March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

RC Kagera aweka wazi mafanikio ya Mkoa huo,serikali awamu ya sita

Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma

MKUU wa Mkoa wa Kagera Hajjat Fatma Mwasa  amesema kuwa Mkoa huo umepokea Jumla ya Tshs.Trilioni 1.131 katika kipindi cha mwezi Novemba, 2020 hadi Aprili, 2025 kwa ajili ya maendeleo ya sekta mbalimbali.

Mwasa amesema hayo jijini hapa leo,Julai Mosi,2025 wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya Serikali ya awamu ya Sita.

Amesema kuwa katika Sekta ya Afya, Jumla ya Tshs 146,340,236,113.41 zimetolewa ambapo Vituo vya kutolea huduma za afya vimeongezeka hadi 336 kutoka vituo 249. Ongezeko la vituo vipya 87.

Hospitali kutoka 3 hadi 11, mpya za Wilaya 8,vituo vya afya kutoka 29 hadi 42, vipya 13 na zahanati kutoka 217 hadi 283 na mpya 66

Katika Sekta ya Elimu,Mwasa amesema Jumla ya Tshs 128,054,003,364.69 zimetolewa
Ongezeko la miundombinu ya kutolea huduma ya elimu,Shule za awali na msingi kutoka 942 hadi 1,058, mpya 116,Shule za sekondari kutoka 224 hadi 292, mpya 68, zikiwemo shule mpya za amali (ufundi) tatu (3) na shule mpya ya bweni ya wasichana ya Mkoa ya Kagera River ambayo imegharimu zaidi ya Tshs. Bilioni 4.1

” Vyuo vya VETA vimeongeza kutoka vinne  hadi Tisa huku vitano vikiwa vipya, kikiwemo Chuo kipya cha VETA Mkoa cha Burugo kilichogharimu zaidi ya Tshs. Bilioni 20 na Ujenzi wa Chuo Kikuu cha Da es Salaam Kampasi ya Kagera unaendelea na kufikia asilimia 70,”amesema.

Akizungumzia Sekta ya Huduma ya Maji Mijini na Vijijini,amesema jumla ya Tshs. Bil. 184.8 zimetolewa ambapo hali ya upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama imeongezeka,Mijini hadi asilimia 93 kutoka asilimia 85 na Vijijini hadi asilimia 83 kutoka asilimia 76.

“Jumla ya miradi ya maji 41 imetekelezwa Vijijini 23 na Mijini 18 yenye thamani ya Tshs. Bilioni 164.7,”amesema.

Aidha ametaja baadhi ya miradi mikubwa iliyotekelezwa kipindi hicho Vijijini na Mijini kuwa ni Upanuzi mradi wa maji Bukoba Mjini, Tshs. Bil. 3.1 umekamilika.

Mradi wa maji Kyaka – Bunazi (Missenyi), Tshs. Bil. 15. 71 umekamilika,Mradi wa maji wa Miji ya Kayanga – Omurushaka (Karagwe), Tshs. Bil. 64.2 sawa na utekelezaji wa asilimia 64 na Mradi wa maji wa Kemondo (Bukoba Vijijini), Tshs. Bil. 4.57 sawa na utekelezaji wa 100%.

Vilevile amezungumzia Nishati ya Umeme,ambapo amesema jumla ya Tshs 103,376,838,198 zimetolewa  katika
Vijiji na Vitongoji ambapo Vijiji vyote 662 Mkoani vimeunganishwa na umeme sawa na asilimia 100 na Vitongoji 1,763 kati ya 3,665 vimeungwa umeme sawa na asilimia 48.

Pamoja na hayo amezungumzia Sekta ya Kilimo ambapo amesema Maendeleo ya zao la kahawa, Serikali imepunguza tozo katika zao la kahawa kutoka idadi ya tozo 17 hadi 5 pamoja na kuhakikisha kahawa inauzwa katika minada rasmi, hali hii imesababisha Uzalishaji umeongezeka kutoka tani 53,417 hadi tani 54,203 za maganda kwa mwaka na bei kwa kilo moja kupanda kutoka Tshs. 1,200 hadi Tshs. 4,200.