Na George Mwigulu Katavi
MKUU wa Mkoa wa Katavi, Juma Homera amewapa Polisi mkoani hapa saa 48 kumfikisha mahakamani mfanyabiashara raia wa China, Lin Guosong (34) ambaye anadaiwa kukataa kutii masharti ya kujikinga na ugonjwa wa Corona.
Homera alitoa agizo hilo jana kwa waandishi wa habari baada ya kukabidhiwa vifaa tiba vya kujikinga na Corona.
Vifaa hivyo vyenye thamani ya zaidi ya sh. milioni 25 vilitolewa na shirika la Walter Reed na vilikabididhiwa kwa RC Homera na Meneja wa Mradi Walter Reed (HJFMRI) Dkt. Shaban Ndama .
Alisema raia huyo wa china alikamatwa na Polisi Kijiji cha Kasansa wilayani Mlele mkoani Katavi na kisha kupelekwa katika Kituo cha Polisi cha Majimoto baada ya kukataa kutii kunawa mikono na maji yenye dawa .
Alisema raia huyo akiwa kwenye kizuizi alitakiwa na Kamati Maalumu ya Mkoa kunawa maji yenye dawa kwa ajili ya kujihadhari na maambukizi ya Corona, lakini alikataa, hivyo kukamatwa na Polisi.
Homera alisema baada kukamatwa aliagiza hati ya mtuhumiwa ichukuliwe na Polisi, hivyo anaitaka Polisi kumfikisha mahakamani ndani ya saa 48.
Aliwaonya watu wanaoishi kwenye makazi ya wakimbizi ya Katumba na Mishamo waliokuwa raia wa nchi ya Burundi ambao wamepewa uraia wa Tanzania kuacha tabia ya kuwapokea ndugu zao wanaotoka nchi ya Burundi.
More Stories
DC Korogwe awataka viongozi wa vijiji kuwatumikia wananchi kwa uadilifu
Premier Bet yamtangaza mshindi mkubwa
Dkt. Kazungu atembelea miradi ya umeme Dar es Salaam