata maendeleo ya kijamii,kiuchumi na kisiasa.

Makalla ametoa maelekezo hayo Februari 23,2024 katika mkutano na wanachama wa Chama Cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Mwanza (MPC) pamoja na waandishi wa vyombo mbalimbali,uliofanyika katika ukumbi mkubwa wa mikutano wa ofisi yake.

“Kukosa ushirikiano katika taasisi za serikali,nawaelekeza viongozi wote watoe taarifa kwa waandishi wa habari wanazozihitaji,wasizikalie,wazitoe wazipate kwa wakati bila kujali ni habari mbaya au nzuri,”amesema Makalla.

Amesema atatoa ushirikiano wa kutosha na katika kukabiliana na changamoto ya utandawazi,serikali itatoa taarifa haraka kuepuka upotoshaji unaofanywa hasa na mitandao ya kijamii na kutahadharisha,wasipozitoa waandishi wata ‘provoke’ na kuzitoa.

“Natakiwa kumuunganisha Rais Dk.Samia Suluhu Hassan na wananchi kupitia waandishi wa habari walio daraja kati ya serikali na jamii kwa kutangaza mazuri yaliyofanywa na serikali,upo umuhimu na mchango mkubwa wa vyombo vya habari katika maendeleo ya nchi,”amesema Makalla huku na akisistiza ukosoaji chanya unakubalika na hilo litafanyiwa kazi.

Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Mwanza (MPC),Edwin Soko akizungumza katika mkutano wa wana habari ulioandaliwa na Mkuu wa Mkoa huo,Amos Makalla.

Mkuu huyo wa Mkoa amesema takwimu zinaonesha Mwanza ni ya pili kwa wingi wa watu na kuchangia pato la taifa,hivyo mkakati na agenda yake ni kuufanya kuwa Mkoa wa kwanza katika kuchangia pato la taifa pia kitovu cha Kanda ya Ziwa na Ukanda wa Maziwa Makuu.

“Mwanza imependelewa kwa miradi ya kimkakati ya ujenzi wa daraja la J.P.Magufuli,SGR,meli ya MV.Mwanza,uboreshaji wa bandari na sasa ujenzi wa jengo la abiria lenye hadhi ya kimataifa,Rais amejitahidi sana na ameonesha dhamira ya kuufanya uwanja wa ndege wa Mwanza kuwa wa kimataifa,”ameeleza.

Makalla ameeleza zaidi kuwa mwelekeo wa pili ni mkakati wa kukuza utalii mkoani humo na tayari ameunda kikosi kazi cha kuandaa mkakati huo,ukikamilika utawashawishi watalii kuwa akishuka uwanja wa ndege wa Mwanza baada ya saa moja atakuwa amewaona wanyama katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na vituo vingine.

“Tunataka kukuza utalii lakini kuna mambo mengi yanatakiwa,rai yangu wawekezaji waje kuwekeza katika ujenzi wa kumbi kubwa za mikutano za kimataifa na hoteli za kitalii zenye hadhi ya kimataifa,”amesema.

Hivyo amewahimiza waandishi wa habari kutangaza vivutio vya Mwanza na kuifanya kitovu cha Kanda ya Ziwa.

Akizungumzia uchaguzi wa serikali za mitaa Makalla amewaasa waandishi wa habari kutanguliza uzalendo na maslahi ya nchi na kuifanya Tanzania kubaki salama baada ya uchaguzi huo kumalizika.

Amedai kalamu za waandishi wa habari zinaweza kuufanya uchaguzi huo ukawa salama na nchi ikabaki salama,hivyo kila mtu aangalie Tanzania kwanza na kutahadharisha kuwa nchi zilizoharibikiwa chanzo ni kalamu.

“Niwashukuru kuona mko tayari kwa uchaguzi,hivyo tutangulize uzalendo,uchaguzi utapita nchi na Tanzania ibaki salama,tutawapa ushirikiano na usalama wenu tutaendelea kuusimamia,”ameahidi Makalla.

Awali Mwenyekiti wa Chama Cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Mwanza (MPC),Edwin Soko amesema kupata taarifa katika taasisi za umma bado ni changamoto,wamegeuza utoaji taarifa ni hisani badala ya haki kwa mujibu wa Sheria ya Huduma ya Habari ya Mwaka 2016.

“Waandishi wa habari ni mdomo wa wasio na sauti na daraja kati ya wananchi na serikali,kazi zimeleta mabadiliko na matokeo chanya yaliyoleta maendeleo,bado sheria baadhi zinawakwamisha kutekeleza majukumu yao na tunamshuruku Rais Dkt.Samia ameridhia kufanyika maboresho kwa baadhi ya sheria kikwazo,”amesema Soko.

Kwa mujibu wa Soko, malengo ya MPC ni kufanya uandishi wa kuleta majawabu katika jamii badala ya kukosoa pekee,katika malengo ya maendeleo watazingatia miiko na kusimamia maadili ya taaluma.

Hivyo ameziomba taasisi zinazowatumia kuzingatia usalama wao na kuwapa vyombo bora vya usafiri.