February 21, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

RC.Kagera:Zaidi ya wahamiaji haramu 150, kila wiki urejeshwa kwao

Ashura Jumapili TimesMajira online, Kagera,

Serikali mkoani Kagera kila wiki imekuwa ikiwarejesha kwao zaidi ya wahamiaji haramu 150,ambao uingia mkoani humo kinyume na taratibu.Huku chanzo cha Mkoa huo kuwa na idadi kubwa ya wahamiaji haramu ni kutokana na kupakana na nchi za Uganda, Rwanda na Burundi.

Takwimu hizo za zimetolewa Februari 19,2025 na Mkuu wa Mkoa wa Kagera Hajat Fatma Mwassa, katika kikao cha Kamati ya Ushauri Mkoa ( RCC )kilichofanyika ukumbi wa Mkuu wa Mkoa Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba.

Hajat Mwassa, amesema kuwa, baadhi ya viongozi wa vijiji na vitongoji wamekuwa wakipewa fedha kidogo na wahamiaji hao hivyo kuwaruhusu kuingia nchini kinyume na na taratibu.

“Idadi ya wahamiaji haramu ni kubwa,tumeanza utaratibu wa kuwaondoa na kuwarudisha kwenye nchi zao ambapo kila wiki tunarudisha zaidi ya wahamiaji 150 kwenye nchi zao.Hii namba ni kubwa tunajiletea matatizo, niwaombe wadau wa kikao hiki mbariki mchakato tunaoendelea nao kwa manufaa ya kizazi kilichopo na kijacho,” amesema Mwassa.

Pia ameeomba kuungwa mkono na makundi yote ili kutokomeza tatizo la wahamiaji haramu,kwani Watanzania wanachukua vitalu kwa gharama ya chini wanawakodisha raia kutoka nchi jirani wanaingiza ng’ombe wengi matokeo yake wanaendelea kukaa na umaskini lakini wanaonufaika na vitalu ni wageni wakati vilitengwa vikawasaidie Watanzania.

“Nimeishafika eneo inapofugiwa mifugo, lakini ng’ombe walioko humo ni kutoka nchi jirani, Mwanakagera hanufaiki chochote ni kukimbizwa kimbizwa, hawalimi ardhi walioacha mababu wanaambiwa ni maeneo ya wafugaji,”amesema Mwassa na kuongeza:

“Hakuna faida yoyote wala mapato yanayoingia kupitia mifugo hiyo kwani wanapohitaji kuuza ng’ombe hao huwapeleka nchini mwao bila Serikali ya Tanzania kupata kodi.Madhara ya jambo hili ni pale walowezi hawa wataishi miaka mingi, watazaa wajukuu, watagombea uongozi katika ngazi mbalimbali na baada ya muda kadhaa watadai haki kama raia wa Tanzania,”.

Mbunge wa Jimbo la Bukoba Vijijini,Jasson Rweikiza,amesema wahamiaji haramu ni lazima wadhibitiwe maana wanapokuja nchini wanafuga, wanajenga nyumba, wanalima lakini wakiwa ni wahalifu.

Rweikiza amesema, wahamiaji wanapotoka hawana amani katika nchi zao hivyo wanakimbilia Tanzania katika kisiwa cha amani na bahati mbaya wakija wanakuwa hawana amani wanaleta vurugu wanaua watu.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe,Walles Mashanda, ameeleza kuwa licha ya changamoto ya wahamiaji haramu kusababishwa na viongozi wa vijiji na vitongoji lakini pia hata ngazi za juu pia kuna watu wanachangia.

Hivyo amemuomba Mkuu wa Mkoa kutembelea Wilaya yoyote yenye changamoto ya wahamiaji labda Ngara, Muleba au Karagwe, ukae na Wenyeviti wa vijiji na vitongoji na Watendaji wa vijiji uwaulize kwa nini tatizo la wahamiaji haramu linaendelea kuwepo.

“ Na sisi kuna sehemu tunachangia kwa kutowapa ushirikiano wa kutosha,kesi ziko wazi anakamatwa mhamiaji haramu anapelekwa ofisi za uhamiaji au ofisi yoyote, baada ya wiki mbili anarudi pale kijijini wakati anajulikana kwamba ni muhamiaji,” amesema Mashanda na kuongeza:

“Jambo hilo liliondoa imani kwa watu na lazima lifanyiwe kazi, hakuna kurudi nyuma hata wananchi wakishirikishwa kama wanaona ni njia ya ukweli watu watasaidia na kutoa ukweli,”.