November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

RC Chalamila ahimiza kazi, ataka wanasiasa kubadilika

Na Esther Macha,Timesmajira,Online,Mbeya

MKUU wa Mkoa wa Mbeya ,Albert Chalamila ameshauri Watanzania kuhama kwenye ubishi wa kisiasa wa maneno matupu na badala yake kufanyakazi kwa vitendo.

Amesema kuwa aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Magufuli alisisitiza kufanya kazi na kuleta maendeleo na sasa Rais Samia Suluhu Hassan naye amesisitiza hayo.

Kwa msingi huo amesema ni jukumu la kila mmoja kufanya kazi kwa bidii kama ambavyo viongozi wanasisitiza ili kazi zinazofanywa ziweze kufanikiwa na kuleta matokeo mazuri.

Chalamila amesema hayo juzi wakati alipotembelea na kukagua utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa Hospitali ya Wilaya Igawilo unaondelea .

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya ,Albert Chalamila

Amesema siasa ya kweli ni kuona majengo yanajengwa, barabara zinatengenezwa na sio maneno matupu.

“Hameni kwenye maneno fanyeni kazi kwa bidii ili muweze kusonga mbele. Jukumu letu sote hapa ni kufanya kazi kwa bidii,” amesema.

Amewataka wakuu wa idara waliopewa dhamana ya kusimamia ujenzi huo wa hospitali kujenga uaminifu na kazi ifanyike kwa ufanisi mkubwa .

“Ndugu zangu wakuu wa idara ni raia yangu kwenu kuhakikisha mnasimamia vizuri ujenzi huu,”amesema Chalamila.

Akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi huo wa Hospitali Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya, Dkt.Jonas Lulandala amesema Halmashauri ya Jiji la Mbeya ilipokea sh. Bil.1 kutoka Serikali kuu Mwezi Machi kwa ajili ya kuendeleza ujenzi wa hospitali ya Wilaya Igawilo .
Naye Diwani wa Kata ya Iganjo, Eliud Mbogela amesema wananchi wa kata hiyo wamekubali mradi uendelee ila wana changamoto ya barabara ambayo imekatiza ndani ya mradi huo.