January 12, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

RC Chalamila ahairisha ziara, kuomboleza kifo cha Lowasa

Na Agnes Alcardo, Timesmajira Online.Dar

MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, Februari 12, 2024 ametoa taarifa kwa umma kupitia vyombo vya habari ofisini kwake kuhusu kuhairisha ziara yake ya kukagua na kusikiliza kero za wananchi katika Wilaya zote za Mkoa huo.

Ziara ambayo ilipangwa ianze leo, Februari 12, Mwaka huu katika Wilaya zote akianza na Wilaya ya Temeke,ameahirisha ili kuungana na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, familia na Watanzania wote kufuatia kifo cha Waziri Mkuu Mstaafu Edward Ngoyai Lowassa

Akiongea na waandishi wa habari, Chalamila amesema kwa kuwa msiba wa Waziri Mkuu Mstaafu Hayati, Edward Ngoyai Lowassa upo mkoani humo, Mkoa umejipanga katika nyanja zote ikiwemo usalama na uratibu wa wageni mbalimbali kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu ambaye ndiye mratibu mkuu wa msiba huo.

Aidha, Chalamila amesema siku ya kesho Februari 13, mwili wa marehem Edward Lowassa utaagwa katika viwanja vya Karimjee vilivyopo Ilala, ambapo ametoa rai kwa wakazi wa Mkoa huo na Watanzania kwa ujumla kutumia siku hiyo kuja kwa wingi kumuaga aliyekuwa kiongozi mstaafu.

Pia amesema, Februari 14, Mwaka huu mwili utapelekwa katika kanisa la Azania Front kwa ajili ya Ibada, na Februari 15, mwaka huu mwili wa marehemu utasafirishwa kuelekea nyumbani Monduli- Arusha ambapo maziko yanatarajiwa kufanyika Februari 17, Mwaka huu ambayo yataongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Sambamba na hilo, Chalamila amesema ziara hiyo itaanza rasmi Februari 19, 2024 Wilaya ya Temeke Jimbo la Mbagala Februari 20,024 Jimbo la Temeke, Wilaya ya Kinondoni, Februari 21,2024 Jimbo Kawe Februari 22,2024 Jimbo la Kinondoni.

Huku Wilaya ya Ubungo Februari 23,2024 Jimbo la Ubungo, Februari 24,2024 Jimbo la Kibamba, Wilaya ya Kigamboni Februari 26-27,2024 na Wilaya ya Ilala Februari 28,2024 Jimbo la Ilala, Februari 29,2024 Jimbo la Ukongo na kuhitimisha Machi 01,2024 katika Jimbo la Segerea.