Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online, Dodoma
MKUU wa Mkoa wa Dodoma Dkt.Binilith Mahenge ameziagiza Mamlaka ya Mipango Miji ya Jiji la Dodoma na kamati maalumu iliyoundwa kuchunguza mgogoro wa ardhi Kati ya wananchi wa mtaa wa Chigongwe na Kanisa la TAG kuleta hati zote zinazoonyesha umiliki wa ardhi hiyo.
Dkt.Mahenge ametoa agizo hilo Jijini Dodoma alipotembelea eneo hilo yenye mgogoro na kupokea ripoti ya kamati hiyo ambapo amesema anatoa siku kumi na nne (14) kwa Mamlaka hiyo na kamati kuleta hati za watu ambao wanamiliki eneo hilo kihalali.
“Nawapa siku kumi na nne(14) nataka mlete hizo nyaraka mimi nizione na nyingine ziende kwa Mkuu wa Wilaya ili tuthibitishe je ni kweli watu waliuziwa maeneo hayo wanamiliki ardhi hizo kihalali” amesema Dkt.Mahenge.
Pia Dkt Mahenge ameagiza Mamlaka ya Mipango Miji Jiji la Dodoma kwenda kupitia eneo hilo na kupima maeneo yote ambayo hayajapimwa na kumilikishwa watu kupima na kuwamilikisha kanisa la TAG kama eneo litakidhi uwekezaji wanaotaka kuwekeza.
”Mipango miji mpitie eneo hili lote mkitoa maeneo ya milima na maeneo yaliyomilikishwa wananchi kihalali linalobaki wapewe wawekezaji hawa na kumikikishwa bila gharama yoyote isipokuwa zilizopo kisheria” amesema .
Aidha amewataka wawekezaji hao ambao ni Kanisa la TAG kukubali kupokea eneo hilo litakalobaki huku akikiri kunaudhaifu ulifanyika na iliyokuwa Mamlaka ya ustawishaji Makao makuu CDA, hakuna Mamlaka inayoweza kufuta hati isipokuwa Rais pekee.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati maalumu iliyoundwa kuchunguza mgogoro huo Mhandisi Happiness Mgalula amesema kamati hiyo imepitia maeneo hayo na kukutana na pande zote mbili na kubainisha kuwa kuna nyaraka zinaonyesha Kanisa la TAG walipewa eneo hilo na uongozi wa Kijiji cha Chigongwe lakini kuna baadhi ya nyaraka hazikupatikana.
“Tumepitia maeneo yote na kubaini CDA iliomba andiko la mradi kwa Kanisa lakini hakuna nyaraka zinazoonyesha kuwa CDA ilijibiwa na kanisa japo kuwa kanisa linadai linanakala ya barua ya andiko walilotuma kwa CDA” amesema.
Naye Kaimu afisa Mipango Miji Jiji la Dodoma Emelye Chaula amesema kuna nyaraka zinaonyesha Kanisa lilipewa eneo lenye ekari 200 na kijiji lakini baada ya CDA kupima eneo hilo walikuta ekari mia tano sitini(560) na tangu siku hiyo Kanisa likajua linaekari 560.
Lakini Jiji kupitia wataalamu wake waligundua kuwa eneo hilo linaekari mia sita thelathini na tano point saba(635.7) wakaanza kujiridhasha kama kunaupimaji wowote uliwahi kufanyika na kubaini tangu mwaka 2013 kipindi cha CDA kuna taasisi nyingine na watu binafsi walipimiwa viwanja ndani ya viwanja hivyo vya kanisa.
Pia akabainisha kuwa baada ya kutoa maeneo hayo yaliyopimwa na kukuta ekari kama mia moja hamsini ndizo hazijapimwa katika eneo hilo.
Askofu wa TAG Jimbo la Dodoma Askofu Stephen Mahinyila amesema eneo hilo walipewa na uongozi wa Kijiji mwaka 2009 na baada ya hapo wakaanza kufuatilia nyaraka za umiliki kihalali kupikia CDA lakini mpaka sasa hawajafanikiwa huku eneo hilo likiwa limeuzwa baadhi ya maeneo.
More Stories
Madaktari wa Tanzania, Comoro waanza kambi kwa kishindo
Watakiwa kushirikiana kutikomeza matatizo ya lishe
CCBRT yazidi kuunga mkono juhudi za Rais Samia