May 18, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

RC Chalamila atangaza fursa,mkutano wa Jukwaa la  mfumo wa Chakula AGRF

 David John Timesmajira online

MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila ametoa wito kwa wananchi kutumia fursa zitakazoatikana kupitia  mkutano mkuu wa Jukwaa la Mifumo ya Chakula Afrika (AGRF) ili kuboresha shughuli za kilimo 

 Amesema mkutano huo ambao unatarajia kufanyika hapa nchini kuazia Semptemba 5 mwaka huu  utaleta matokeo muhimu katika uendelezwaji wa mfumo wa chakula  Afrika , ukuzaji wa sekta ya utalii,biashara na uwekezaji  ikiwemo  teknolojia mpya.

Mkuu wa mkoa Chalamila ameyasema haya leo Semptemba 1 kwenye ukumbi wa Mikutano wa kimataifa wa mwalimu Nyerere Jijini Dar es Salaam wakati akizungumzia maandalizi ya mkutano huo mbele ya waandishi wa habari

“Jukwaa la mfumo wa chakula la Afrika(AGRF) ni jukwaa kuu la kilimo linalowakutanisha wadau mbalimbali wa sekta ya kilimo ili kujadili na kuchukua hatua za kiutendaji katika kiboresha upatikanaji na usalama wa chakula na lishe kwa ujumla,”amesema Chalamila 

Chalamila ameongeza kuwa  mkutano huo utawakutanisha wadau mbalimbali wakiwemo wazalishaji, wawekezaji, na wafanyabiashara.hivyo nivema wananchi  hususani wajasiliamali wakatumia fursa hiyo.

Amesema wakazi wa Dar es Salaam wanapaswa kuchangamkia fursa zitakazotokana  mkutano huo  kwa lengo la kuongeza uzoefu na kujifunza teknolojia za kisasa ili kutimiza malengo ya Rais Dk.Samia Suluhu Hassan ya kulisha dunia.

Pia Chalamila amewataka wakazi hao  kudumisha usalama,amani  ukarimu na usafi katika kipindi  chote cha mkutano huo ili kuweka taswira ya nchi vizuri.

Kwa upande wake mkurugenzi mtendaji wa kituo Cha mikutano Cha Julius Nyerere JNICC Ephrahim Mafuru amesema serikali inatatarajia kupokea wageni  zaidi  3000 wa masuala ya kilimo jumla ya sh. Bilioni 12.5 zimetolewa kwa ajili ya maandalizi ya mkutano (AGRF).

 Amesema  JNICC wamejipanga kuwahudumia wageni hao kwa kutenga jumla ya kumbi 27 ambazo zote maandalizi yake yamekamilika.

“Mchango wa kituo katika mnyororo wa thamani hivyo serikali kwa kushirikiana na AGRF imejipanga kwa bajeti ya bilioni 12.500 na fedha hizo ni maandalizi ya mkutano ambazo zitaingia katika mnyororo wa thamani wa maandalizi na gharama za kuuendesha mkutano huo,”amesema.

Aidha Mafuru ameongeza kuwa zaidi ya vyumba 2600 vya hoteli vimeandaliwa kwa ajili  ya wageni hao hivyo amewaomba Watanzania kuwakarimu wageni hao kwani mchango wao ni mkubwa kwa taifa.

Hata hivyo Mafuru amewataka wajasiriamali watakaopata nafasi ya kushiriki mkutano huo watumie fursa hiyo kukutana na wajasiriamali kutoka nje ya nchi ili kubadilishana uzoefu.

Mkutano huo unatarajia kufanyika nchini Septemba 05 hadi 08,mwaka huu katika ukumbi wa kimataifa wa mikutano wa Julius Nyerere jijink Dar es Salaam na utazinduliwa na Rais Dk.Samia