May 27, 2022

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

RC Makalla atoa agizo kwa kampuni za usafi

Na Mwandishi wetu TimesMajira Online

Katika kuelekea uzinduzi wa Kampeni endelevu ya usafi Dar es salaam Disemba 04, Mkuu wa Mkoa huo Mhe. Amos Makalla amezielekeza Halmashauri za Mkoa huo kulipa Fedha za Wakandarasi wa taka kwa wakati ili kuondoa visingizio vya kutofanyika kwa Usafi na uzoaji wa Taka.

RC Makalla ametoa maelekezo hayo wakati wa kikao Cha pamoja na Wakandarasi wa Usafi na vikundi vya Usafi kilichoketi leo kuweka mikakati endelevu ya Usafi Dar es salaam.

Aidha RC Makalla ameelekeza Halmashauri hizo kuanza kutoa mikataba ya Muda mrefu kwa kampuni za Usafi tofauti na Sasa ambapo wanatoa mkataba wa mwaka mmoja Jambo linalopunguza ufanisi.

Hata hivyo RC Makalla amewataka Wakandarasi wa Usafi kuhakikisha wanatekeleza jukumu la kimkataba kwa kufanya Usafi na kuajiri Vijana Wenye uwezo wa kazi tofauti na Sasa ambapo baadhi wameajiri Wazee wa miaka zaidi ya 60.

Pamoja na hayo RC Makalla ametaka kila Mkandarasi kuwa na namba ya simu Mkurugenzi wa Manispaa husika na kutoa taarifa pindi wanapobaini Machinga wamerudi kwenye maeneo yaliyokatazwa na kuwazuia kutekeleza majukumu yao ya Usafi.

Sanjari na hayo RC Makalla ametoa wito kwa Wananchi kuunga mkono Kampeni hiyo kwa kufanya Usafi wa Kaya na Usafi wa kila Jumamos ya mwisho wa Mwezi.

Kwa upande wao Wakandarasi wa Usafi kutoka Manispaa za Mkoa huo wamemuahidi RC Makalla kuwa wamejipanga kuhakikisha mandhari Jijini inakuwa katika Hali ya Usafi huku wakieleza kukerwa na tabia ya baadhi ya Wanasiasa wanaojiingiza kwenye kamupni za Usafi.