December 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

RC Makalla amaliza mgogoro wa muda mrefu wa Boko Dovya kwa Somji

Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Amos Makalla amemaliza Mgogoro wa muda mrefu wa eneo la Dovya kwa Magufuli “Somji” uliokuwa ukiwakabili Wananchi ambao walivamia eneo na kujenga Baada ya Kuwapunguzia Bei thamani ya Soko kutoka Tsh 30,000 kwa Mita moja ya mraba iliyopangwa na Wizara ya Ardhi, Tsh 10,000 iliyopangwa na Halmashauri hadi kufikia Tsh 8,000.

RC Makalla ametoa tamka hilo la Serikali wakati wa kikao Cha pamoja na Wananchi hao ambapo ameelekeza Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni kukutana na Kamati ya Uongozi inayowakilisha Wananchi kuweka utaratibu wa malipo kwa wale walio tayari na muda wa kikomo Cha malipo.

Aidha RC Makalla amesema kwa wale watakaokamilisha Malipo wapatiwe hati zao haraka ili wawe huru Kuendeleza Makazi yao.

Hata hivyo RC Makalla pia ameelekeza kabla ya kufanyika kwa chochote Kamati ipite kila eneo na kuwahakiki Wananchi na eneo lake.

Maelekezo hayo ya RC Makalla yamepokelewa kwa mikono miwili na Wananchi hao ambapo wameshukuru punguzo kubwa la Bei walilopatiwa na wamepongeza Serikali ya awamu ya sita Chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwajali Wananchi.

Eneo la Dovya kwa Magufuli Lina ukubwa wa Square meter Milioni 1.4 ambapo Serikali imetenga zaidi ya Square meter laki mbili kwaajili ya huduma za kijamii ikiwemo Shule, Zahanati, Barabara, Makaburi, Soko, Viwanja vya michezo na Kituo Cha Daladala na Square meter 1.2 zinazobaki Ni kwaajili ya Makazi ya Wananchi.